Na Emmanuel Makene
MADA
Januari 24, 2012 madaktari zaidi ya 1,000 waligoma karibu nchi nzima.
Mgomo huo uliendelea hadi 09 Februari 2012 mara baada ya Waziri Mkuu
kukutana na madaktari na wahudumu wa sekta ya afya.
Hata hivyo, 28 Januari 2012, TUCTA (Shirikisho la Wafanyakazi
Tanzania) walitangaza kuwa mgomo wa madaktari ni batili, kinyume na
sheria na hauna maslahi kwa taifa.
29 Januari 2012, Waziri Mkuu aliomba kukutana na madaktari katika
ukumbi wa Karimjee lakini madaktari waligoma kuja katika kikao
wakasema wanawasubiri wenzao watoke mikoani.
Vilevile siku ya tarehe 09 Februari 2012, Waziri Mkuu alitangaza
kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Blandina Nyoni, na
Mganga Mkuu wa Serikali, Dr. Deo Mtasiwa.
Waziri Mkuu pia aliunda kamati ya pamoja ya watu tisa ikiwa na
wahudumu wa sekta ya afya na wawakilishi wa serikali ili kupitia madai
ya madaktari na kuishauri serikali nini kifanyike kwa ajili ya madai
hayo.
Machi 07, 2012 kulitokea mgomo mwingine ambao madaktari walitoa masaa
sabini na mbili (72) kwa serikali iwe imewafuta kazi Waziri wa Afya na
Naibu wake.
Migomo yoye hii iliathiri sekta ya afya kwa kiwango kikubwa sana.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali alipeleka kesi katika Mahakama ya Kazi na
kuwashitaki madaktari kwa kuitisha mgomo haramu. Madaktari walikataa
kwenda mahakamani wala kupeleka wakili wao. Mahakama Kuu, Divisheni ya
Kazi ili tamka kuwa mgomo wa madaktari ni haramu; madaktari
waliamrishwa kurudi kazini na vilevile kukaa katika meza ya
majadiliano na serikali kuhusu maslahi yao.
Baada ya madaktari kuongea na Mhe. Raisi mgomo ulisitishwa na
madaktari walirudi kazini.
Madakatari na wafanyakazi wote wa sekta ya afya walikuwa katika meza
ya pamoja na serikali ambapo masuala ya masalahi ya madakatari
yalikuwa yakishughulikiwa.
Juni 9, 2012 madaktari walikutana tena na kuazimia kugoma nchi nzima
katika mgomo ambao wao wenyewe wamesema utaleta madhara makubwa sana
kwa taifa. Ina maana lengo lao ni kuleta madhara kwa taifa, na madhara
hayo si ukosefu wa huduma za afya tu bali hata vifo vya watu wasiokuwa
na hatia.
Ibara ya 14 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977
inasema hivi:-
'Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi
ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria'
Hivyo daktari akigoma, na mgonjwa akifariki dunia; maana yake ni kuwa
mgonjwa amenyimwa haki ya kuishi na daktari.
Ibara ya 22 hadi ya 24 ya katiba yetu inatoa haki kwa kila mtu
(daktari) kufanya kazi na kulipwa ujira unaostahili kulingana na kazi
anazozifanya au kulipwa malipo ya haki kwa kazi alizozifanya.
Lakini bado haki ya kuishi ndio haki kuu kuliko haki zote kwani
atakaye kufa kutokana na daktari kugoma ni mhasibu, daktari, mwalimu,
wazazi wa daktari, nduguze daktari, marafiki wa madaktari, na
wengineo. Mgomo wa madaktari unawathiri madaktari wenyewe pia na
unashusha hadhi ya daktari katika jamii. Jamii itamuona daktari ni mtu
anayejari maslahi yake binafsi bila kujali wajibu wake kwa wagonjwa na
jamii kwa ujumla. Afya ya mtu si jambo la mjadala.
Ukosefu wa mazingira mazuri ya kufanyia kazi siyo sababu ya
kuhalalisha mgomo. Naomba niwape mfano wa mawakili wa serikali.
Utakuta wakili wa serikali anaendesha kesi inayohusu uingizaji wa
madawa ya kulevya yenye dhamani ya zaidi ya mabilion lakini anapanda
daladala na anaishi uswahilini, nyumba ya kupanga. Zipo kesi nzito
sana za ujambazi wa kutumia silaha za kivita ambapo watuhumiwa wameiba
zaidi ya mabilioni lakini wakili wa serikali anayeendesha kesi hiyo
hadai alipwe zaidi ya kile kilichopo.
Mimi mwenyewe niliishawahi kupewa kazi na serikali ya kuwatetea
watuhimiwa wa kesi za mauaji kwa malipo ya shilingi elfu sitini tu.
Ukihesabu siku ambazo nilikwenda Gerezani kuongea na mtuhumiwa,
gharama za usafiri za kwenda gerezani, gharama zangu za kiofisi,
gharama za kwenda mahakamani tangu kesi ilipoanza hadi ilipoisha.
Utagundua kuwa elfu sitini haikuwa hela iliyonistahili hata kwa
kufuata Ibara ya 22 na 23 ya Katiba kama nilivyotaja hapo juu.
Na hela yenyewe serikali walinilipa baada ya miezi 5 baada ya kesi
kuisha. Kwa hiyo tangia mwanzo mwa kesi hadi mwisho nilikuwa natumia
pesa yangu ya mfukoni. Ukumbuke mimi ni wakili wa kujitegemea. Kesi
hiyo ilikuwa kesi ya mauaji namba 11 ya mwaka 2006: Jamhuri dhidi ya
Thomas Anthony Mahiringa (mbele ya Jaji Madam Beatrice Mutungi).
Ni utaratibu wa serikali kuteua wakili wa kujitegea ili amtetea
mtuhumiwa wa kesi ya mauaji pale ambapo mtuhumiwa wa kesi ya mauaji
hana uwezo wa kuweka wakili wa kumtetea. Katika kesi hii ambayo,
mtuhimiwa huyo nilimtetea vizuri, bila kunung'unika, bila kinyongo na
nilikuwa simfahamu hata yeye alikuwa haamini, nilimtetea hadi
akashinda. Alikutwa na hatia ya kuuuwa bila kukusudia na akapewa
kifungo cha miezi sita nje ya gereza na alionywa asitende kosa lolote
la jinai ndani ya ile miezi sita.
Hivyo mteja wangu huyu ambaye alikuwa amekaa jela pale Ukonga kwa
zaidi ya miaka saba, siku hiyo aliachiwa huru. Hata ukiwa daktari
utatibu wagonjwa usiowajua ila watibu hadi wao washangae jinsi
unavyowajali.
Ipo kesi nyingine ya mauaji nayo nilishinda. Jamhuri dhidi ya GM
(hataki jina lake lijulikane) kesi ya mauaji namba 30 ya mwaka 2007
(mbele ya Jaji Emilian Mushi). Nayo niliipata kwa utaratibu huo huo na
nikashinda pia. Mtuhumiwa hakuwa ndugu yangu wala rafiki yangu. Ila
kwangu mimi WATANZANIA KWANZA, MASLAHI YANGU BAADAE.
Mimi kama wakili nina haki ya kugoma ili serikali iongeze malipo
ambayo sisi mawakili wa kujitegemea tunalipwa na serikali
tunapowatetea watuhumiwa wa mauaji. Lakini siwezi fanya hivyo sababu
hoja yangu haina maslahi kwa taifa. Wakili anapogoma anayeumia ni
mtuhumiwa na si serikali. MADAKTARI WANAPOGOMA ANAYEUMIA SI SERIKALI
BALI NI WAGONJWA.
NA WAGONJWA NI NDUGU ZETU WOTE NA NDUGU ZA MADAKTARI. Ukitaka
kuigomea serikali acha kazi za serikalini kaajiriwe kwingine unakoona
kuna maslahi mazuri. Hivi kweli hao madaktari wanaotaka kugoma,
wakigoma halafu wazazi wao au wake zao au waume zao wakiugua
hawataenda kuwatibu? Au wanagoma ili wafe watu wengine wasiokuwa ndugu
zao?
Ukweli unauma ila lazima niwaambie ndugu zangu madaktari. Mimi
nimebahatika sana kwani familia yetu ina madaktari wengi sana. Baba
yangu, Baba zangu wakubwa na baba zangu wadogo, madada, kaka zangu na
hata mke wangu naye ni daktari pia. Dada yangu mmoja ambaye ni daktari
aliwahi kutania siku moja tulikuwa na sherehe ya familia nakusema
yafuatayo:-
'Ukoo huu unanishangaza, yani hata wale waliosoma kozi za zisizokuwa
za sayansi, huwa wanafaulu somo la biolojia. Nadhani kila mtu katika
nyumba hii, alipaswa awe daktari'
Nakumbuka baba yangu kabla hajastaafu alikuwa akitibu wagonjwa muda
wote. Nyumba tuliyokuwa tukiishi ilikuwa jirani na hospitali. Kila
mara usiku, walinzi wa hospital walikuwa wakija kumuamsha pale ambapo
walikuwa wanapata wagonjwa waliyoitaji ujuzi wake. Na hata siku moja
sikuwai msikia akikataa kwenda kutibu wagonjwa. Na wakati huo,
mishahara ndiyo ilikuwa mibaya kuliko leo hii. Nilijifunza uzalendo
kutoka kwake.
Nilijifunza kuwa kama kijana, kama mtanzania; ni lazima nipende
kuwahudumia watanzania kwanza bila kujali maslahi binasfi. Mpaka leo
hii, baba anaheshimika sana kila mahali alipofanya kazi. Na mie huwa
nafurahi kwani kila mahali ninapoenda; huwa waniambia kuwa baba yangu
alikuwa mtu mwema, alijali sana kutibu wagonjwa wake kwa moyo wa
upendo.
Mimi sipingi madaktari kudai haki zao; haki zao wadai ila kwa kufuata
sheria na bila ya kugoma na bila kuleta madhara katika utoaji huduma
za afya.
Kuna wakati hata huwa nashindwa kuelewa mikutano ya madaktari huwa
wanaongelea nini! Kuna siku niliona kwenye vyombo vya habari walikuwa
wanasema yafuatayo:-
waliongea na kulalamika kuwa mishahara ya wabunge ni mikubwa wakati
wao madaktari wanaowapokea watu duniani wakati wa kuzaliwa na watu
wanawafia wao mikononi: wanalipwa kidogo!
Pia walisema kuwa kwanini Mwanasheria Mkuu wa Serikali analipwa
mshahara mkubwa kuliko Mganga Mkuu wa Serikali (CMO) wakati wote wana
nyadhifa sawa!
Napenda niwaelimishe madaktrai kuwa sijawai kuona sheria ya ajira
ambayo inasema mshahara wa mfanyakazi unapaswa upunguzwe (ukiacha
adhabu za kinidhamu) kama wao wanavyotaka wabunge wapunguziwe
mishahara. Mshahara siku zote huwa unaongezeka. Ukiona mwenzio
(wabunge) kaongezewa na wewe nenda ukadai uongezewe ila usiseme kuwa
fulani apunguziwe ili mimi niongezewe…..sema hivi…..naomba niongezewe,
kama mlivyomuongeza fulani.
Pia tambuemni mbunge si mfanyakazi, bali ni mwakilishi wa wananchi na
sisi wananchi tumewabidili wabunge wetu kuwa mashine za kutolea hela.
Badala ya kumueleza mbunge akatutetea bungeni, tunataka atugaie hela
ili tukatatulie matatizo yetu binafsi! Mbunge akiwanjima hela
wananchi, wananchi husema subiri uchaguzi, lazima atatukoma. Ukitokea
msiba, au jambo la kheri au harambee yeyote; watu humsubiria mbunge
achangie! Hata katika mgomo wa madaktari wapo wabunge wanaowachangia
ili wazunguke katika kila hospitali kufanya vikao haramu vya
kuhamasisha mgomo haramu!
Madaktari mnapswa mjue kuna wafanyakazi wa serikalini, hasa wakuu wa
idara ambao si wabunge ila wana mishahara mikubwa kuliko wabunge na
hata kumliko hata waziri mkuu. Mbona hamkusema kuhusu hao wakuu wa
idara za mashirika ya umma na idara za serikali? Mkabaki kuwasakama
wabunge peke yao? Pia mimi najiuliza kama daktari anaona ubunge una
maslahi mazuri, sasa kwanini hajaenda kugombea mbunge! Au madkatari
mnapiga kampeni Dr Ulimboka na viongozi wenzake wawe wabunge kwa
kupitia mgomo?
Wapendwa madaktari mnapaswa mjue kuwa CMO (MMS) hana madaraka/majukumu
sawa na Mwanasheria Mkuu (AG/MM) kama mnavyodhania. AG ni mshauri mkuu
wa masuala ya sheria wa serikali na anaingia katika vikao vikuu vya
maamuzi kama vile Baraza la Mawaziri, Bunge na nyinginezo!
Je CMO naye mliisha sikia anaingia katika vyombo hivyo! AG kwa hiyo
ndio mshauri mkuu wa sheria wa kila wizara na serikali nzima. Ana
majukumu mengi sana kuliko CMO. Licha ya kuwa maslahi ya CMO au AG
yanategemea elimu, ujuzi, maarifa na uzoefu wake lakini watu hawa wana
majukumu tofauti kabisa si kwa Tanzania bali hata nchi nyingine. CMO
hana cha kujibu Bungeni, liwe jema au baya kuhusu huduma za afya,
mzigo huo unabebeshwa waziri wa afya kulijibu bunge.
Serikali ikashambuliwa bungeni kuhusu sekta ya afya; mwenye jukumu la
kujibu siyo CMO ni waziri wa afya. Wakati hoja ikiwa ya kisheria
mwenye kujibu au kulishauri bunge ni AG.
MADAI YA MADAKTARI
Madai ya madaktari yalikuwa kama ifuatavyo:-
Kuongeza Mshahara wa Mwezi kutoka Tshs. 700,000/= hadi Tshs. 3.5 Mil
10% ya Mshahara wa Mwezi kuwa Posho ya Kuitwa Kazini (Call Allowance)
30% ya Mshahara wa Mwezi kuwa Posho ya Kazi za Hatari ( Risk
Allowance)
30% ya Mshahara wa Mwezi kuwa Posho ya Maladhi/Nyumba (Accommodation/
Housing Allowance)
40% ya Mshahara wa Mwezi kuwa Posho ya Kufanya kazi katika mazingira
magumu (Hardship Allowance) 10% ya Mshahara wa Mwezi kuwa Posho
Usafiri (Transport Allowance) Kukopeshwa magari na kupatiwa Bima ya
Afya Daraja la Kwanza (First class/Green card).
Pamoja na madai mengine ya kimaslahi
MAONI
Masharti ya kugoma au kutokugoma yapo katika Sheria ya Ajira na
Mahusiano Kazini, Namba ya 6 ya 2004 katika kifungu cha 75 hadi 85.
Sheria hii ni moja ya sheria zenye kulinda maslahi ya mfanyakazi na
mwajiri ambayo bunge liitunga baada ya maridhiano baina ya
wafanyakazi, waajiri, serikali na Shirika la Kazi la Kimataifa/la
Umoja wa Mataifa (ILO).
Kwa sheria zote za Tanzania, sijawai kuona sheria ambayo wadau
walishirikishwa kwa hatua zote na kwa maamuzi yote. Tena nikiwamegea
siri, Bunge ni kama halikutunga sheria hii, kwani kila kitu kilifanywa
nje ya Bunge na wafanyakazi na waajiri; Bunge ni kama lilipiga muhuri
tu. Nashangaa kuona madaktari wanaotaka kugoma kwa kutokufuata sheria
za nchi.
Madaktari wakumbuke kuwa Mwajiri anayo haki ya kuwafukuza kazi na
kuajiri wafanyakazi wengine, hili sio jambo la mchezo hata kidogo.
Hawa viongozi wa madaktari wanatumiwa na wamerubuniwa na watu
wasioipenda Tanzania. Wamerubuniwa na watu wanaopenda kufurahia
watanzania wafe sasa sijui wanataka kula njama za wataokufa.
Mgomo wa madaktari haukuwa halali na hautakuwa halali kwani Sheria za
Kazi za Tanzania haziruhusu migomo isipokuwa kwa masharti yafuatayo:-
Mgomo unapaswa uwe ni kuhusu suala la haki ambalo halipo katika sheria
za kazi na wala halipo katika Mkataba wa Ajira wa Mfanyakazi husika.
Kwa mfano, kama posho ya mazingira magumu haipo katika mkataba wa
ajira na sheria haijaizungumzia, mfanyakazi ataruhusiwa kugoma.
Wafanyazi walioko katika huduma ya maji, huduma za usafi/huduma za
kuondoa uchafu/taka (sanitation), umeme, huduma za afya & maabara,
zima moto & uokoaji, huduma za udhibiti, uongozaji safari za anga &
mawasiliano ya ndenge na usafiri katika huduma hizo hapo juu
hawaruhusiwi kugoma.
Wafanyakazi wanaopaswa kutoa huduma wakati wa mgomo hawaruhusiwi
kugoma. (kuna kipindi wafanyakazi baadhi wanaruhusiwa kugoma kwa
sharti kuwa baadhi yao wafanye kazi wakati wa mgomo ili kazi zifanyike
na huduma zitolewe)
Wafanyakazi ambao wamekatazwa na mkataba wa hiari na mwajiri
kutokugoma.
Pia mahakimu, waendesha mashitaka na maafisa wa mahakama hawaruhusiwi
kugoma. Vile vile wafanyakazi wote walioko katika sekta ya huduma
muhimu kama za nilivyoeleza hapo awali:
matibabu/hospital/afya,
waongoza ndege,
huduma za umeme,
huduma za usambazaji/uzalishaji maji,
huduma za sanitation,
huduma za zima moto na ukoaji,
huduma za uongozaji wa ndege,
huduma za masiliano katika huduma za anga na
huduma zote za usafiri katika sekta tajwa hapo juu
hawaruhusiwi kugoma ila sheria ina wapa kipaumbele cha kupeleka
malalamiko yako katika Kamati ya Huduma Muhimu (Essential Services
Committee) badala ya kugoma. (Kifungu cha 76 na 77, Sheria ya Ajira na
Mahusiano Kazini, Namba ya 6 ya 2004)
Hii ndiyo sheria na sheria lazima ifuatwe, nchi haiongozwi kwa jazba
na hamaki za watu. Ingekuwa hivyo basi kila mtu angafanya analolitaka
basi hata amani, utulivu na ustarabu usingekuwepo.
Licha ya a-e hapo juu; Pia kabla ya kugoma kwa wafanyakazi
wanaoruhusiwa kugoma (ambao siyo madaktari na siyo wafanyakazi
wanaotoka katika huduma muhimu kama nilivyoanesha hapo juu i-ix)
inabidi suala la mgomo liwe limepelekwa katika Tume ya Maridhiano na
Usuluhishi wa Masuala ya Kazi, pia Tume iwe imeshindwa kusuluhisha,
mgomo unapaswa uitishwe na chama cha wafanyakazi, kura ya siri ipigwe
kulingana na katiba ya chama na wafanyakazi kwa wingi wao wakukubali
kugoma, mwajiri anapaswa apewe notisi ya masaa 48 kabla ya kugoma.
(Kifungu cha 75, 76 na 80, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Namba
ya 6 ya 2004)
MAONI NA HITIMISHO
Mgomo wa madaktari ni haramu. Si kuwa ni kinyume cha sheria bali hata
kinyume na maadili na kinyume na mafundisho ya dini zote ambazo
watanzania wanaziamini. Yafuatayo yanapendekezwa yafanyike ili tatizo
kama hili lisitokee:-
Madaktari wasiruhusiwe kufanya tena vikao vya mgomo kwani sheria
hairuhusu. Wao wana viongozi wao, hao viongozi ndio wakae na serikali
ili kutatua hilo tatizo. Haiwezekeni madaktari wote wakae katika kikao
kimoja. Je nani atabaki hospitali kutibu wagonjwa? Uliona wapi
waandishi wa habari au walimu nchi nzima wamekaa kikao kimoja? Hakuna
kikao cha wanataaluma wote kwa pamoja kwa siku moja!
Madaktari waelimishwe kuhusu sheria za kazi na sheria za nchi na haki
zao.
Madaktari waelezewe kuwa licha ya kuwa mishahara ya madaktari haikidhi
gharama za maisha kwa sasa; lakini kwa wanataaluma wote wanaoajiriwa
na serikali kama wahandisi, walimu, wanasheria, nk…..ni madakatari
ndio wenye mishahara mikubwa. Kama ni kuwa maslahi ya udaktari si
mazuri hata kwa wanataaluma wengine pia. Kila mfanyakazi wa serikali
ukimuuliza atakueleza mshahara haumtoshi! Maisha huwa yanapande
gharama na sijawai kuona yakishuka. Madaktari waeleimishwe jinsi ya
kupambana na maisha na kuacha kujipendelea kwani wafanyakazi wote wa
sekta ya afya na sekta nyingine pia wanaitaji kuongezewa mishahara na
posho zao.
