Wednesday, 6 June 2012

[wanabidii] UDINI NA UTANZANIA:TULIPOTOKA,TULIPO,TUELEKEAPO


----- Forwarded Message -----
From: Blogger <no-reply@blogger.com>
To: chambi78@yahoo.com
Sent: Wednesday, June 6, 2012 6:30 PM
Subject: [UDADISI: Rethinking in Action] UDINI NA UTANZANIA:TULIPOTOKA,TULIPO,TUELEKEAPO



MCHANGO WA MOBHARE MATINYI KATIKA MJADALA WA UDINI

Naomba nichangie hapa kama Mtanzania - na si kama mwislamu au mkristo
au mpagani.

1. Kwanza ni kweli kwamba kitabu cha yule padri mzungu kinaleta shida
sana mawazoni mwa watu, Dkt. Sivalon. Lakini turejee kwenye ukweli wa
kisomi, kwamba huwezi kuhitimisha jambo zito kwa kutumia chanzo
kimoja. Hatuna maandiko mengine ya watu wasiokuwa na upande
yanayothibitisha aliyosema bwana huyu. Hakuna utafiti wowote. Aidha,
ni muhimu pia kuchunguza kujua alisema hivyo katika mazingira gani.
Kuna Mkenya mmoja London aliwahi kuzuliwa na wenzake kwamba ni shoga
na akatengwa kabisa. Aliyemzulia siku moja akamwambia Mkenya mwingine
ninayemfahamu, kwamba anajua fika kuwa bwana yule si shoga lakini
alifanya vile kumlipizia kisasi cha ugomvi wao. Uongo ulibadilishwa
kuwa ukweli. Je, tuna hakika na maneno ya huyu mwandishi padri? Najua
ukivutia upande mmoja itabidi useme uhakika upo kwa sababu kuna
uthibitisho mwingine, lakini hali halisi inagoma. Nitaeleza.

2. Pili, ingawa Mwalimu Julius Nyerere analaumiwa sana na waislamu au
watetezi wa waislamu, lakini kiukweli kama si yeye, hali ya kielimu ya
waislamu nchini ingekuwa mbaya sana. Tusisahau kuwa, tulipopata uhuru
serikali ya Mwingereza hakituachia shule za kutosha. Wakristo na dini
za Waasia wakiwemo Wabohora, Waismailia na Wahindu walikuwa na shule
lakini Waislamu hawakuwa na shule. Sasa ukumbuke pia kuwa, wakoloni wa
Ulaya walikuja Afrika Mashariki kwenye karne ya 19 wakati wakoloni wa
Uarabuni walikuwa tangu karne ya 13. Kwa miaka 600 Waarabu hawakujenga
shule hata moja; bali walijenga madrasa kwa ajili ya masomo ya dini - jambo ambalo hakuwa dhambi.
Shule za kwanza zilijengwa Tanganyika na Mjerumani zikiwa ni za darasa
la kwanza hadi la nne kwa kutumia Kiswahili. Zanzibar zilijengwa sana
sana na Mwingereza. Tafuta maana na historia ya maneno haya: (i)
Darasa/Madarasa (ii) Shule (iii) Skuli. Kimsingi, Nyerere ndiye
aliyezitaifisha shule za wasiokuwa waislamu ili na watoto wa waislamu
waende kusoma kwa sababu walikuwa wanakwepa kubadilishwa dini na
kulishwa nguruwe ingawa wakristo wengine kama wasabato hawali nguruwe.

3. Nchi yetu ikapiga hatua zaidi na tukaanza kujenga shule za msingi.
Nyerere akajenga shule kwa juhudi kubwa zaidi kwenye mikoa iliyokuwa
nyuma, ambayo mingi ilikuwa ni ya pwani waliko waislamu wengi zaidi.
Haikutosha, baada ya Nyerere kuibana mikoa mingine, ambayo wananchi
wake waliamua kujijengea wenyewe, akaweka nafasi maalum kwa watu wa
makabila ambayo hayakuwa na watoto wengi shuleni, yaani hayakuwa
yanataka shule. Waliofaidika zaidi ni makabila ya pwani ambako shule
ilikuwa kama kituo cha polisi kwao. Dini yao wengi wao tunaijua.
Mwalimu akiwa anaongoza TANU na CCM akajenga shule za jumuiya ya
wazazi kwenye mikoa ya pwani na hata alipopata msaada kutoka Kuba
(Cuba), aliichagua mikoa ya pwani pia kujengewa shule, na ndipo
tukapata shule kama Kibiti, Ruvu, n.k. Hata ile ya Waswidi ilijengwa
Kibaha. Alifanya hivi kuwasaidia hao mnaowaita waislamu (mimi nawaita
Watanzania). Kule kwingine kama Kilimanjaro, wakaamua kujenga shule za
binafsi zao wenyewe na ndio maana hadi leo wanazo nyingi. Serikali ya
Nyerere haikujenga shule za sekondari kule bali ilijenga hizo chache kwenye mikoa
yenye waislamu wengi. Ndio ukweli huo ila watu hawataki kuutafuta.
Rekodi zipo, tafuta shule zote uone.

4. Serikali ya Tanzania haikuishia hapo. Wakati wa Rais Mwinyi
waislamu wakiongozwa na Waziri Kighoma Malima walilalamika sana.
Zikafanyika juhudi nyingi ikiwemo kumweka Malima kwenye sehemu kama
elimu ambapo alianzisha awamu mbili za kwenda shule, lengo likiwa
kuongeza idadi ya watoto wa kiislamu wanaoingia sekondari ingawa na
wakristo pia waliongezeka. Pia Tanzania ikapata nafasi za masomo
kwenye mataifa ya Misri, Algeria, Iran, na Uturuki, maalum kwa ajili
ya waislamu tu. Marafiki zangu walikwenda huko na walinithibitishia
kwamba hii ilikuwa maalum kwa waislamu tu. Bado Waislamu waliendelea
kwenda nchi zingine zisizokuwa za kiislamu bila tatizo. Huu ulikuwa
msaada mkubwa.

5. Ikaja serikali ya Ben Mkapa na yenyewe ikaweka rekodi ya kuipa dini
moja majengo ya chuo kikuu. Leo hii kipo chuo kikuu cha waislamu
Morogoro kwa kutumia majengo ya serikali. Serikali ya JK imejenga shule
nyingi sana za sekondari nchi nzima na sijasikia ubaguzi kwa upande wa
mikoa yenye waislamu wengi. JK pia amehakikisha waislamu wanaongoza
wizara ya elimu ili kuondoa malalamiko, na si kweli kwamba eti
asiyekuwa mwislamu akiwa waziri wa elimu, basi waislamu wanashindwa
kusoma. Hakuna ukweli hapa.

6. Najua kuna malalamiko mengi kuhusu shule na hata hospitali za
misheni, lakini tuzitendee haki. Hizi ni za kuhudumia Watanzania wote,
na ndiko Kikwete na binti yake waliposoma, hata Mzee Makamba. Tuweni
wakweli kwenye hili. Waislamu wanatibiwa kote huku, na ruzuku ndiyo
mkombozi wa Mtanzania mnyonge.

WAISLAMU KWENYE VYEO NA ELIMU

7. Labda, tuje kwenye hili moja: KWA NINI HATUNA WAISLAMU WENGI KATIKA
NAFASI ZA JUU SERIKALINI? Hili jambo ni la kweli lakini inabidi
tujiulize swali jingine zaidi: KWA NINI KUNA MADAI KWAMBA WAISLAMU
HAWAJASOMA?

8. Nianze na historia yetu. Waarabu walipokuja kwenye karne ya 13
walileta vitu kadhaa vikuu vikiwa ni dini nzuri ya Kiislamu na pili
utamaduni wao wa kishenzi. Ndiyo, walileta utamaduni wa kishenzi.
Utamaduni wa Kiarabu siyo dini ya Kiislamu na dini ya Kiislamu siyo
utamaduni wa Kiarabu. Uislamu ndio ulioongoza elimu duniani kwenye
karne ya saba na nane na hata vyuo vikuu vya kwanza duniani vilikuwa
vya Waislamu, lakini si Waislamu wote hupenda elimu, kama ilivyo kwa
dini zote zingine pia. Ukienda kwenye nchi za Maghrebu na baadhi ya
Mashariki ya Kati, yaani Moroko, Algeria, Tunisia, Misri na zile za
Uturuki, Siria, Iraki na Yodani, kuna waislamu wengi wenye elimu. Hapa
Marekani wanaheshimika, mathalani, wahandisi mahiri hutoka Uturuki,
Pakistan na India kwenye majimbo yenye waislamu.

9. Hali ni tofauti kabisa kule Ghuba kwenye nchi za Saudia Arabia,
Yemeni, Kuwaiti, Omani, Katari, Imarata na Bahraini. Ghuba watu
hawataki shule. Hawa wa Ghuba ndio walioletea ushenzi wao huu Afrika
Mashariki kuanzia kule Somalia hadi Msumbiji kaskazini - kote huku
kuna watu wenye utamaduni wa Ghuba wa kukataa shule. Hili liko wazi.
Kwa kuwa Waarabu wa Ghuba ndio walioleta pia Uislamu, basi watu
hujumuisha kwa pamoja tatizo la kukosa elimu kwa sababu za kuiga
utamaduni wa Ghuba na dini nzuri ya kiislamu ambayo inajali elimu
sana. Saudia watu ni vilaza watupu kiasi kwamba kuna Wamisri milioni
moja na zaidi wanaofanya kazi za kisomi. Kote huko Ghuba kasoro Yemeni
na Omani (kwa sababu ya umaskini wao) kuna wageni wengi ndani ya nchi
kuliko wenyeji kwa sababu watu hawataki shule.

10. Waislamu wa pwani ya Tanzania, kama wenzao wote wa Somalia yote,
Lamu, Malindi, Mombasa, Zanzibar, Mafia, Kilwa, Lindi na Pemba ya
Msumbiji, wana utamaduni wa Waarabu wa Ghuba wa kugomea shule. Tofauti
na wenzao, waislamu wa Tanzania walioko Machame na Usangi mkoani
Kilimanjaro, au Bukoba, na hata wale wa kabila la Waganda (Baganda) kule Uganda,
wao wanapenda shule. Maeneo yote waliyokaa Waarabu, kuanzia Bagamoyo
nenda hadi Tabora/Nzega, na Ujiji, shule si mali kitu. TATIZO SI
UISLAMU BALI UARABU WA GHUBA. Anayebisha hongera zake.

11. Tafiti mbili ninazozijua, nitazisaka baadaye, zinasema kwamba
kwenye miaka ya nyuma kama ya 1990, pale UDSM waislamu walikuwa ni
kati ya 14 - 15% ya wanafunzi wa shahada ya kwanza wote. Hiki ni kiasi
kidogo mno lakini ni kidogo cha kiasi gani? Lazima tujue hili nalo,
hata kwa makadirio tu.

12. Nyerere aliamua tuachane na sensa ya kupekua dini za watu kwa
sababu nzuri kabisa - alitaka Watanzania tusitambuane kwa dini zetu
(na makabila pia). Hivyo, ili kuweka usawa tukaanzisha msemo huu:
Tanzania sisi nusu ni Waislamu na nusu ni Wakristo. Huu ni msemo tu na
hauna usahihi. Pili, hata kama sensa ya zamani ilionesha kwamba
waislamu ama wakristo au wapagani ndio wengi, haina maana yoyote leo
wakati taifa letu lina watu milioni 45 hivi. Tulipata uhuru tukiwa
milioni 12 na baadaye Zanzibar ikaongeza laki tatu. Watanzania
hatukuwa na kelele za asilimia ngapi ni dini hii na ile. Leo zimerudi.

13. Kwa mujibu wa taarifa za kitafiti (siyo mimi), Waislamu nchini
Tanzania ni theluthi moja ya watu wote. Naomba Nasser na Salim muende
mkamuulize rais wetu, Jakaya Kikwete, kwamba kwa nini alipoteua
mawaziri mwaka Novemba 2010 aliweka theluthi moja waislamu, na kisha
manaibu akafanya hivyo hivyo? Pia, muulizeni, kwa nini alipoteua
mawaziri hii juzi, aliweka 1/3 waislamu na kwenye manaibu akafanya
hivyo hivyo? Kabla hamjaenda, chukueni rekodi zenu kwanza muone. Jiulizeni pia, kwa nini wajumbe wa Tume ya Kupitia Katiba ya Muungano, wale wa Bara, theluthi moja tena ni waislamu? Rais
Kikwete, nijuavyo mimi, anajaribu sana kuliangalia hili suala la
kelele za dini ili asiharibu nchi yetu. Anakuwa mwangalifu sana, hata
kama kuna wakati anateleza. Je, mahesabu yake haya yana maana gani?
Nina hakika anajua anachokifanya na kamwe hawezi kuwaonea waislamu
wenzake ambao ni Watanzania kama yeye. Hawezi kufanya uonevu.

14. Zifuatazo ni taarifa zinaonesha idadi ya waumini wa kiislamu
nchini Tanzania:
(i) 35% = http://www.qran.org/a/a-world.htm.
(ii) 29 - 35% =
http://en.wikipedia.org/wiki/List_of_countries_by_Muslim_population or
The Future of the Global Muslim Population (Pew Research Center),
http://pewforum.org/future-of-the-global-muslim-population-preface.aspx.
(iii) 35% = http://www.state.gov/j/drl/rls/irf/2010_5/168434.htm.

15. Hiyo taasisi ya kwanza ni ya kiislamu. Sijaweka za Wakristo kwa
sababu sitafuti ushindani na siamini kama idadi ina maana yoyote,
lakini kwa kuwa watu mnataka kupigia kelele, basi mzigo huo hapo.
Mwaka jana mwanaharakati mmoja wa Tanga alikuja Marekani na akasema
mkutanoni kwenye chuo kikuu kimoja kwamba waislamu ni 70% ya
Watanzania wote, na pia kuna mwislamu mmoja mwenyeji wa Songea
aliandika makala ya kitaaluma na akasema kwamba waislamu Tanzania ni
55% lakini akashindwa kueleza wanaishi wapi. Huyu wa 70% alishindwa
pia kusema wanakaa wapi ambako hawaonekani. Pointi ni kwamba madai
haya ni ya kijinga. Makala nyingine iliyoandikwa na msomi huyu
Mtanzania ilisema kwamba Uganda wapo 45% na Kenya 33% na Msumbiji 40%
(kama sijakosea). Hakuna popote duniani, hata kwenye mashirika ya
kimataifa ya kiislamu zinapotajwa namba hizi za 55% kwa Tanzania na
hao wengine wa Afrika Mashariki. Mashirika ya kiislamu yanasema kwamba
Tanzania ina 30 - 35% tu. Ili kuleta amani, naomba tuseme kwamba
Tanzania haina Wakristo kabisa, hata mmoja hayupo isipokuwa wale wenye
madaraka serikalini. Tukumbuke pia, marais wetu wote watano wa sasa
(kule Zenji na kwenye Muungano) ni waislamu.

16. Kwa nini idadi inakuwa muhimu hapa, achilia mbali kelele? Ni kwa
sababu tunataka kuielewa ile 14-15% ya UDSM ambayo huenda hivi leo
imeshabadilika kwa kuwa tuna vyuo vingi nchini. Tunahitaji maelezo,
kwamba hao waislamu wengine wameishia wapi? Jibu lake linarudi kwenye
ule UTAMADUNI WA WAARABU WA GHUBA. Hakuna mwislamu anayeonewa wala
anayenyimwa shule. Mimi nimekulia na kusomea Dar es Salaam kwenye waislamu wa kutosha kuanzia
darasa la kwanza hadi kidato cha sita, na JKT kabisa. Waislamu wote
marafiki zangu waliokuwa wakali darasani waliendelea na elimu ya juu.
Shule ya msingi tulikuwa watoto wanne machachari, mimi, Waziri, Salum
na Izihaki, na wote tulifaulu. Vijana wa mwaka mmoja nyuma yetu pale
Azania walikuwa na Mpemba aliyepata pointi SABA. Alikwenda tena
Tambaza akawa nyuma yetu na akapata pointi TATU. Akaenda Ulaya.
Hakunyimwa nafasi yoyote. Mwaka niliomaliza kidati cha sita kijana aliyeongoza Tanzania nzima alikuwa Karim, na yeye pia mwislamu. Hao wanaonyimwa wako wapi?

17. Kwa hiyo, kama 1/3 tu ndio waislamu (walau kinadharia), na pia wengi wao wako pwani
kwenye utamaduni wa Ghuba usiotaka shule, tunashangaa nini wakienda
wachache vyuo vikuu, tuseme 20%? Je, watakuwaje sawa serikalini na
Wakristo ambao walianza utamaduni wa elimu tangu enzi hizo? Ni suala la historia tu lakini si kwamba ukiwa mwislamu huwezi kwenda shule.

OMBI

Tufanye juhudi kuwakomboa wale wote walio nyuma kielimu Tanzania. Wako
wengi, kwa dini na makabila, lakini wote ni Watanzania. Walio nyuma
wasiseme kuna uonevu, bali waondoe kilichowakwamisha. Hatuwezi
kulinganisha utamaduni wa elimu wa watu wa Kilwa, Mafia, Rufiji na
Pangani, na watu wa Moshi, Kyela, au mkoani Kagera. Tuwe wakweli.
Mwenyezi Mungu hapendi waongo. Kwa nini shule za binafsi hazina pia
waislamu wengi? Nani anawazuia waislamu kujenga shule Tanzania? Je,
kama kweli unataka mtoto wako apate elimu safi, na amekosa nafasi ya
shule ya serikali, utampeleka wapi? Pale Kinondoni Muslim? Tuseme
ukweli.

Naamini tunao uwezo wa kuyatatua matatizo yetu ya kihistoria na
kitamaduni na si kukaa chini kupanga vurugu kwa madai ya kuonewa.
Waislamu wa Saudi Arabia hawajasoma licha ya utajiri wao. Je, hao nao
waziri wao wa elimu na baraza la mitihani ni ya Tanzania? Mbona
waislamu wa Uturuki, Tunisia, Misri, Senegal na Afrika Magharibi yote
wana elimu?

Tutafute chanzo cha kweli cha tatizo, halafu wote tushirikiane
kulitatua; wote kabisa.


--
Posted By Blogger to UDADISI: Rethinking in Action at 6/07/2012 01:30:00 AM


0 comments:

Post a Comment