Taasisi ya masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imeunga mkono
kauli iliyotolewa hivi karibuni na Sheikh mkuu wa Tanzania, Mufti Issa
Shaaban Simba ya kuwataka waislamu na watanzania kote nchini
kushiriki kikamilifu katika Sensa ya watu na Makazi itakayofanyika
Agosti 26 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kwa niaba
ya mwenyekiti wa jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania
Sheikh Hamis Mattaka amesema hatua hiyo inafuatia kuwepo kwa baadhi ya
makundi yanayowahamasisha waumini wa dini ya kiislamu na wananchi
kutoshirika zoezi la Sensa ya watu na makazi.
Amesema wao kama jopo la wanazuoni hawaoni tatizo la zoezi hilo
kutokana na umuhimu wake kwa taifa na kuongeza kuwa Sensa ya watu na
makazi ipo kwa mujibu wa sheria za nchi na imepitishwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jopo hilo limeiomba serikali kuweka sheria itakayozuia utoaji wa
takwimu zinazohusu dini za watanzania zinazotolewa na vyanzo
mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kuwa kipengele hicho si sehemu ya
sensa nchini.
"Tunajua kuwa serikali ilikua na nia njema kukiondoa kipengele cha
dini katika Sensa hapana budi nia njema hiyo ya serikali ilindwe kwa
kuweka sheria itakayozuia kutoa takwimu zinazohusu dini za watanzania"
amesema Sheikh Mattaka.
Amefafanua kuwa Sensa ya awali ya mwaka 1957 kipengele cha dini
kilihusishwa na baadaye kuondolewa katika Sensa zilizofuata kwenye
madodoso ya kukusanyia takwimu za kaya.
"Sisi kama jopo kila siku tunasema ili twende salama kama wananchi wa
nchi hii ni wajibu wetu kuheshimu na kufuata sheria kwa maana ya
kutii sheria bila shuruti, kwa hiyo tunasema Sensa ya watu na makazi
ni jambo la kisheria si jambo la mitaani, hatuwezi kulumbana na
kujadili jambo ambalo liko wazi kisheria na limepitishwa na wabunge
tuliowachagua sisi wenyewe"
Amefafanua kuwa zoezi la Sensa ya watu na makazi litaiwezesha serikali
kupanga mipango ya maendeleo kwa kuwa na takwimu sahihi za watu na
makazi, hali ya kipato cha kaya, vizazi na vifo na pia kuiwezesha
serikali kwapatia huduma bora wananchi wake.
Katika hatua nyingine jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu
Tanzania imewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa
ukusanyaji wa maoni ya katiba.
Aidha jopo hilo limewataka watanzania wote kwa ujumla kuitumia fursa
hiyo muhimu kutoa maoni ambayo yataiwezesha nchi kupata katiba
itakayokidhi matakwa ya wananchi.
" Sisi kama jopo la wanazuoni wa kiislamu tunawataka waislamu na
watanzania wote kwa ujumla kuitumia fursa hii muhimu kwa kutoa maoni
yao ili hatimaye nchi yetu ipate katiba itakayokidhi matakwa ya
wananchi kwa miaka mingi ijayo" amesema Sheikh Mattaka.
--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
0 comments:
Post a Comment