Serikali ijipange kuwabana wanaharakati ambao ndio walikuwa
wanawashawishi madaktari ili wagome. Inasemekana vikao vya viongozi wa
madaktari vilikuwa vinafanyika katika baadhi ya ofisi za wanaharakati
tena mbaya zaidi wanaharakati wa haki za binadamu. Sasa hawa
wanaharakati wa haki za binadamu ambao hawajali haki ya uhai wa
mgonjwa ila wanajali haki ya maslahi ya daktari. Serikali izifute hizi
taasisi. Kuna haja ya kuwabana sana wanaharakati hawa waliokuwa
wanawashawishi madaktari na kuwaletea waandishi wa habari wa kuandika
habari zenye kuwapendelea madaktari na kuliangamiza taifa. Hata hao
watu wanaojiita wanadai haki za binadamu na kutoa ushauri wa kisheria
kwa madaktari sijawai kuwaona mahakamani wakishinda kesi hata moja!
Sijawai kuwaona wakipewa leseni ya uwakili! Sheria ya uwakili wa
kujitegemea inasema kuwa ni wakili aliyesajiriwa baada ya kufanya
mitihani ya kitaaluma na kufaulu ndiye anayepaswa kutoa ushauri wa
kisheria. Sasa hawa hawajafaulu mitihani ya kuwa mawakili wanatoaje
ushauri wa kisheria kwa madaktari? Ndiyo maana wanaishia kuwadanganya
madaktari kama wanavyowadanganya wajane, walemavu na watu wote kutoka
makundi maalumu wanaohitaji ushauri na huduma za kisheria bure. Ina
maana watu hawa wanojiita wataalamu wa haki za binadamu hawajui kuwa
haki ya kwanza ni kuishi! Sasa kwa nini watu wa haki za binadamu
wanaunga mkono mgomo wa madaktari hawajui kuwa wagonjwa watafariki?.
Au wametumwa! Au wanataka wapewe misaada na nchi za nje kwa ajili ya
kujilipa posho wanaharakati wakati mgomo ukitokea!
Madaktari walionekana kufurahia pale walipokuwa wakiona vyombo vya
habari vikilaumu serikali na kuandika habari zao. Kuna haja ya
kudhibiti vyombo vya habari katika masuala ya mgomo pia serikali itoe
taarifa sahihi na muhimu. Madaktari wakigoma hata waandishi wa habari
watakufa kwa kukosa huduma. Naomba sana ndugu zangu waandishi wa
habari, siku madaktari wakigoma, na nyinyi gomeni msiandike habari
zao!
Madaktari watakaogoma na wakatwe mshahara wa siku watakazogoma, na
madaktari watakaokuwa kazini wakati wa mgomo inapaswa wapewe posho ya
kufanya kazi za ziada wakati wenzao wamegoma.
Madaktari ambao wako tayari kuendelea na kazi, walindwe na wasaidiwe
waweze kutibu wagonjwa kwani wao ndiyo mashujaa wetu na wazelendo.
Madakatri waelimishwe kuwa si wao ndio wafanyakazi wa serikali pekee
bali serikali ina wafanyakazi wengi na wote wana umuhimu sana na wote
wanahitaji waongezewe posho na mishahara licha ya kuwa mishahara ya
madaktari ni mikubwa kuliko mishahara ya wanataaluma nyingine.
Unapohitimu chuo kikuu, ukiajiriwa na serikali kama wewe si daktari
basi ujue haulipwi mshahara anaoupata dakatari. Suala hili naona hata
vyombo vya habari hawaliandiki kabisa. Mishahara ya taaluma nyingine
inafuata baada ya mishahara ya madaktari. Sasa mbona wanataaluma
wengine hawajagoma na wanadai maslahi yao kwa kufuata taratibu za
sheria! Iweje kwa madaktari?
Madaktari waelimishwe wajue wakigoma wagonjwa wanakufa na jukumu la
kwanza la daktari ni kuokoa maisha (save life), jukumu ambalo hawataki
kulifanya na kuamua kugoma. Kama ndugu zetu wakifa kutokana na mgomo
wa madaktari; sote tutasema….baba yangu, ndugu yangu, rafiki yangu
alifiariki si kwa ugonjwa ila kwa mgomo wa madakari! Ndugu yangu
alikufa kipindi kile madaktari walipogoma!...
