TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinarudia kutoa mwito kwa
Rais Jakaya Kikwete kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuagiza kukamatwa
kwa watuhumiwa wote wa ufisadi wa RADA ambao CHADEMA imewataja kwa
nyakati mbalimbali ikiwemo katika orodha ya mafisadi (list of shame)
tarehe 15 Septemba 2007 katika Uwanja wa Mwembeyanga.
CHADEMA kinatambua kwamba kuachwa kwa mafisadi bila kuchukuliwa hatua
kamili za kisheria na mali zao kufilisiwa kunafanya taifa kuendelea na
ufisadi ikiwemo ule wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Richmond na
sasa tuhuma mpya za ufisadi kwamba kuna vigogo wenye kiasi cha bilioni
303 kwenye akaunti Uswisi ambazo zinadaiwa kuwekwa na makampuni ya
madini, mafuta na gesi asili.
Kutokana na sheria za usiri za Uswisi; CHADEMA kinaitaka Serikali
inayoongozwa na CCM kuwasiliana na Serikali ya nchi hiyo ili kuanza
mchakato wa kuwezesha mahakama za nchi hiyo kutoa ruhusa kutolewa kwa
taarifa zote kuhusu wenye akaunti hizo na makampuni yaliyoweka kiasi
hicho cha fedha ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa
Sheria za Tanzania na Sheria za Kimataifa.
Izingatiwe pia kwenye orodha ya mafisadi CHADEMA iliwataja pia kwa
majina viongozi wa serikali ambao waliingia mikataba ya kifisadi ya
madini na rasilimali nyingine za taifa; kutolewa kwa taarifa hizo za
benki za nje kutathibitisha ukweli na pia kubainisha watuhumiwa
wengine zaidi.
Wakati huo huo; CHADEMA kinaitaka Serikali inayoongozwa na CCM
kuzingatia mpango kati yake na Serikali ya Uingereza kupanga matumizi
ya fedha kiasi cha Tshs. 72.3 billioni za RADA zilizorejeshwa baada ya
kubainika zilizochotwa kifisadi na Kampuni ya BAE Systems ya
Uingereza.
CHADEMA kimeshangazwa na uamuzi wa serikali inayoongozwa na CCM
kubadilisha mpango wa kujenga nyumba za walimu; kinyume na mpango huo
wakati huu ambapo serikali iko katika mgogoro na walimu kutokana na
kutowatimizia madai yao ya msingi ikiwemo nyongeza ya mishahara,
kulipa madeni na kupunguza kodi kwenye mishahara.
CHADEMA inaitaka serikali kukumbuka kwamba mpango huo ulikuwa moja ya
ushahidi muhimu uliotolewa Mahakamani kumshawishi Jaji kutoa uamuzi wa
kuridhia makubaliano kati ya SFO na BAE kwamba fedha hizo zingetumika
Kununua vitabu 4.4 milioni kwa ajili ya wanafunzi, vitabu 192,000 Kwa
ajili ya walimu kufundishia, madawati 200,000, kujenga nyumba 1,196 za
walimu wa shule za msingi vijijini, kujenga vyoo 200,000 kwenye shule
za msingi.
CHADEMA imeguswa pia na taarifa kwamba zabuni ya kuchapa vitabu hivyo
imetolewa kwa kampuni ya Kampuni ya Kiingereza ya Oxford University
Press hali ambayo itafanya sehemu kubwa ya fedha hizo kurejea huko
huko Uingereza; hivyo CHADEMA inaitaka serikali kuweka mfumo wa
kuhakikisha fedha hizo kwa sehemu kubwa zinatumiwa katika viwanda vya
uchapishaji vya hapa nchini ili kuchangia katika uchumi wa nchi.
Imetolewa na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
25 Juni 2012
--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
0 comments:
Post a Comment