Thursday, 5 July 2012

[wanabidii] WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI KUANZA ZOEZI LA KUHAKIKI VYAMA VYA KIJAMII

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, itaanza zoezi la kutembelea na
kuhakiki Vyama vya Kijamii ambavyo vimesajiliwa na Wizara hiyo ili
kuhakikisha kuwa vyama hivyo vinafanya shughuli zake kwa mujibu wa
matakwa ya Sheria ya Usajili wa Vyama.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Vyama vya Kijamii
katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Numbilya Mpolo amesema leo
kuwa zoezi hilo litaanza mwezi Agosti mwaka huu.

Akizungumza katika Banda la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika
Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo
Maonyesho ya 36 ya Biashara ya Kimataifa yanaendelea, Mpolo alisema
mambo yatakayokaguliwa ni uhai wa Vyama hivyo na utekelezaji wa Katiba
zake kama zilivyosajiliwa.

Mambo mengine yatakayokaguliwa ni kama Vyama hivyo vinalipa ada ya
kila mwaka kwa mujibu wa Sheria, na pia utekelezaji wa matakwa ya
Sheria ya kufanya vikao vya Chama na kuandaa taarifa za fedha ambazo
zinapaswa kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama kila mwaka.
Amesema hatua za kisheria zitachukuliwa kwa vyama vitakavyobainika
kukiuka masharti ya Sheria za uendeshaji wake, ikiwa ni pamoja na
kupewa notisi za kusudio la kufuta chama husika.

Kwa mujibu wa Sheria za Vyama, chama kitapewa notisi ya kusudio ya
kukifuta, na ikiwa hakitatoa hoja kwa nini kisifutwe, ndani ya siku
21, basi Msajili wa Vyama anaweza kutoa notisi ya kukifuta chama, na
baadaye kutoa tangazo la kukifuta chama hicho, katika Gazeti la
Serikali.

Akizungumzia kuhusu malalamiko yanayopokelewa na Msajili wa Vyama,
Mpolo amesema ni pamoja na taarifa za migogoro inayotokana na kugombea
madaraka na pia ubadhirifu wa fedha katika baadhi ya vyama.

Kuhusu Vyama ambavyo vinabadilisha Katiba zao bila mabadiliko hayo
kukubaliwa na Msajili, amesema Katiba kama hizo hazitambuliki
kisheria.Amesema hadi sasa jumla ya Vyama vya Kijamii 6,469
vimesajiliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kati ya hivyo 875
ni Taasisi za kidini.

Amesema zoezi la kusajili Vyama vya Kijamii bado linaendelea na
wananchi wenye mahitaji ya kusajili hivyo wanaweza kuwasiliana na
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakati wowote ili kupata huduma hiyo.

(Background)
Usajili wa vyama vya Kijamii unafanywa chini ya Sheria ya Vyama, Sura
ya. 337 iliyofanyiwa Mapitio mwaka 2002.

Sheria hii inatoa maelezo muhimu kuhusu Vyama hivi, ikiwa ni pamoja na
kufafanua kanuni na mwenendo ambayo Vyama hivi vinatakiwa kuufata.
Vyama vya Kijamii ambavyo vinasajiliwa chini ya Sheria ya Vyama vya
Kijamii ni pamoja na Vyama vya Kidini, Vyama vya Maendeleo ya Kijamii,
Vyama vya Kimataifa na Vyama vya Kitaalamu.

Baadhi ya mahitaji ya Vyama kuweza kusajiliwa ni pamoja na:
· Kuwa na wanachama waanzilishi wasiopungua,
· Katiba ya Chama,

· Majina na maelezo binafsi (CV) na picha za viongozi wa
Chama,
· Barua kutoka Mamlaka ya inayohusika kutambua Chama,
inayotambuliwa kisheria, kwa mfano, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa
Wilaya, au Wizara Mama,
· Barua toka kwa Mwombaji (anayetaka kusajili Chama).

Baada ya kukamilisha vigezo vilivyotajwa hapo juu, na vinginevyo
kufuatana na Sheria ya Usajili wa Vyama, Sheria inasema, Msajili wa
Vyama, akiridhika na malengo ya kuanzishwa kwa Chama husika, atafanya
usajili wa Chama hicho, huku akitilia maanani matakwa umma na taifa
kwa ujumla.

Usajili wa Chama, katika mazingira ya kawaida, unachukua siku tano
hadi 7 na wakati mwingine unaweza kuchukua muda mrefu kutegemeana na
aina ya Chama, ambapo wakati mwingine itahitaji uchunguzi wa kina
zaidi kabla ya kusajiliwa.

MWISHO

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment