Thursday, 5 July 2012

[wanabidii] Wabunge hawa ni mfano wa kuigwa

Tunawapongeza wabunge kutoka kamati za Kudumu za Bunge za Huduma za
Jamii, Katiba, Sheria na Utawala na ile ya masuala ya UKIMWI kwa
kukubali kukutana na kusilikiza maoni na mapendekezo ya Sikika, bila
kudai posho.

Sikika ni shirika lisilo la kiserikali lililosajiliwa nchini Tanzania
kwa lengo la kufanya utetezi katika utoaji na upatikanaji wa huduma
bora za afya kote nchini. Kwa kipindi cha miaka mitano sasa, Sikika
imekuwa ikikutana na Wabunge na kuwasilisha matokeo ya tafiti
mbalimbali na uchambuzi wa bajeti. Tafiti hizo, pamoja na mambo
mengine, zimekuwa zikionesha jinsi ufanisi katika mgawanyo wa
rasilimali unavyoweza kusaidia kuboresha utoaji na upatikanaji wa
huduma bora za jamii.

Kwenye mikutano ya awali, Sikika ilikuwa ikigharamia malipo ya posho
kwa wabunge, jambo ambalo liligharimu shirika fedha nyingi na kuathiri
shughuli nyingine za jamii.Sikika imekuwa ikipinga matumizi yasiyo
lazima ya fedha za umma, ikiwamo malipo ya posho za vikao. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba, Wabunge wana jukumu la kukusanya na
kuwasilisha maoni ya wananchi kwa Serikali. Kwa muktadha huo, mwaka
jana (2011), shirika lilielezea masikitiko yake na kutoridhishwa na
tabia ya kudaiwa kuwalipa posho Wabunge kwa kazi ambazo wanapaswa
kuzifanya.

Tofauti ni miaka ya nyuma, hivi karibuni, Wabunge kutoka kamati hizo,
walijitokeza kwa nyakati tofauti na kushiriki kikamilifu kwenye
mikutano ya Sikika, huku wakifahamu kwamba hakutakuwa na malipo ya
posho. Tulifurahishwa pia na ushirikiano na usikivu wa wabunge wa
kamati hizo ambao walipokea matokeo na mapendekezo ya tafiti zetu na
kuahidi kuzifanyia kazi katika Bunge la bajeti litakaloanza Juni 12,
2012.

Tunawapongeza sana wenyeviti wa Kamati hizo, Mh. Margareth Sitta-
(Huduma za Jamii), Mhe. Pindi Chana- (Katiba, Sheria na Utawala) na
Mhe. Lediana Mngo'ng'o- (Masuala ya UKIMWI) ambao wameonesha kuelewa
na kuthamini mchango wa tafiti zinazofanywa na asasi za kiraia.
Sikika tunaamini kwamba matokeo ya utafiti yanawasaidia wabunge kupata
takwimu, picha halisi, kuwa na uwezo wa kujadili na kupendekeza namna
ya kukabili changamoto mbalimbali katika kuboresha huduma za jamii
nchini.

Asasi za kiraia kama Sikika na watanzania wamekuwa wakiguswa na suala
la ulipaji wa posho kwa wabunge wakati wanalipwa mishahara.Tunaamini
kwamba wabunge wanaweza kutimiza wajibu wao bila kulipwa posho.
Vilevile, kwa kuzingatia nafasi yao ya uwakilishi, Wabunge waisaidie
Serikali kuokoa fedha zinazotengwa kwa ajili ya posho na kuzielekeza
katika maeneo yatakayowanufaisha wananchi wengi, kama vile afya na
elimu.

Mr. Irenei Kiria

Mkurugenzi wa Sikika, P.O. Box 12183 Dar es Salaam,

Simu: +255 222 666355/57, Faksi: 2668015, Barua
pepe:info@sikika.or.tz, Tovuti: www.sikika.or.tz

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment