Wakati Bunge liko kwenye mchakato wa Bajeti ya 2012/13, yameanza
kujitokeza maneno na taarifa mbalimbali juu ya kupanda kwa mishahara
ya watumishi wa Umma wakiwemo Wabunge. Mathalani, siku ya Jumatano
tarehe 20 Juni 2012, gazeti moja linatokalo kila siku lilikuwa na
habari yenye kichwa kisemacho "Mishahara ya Wabunge juu".
Ofisi ya Bunge imeona ni vyema kutoa ufafanuzi juu ya suala zima la
mishahara ya Wabunge ili umma uweze kuelimika ipasavyo juu ya taratibu
zinazotawala jambo hili kama ifuatavyo:
· Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo inajumuisha Fungu Na.
42 lenye Bajeti ya Bunge bado haijasomwa Bungeni, na hivyo haiwezekani
leo hii kueleza kuwa kuna nyongeza ya bajeti inayohusu mishahara kwa
Wabunge.
· Si kweli kwamba mishahara ya Wabunge imeongezwa toka kiwango
wanacholipwa sasa, kwa kuwa mishahara yao kama ilivyo ya watumishi
wote wa umma, hurekebishwa kwa waraka maalum toka Ofisi ya Rais, na
si Kamisheni au Kamati yoyote ya Bunge.
· Waraka wa mwisho wa toka Ofisi ya Rais unaotoa Masharti ya
Kazi ya Mbunge ulitolewa tarehe 25 Oktoba 2010, na kueleza kuwa Mbunge
atalipwa mshahara katika ngazi ya LSS (P) 2, na ni waraka huo
unaotumika mpaka sasa.
· Mapendekezo ya ongezeko la 32% ya Bajeti ya Ofisi ya Bunge
yaliyooneshwa kwenye kitabu cha Bajeti namba 2, cha matumizi ya
kawaida yaliyowasilishwa mezani ni ya matumizi mengine ambayo hayana
uhusiano na ongezeko la mishahara.
Mwisho, Ofisi ya Bunge wakati wote inathamini sana mchango wa vyombo
vya habari katika juhudi za kuelimisha umma juu ya kazi za chombo chao
cha uwakilishi. Hata hivyo, Ofisi inasikitishwa sana na habari za
upotoshaji zinazotolewa kwa lengo la kujenga chuki kati ya Wabunge na
watu wanao wawakilisha.
Kwa mantiki hiyo, tunazidi kuwasihi Waandishi waandike habari au
makala baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu jambo husika na pale
inapobidi waweze kupata ufafanuzi toka Idara husika katika Ofisi ya
Bunge, ili kuepuka kuupotosha umma.
Imetolewa na:
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ya Bunge,
S.L.P 941, DODOMA.
21 Juni 2012
--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
0 comments:
Post a Comment