Daktari anayegoma siwezi mtofautisha na Dr. Harold Fredrick Shipman wa
Uingereza ambaye aliwaua wagonjwa wake zaidi ya wagonjwa 250 kwa
makusudi kabisa . Wagonjwa hao 80% walikuwa wanawake na aliwaua kati
ya mwaka 1995 hadi 2000. Nataka niwaambie watanzania wenzangu akina
Dr. Shipman wameishaingia Tanzania pia. Sisi wagonjwa tujue hatma yetu
imefika kabla ya mwenyezi mungu hajaamuru tufe.
Pia Daktari bingwa wa upasuaji na mashuhuri sana, Dr. Francis E.
Sweeney aliwahi kuuwa zaidi ya wagonjwa wake 13 kwa makusudi kabisa!
Yupo pia Dr. Morris Bolber wa Philadelphia, Marekani katika miaka ya
1930 aliuwa zaidi ya wagonjwa wake 50 ili aweze kunufaika na bima
(death benefits) ambazo ndugu/warithi wa wagonjwa walikuwa wakilipwa.
Dr. Thomas Neil Cream alinyongwa mwaka 1892 huko Uingereza baada ya
kuwauwa wagonjwa wake zaidi ya 10 kwa makusudi kwa kuwapa sumu ya kuua
badala ya matibabu.
Dr. Henry H. Holmes aliuwa zaidi ya watu 230 huko Chigaco, Marekani
katika miaka ya 1870 hadi 1896.
Dr. John Bodkin Adams aliyekamatwa mwaka 1957 kwa kuwaua wagonjwa wake
zaidi ya 10 huko Uingereza.
Serikali iajiri madaktari wengi katika majeshi yote ili kusaidia kutoa
huduma katika hali ya migomo kama hii. Kuna haja ya kuwa na madaktari
wengi katika majeshi yetu.
Vilevile hospitali za majeshi ziongezewe vifaa na wataalamu. Hosptali
za binafsi na hospitali za mashirika ya dini zisaidiwe ili kupunguza
gharama za matibabu katika hospitali binafsi.
Madaktari wasainishwe kiapo cha utii na kiapo cha kutogoma kabla ya
kuanza kazi kama vile sheria inavyotaka.
Madaktari ambao hawaungi mkono mgomo, serikali iwasaidie ili waweze
kufanya kazi bila ya kusumbuliwa na waliogoma.
Madakatri waelimishwe kuhusu vyama vyao kwani hawaelewi ndio maana
hata Dr. Steven Ulimboka anayeongoza mgomo si daktari aliyeajiriwa na
serikali, jambo ambalo si sahihi kwa mtu asiye mfanyakazi wa serikali
kuigomea serikali.
Serikali ifuatilie hasa katika mifumo ya hela ya kibenki, nk kwani
inasemekana kuwa watanzania wanaoishi nje ya nchi wakisaidiana na watu
wasio wapenda maendeleao wanafadhiri mgomo kwa kutuma hela katika
akaunti za benki za viongozi wa mgomo wa madaktari.
Serikali ijitaidi kujenga nyumba za madaktari kwa wingi jirani na
hospitali ili kuboresha huduma za afya kwani madakatri wakiishi jirani
na hospitali inakuwa rahisi kuhudumia wagonjwa. Mfano serikali
ijitaidi kujenga nyumba za madaktari na wafanyakazi wa sekta ya afya
jirani na hospital ili iwe rahisi kwao kutoa huduma. Daktari anayekaa
Mbagala na anakuja kutibu wagonjwa katika hospital ya Mwanayamala
anasafiri umbali mrefu kiasi kuwa anachoka akiwa njiani kuja kazini.
Mahusiano kati ya viongozi wa wizara ya afya na wahudumu wa afya
yaendelee kuboreshwa ili kuwa na mahusiano mazuri katika sekata yote
ya afya.
Madaktari wapunguze kuwe na misimamo ya kihafidhina kama Uamsho na Al
Shabab. Madaktari watambue kuwa haki zao za maslahi mazuri ya kazi
zinapoishia ndio haki ya mgonjwa ya kusihi inapoanzia.
Madakatari wajifunze kutoka kwa wanataaluma wengine jinsi ambavyo
wanataaluma wengine wanavyoendesha umoja/vyama vya taaluma zao.
Wajifunze kutoka kwa wahasibu, wahandisi, nk
Imeandikwa na Ndugu Emmanuel Makene, wakili wa kujitegemea na
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Kinondoni.
--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
0 comments:
Post a Comment