Wednesday, 20 June 2012

[wanabidii] MCHANGO WA NDUGU EMMANUEL MAKENE KUHUSU MUUNGANO WA ZANZIBAR NA TANGANYIKA

Na Emmanuel Makene

Miaka 48 iliyopita, Raisi wa Tanganyika wakati huo, Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Raisi wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume; walisaini mkataba ulioitwa Mkataba wa Muungano (Articles of Union) kwa ajili ya kuunganisha nchi zao (Zanzibar & Tanganyika) kuwa nchi moja yenye dola moja.

Mkataba huo ulikuwa mkataba wa Kimataifa (International Treaty) na kila nchi ilipaswa kuridhia mkataba huo katika sheria za nchi husika. Kazi ya kuridhia ni kazi ya Bunge la kila nchi.

Kwa upande wa Tanganyika, tarehe 25 April, 1964, Bunge la Tanganyika liliridhia Mkataba wa Muungano na Bunge la Tanganyika likatunga sheria iliyoitwa Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Namba 22 ya mwaka 1964. Hii ina maanisha kuwa mkataba wa Muungano ni sehemu ya sheria za nchi (Tanganyika) kuanzia tarehe 26 Aprili 1964.

Kwa upande wa Zanzibar, wao hawakuwa na Bunge wala Baraza lolote la Wawakilishi. Baraza la Mapinduzi la Zanzibar ndio lilikuwa likifanya kazi kama Bunge la Zanzibar na Baraza la Mawaziri. Hivyo Mkataba wa Muungano uliridhiwa na kupitishwa na Baraza la Mapinduzi. Isipokuwa kutokana na uzembe au kutokuwa makini kwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, tangazo la kuridhia Mkataba wa Muungano haukutolewa katika Gazeti la Serikali (Government Gazette) la Zanzibar. Hivyo Mkataba wa Muungano ulipitishwa na kuthibitishwa na Baraza la Mapinduzi.

Wapo wasomi ambao wamekuwa wakikosoa kuhusu jambo hili, lakini inabidi tukubali kuwa masuala yote ya sheria; Raisi husaidiwa na Mwanasheria Mkuu. Mwanasheria Mkuu ndio mshauri mkuu wa masuala ya sheria kwa serikali, yeye ndiye mwenye jukumu la kubariki kazi zote za Raisi au serikali kabla ya serikali haijafanya hiyo kazi husika. Mfano ni Mwanasheria Mkuu wa serikali na Katibu wa Baraza la Mawaziri ndio wenye jukumu la kuhakikisha kuwa wanapeleka Muswada/Mkataba kuridhiwa na Bunge na kutoa matangazo katika gazeti la serikali (Government Gazette).

Miswada yote inayotoka serikalini kwenda Bungeni husainiwa na Katibu wa Baraza la Mawaziri.

Muswada ukiwa sheria baada ya Bunge kuupitisha ni Katibu wa Bunge ndiye  wa kwanza kuuthibitisha kuwa Bunge limepitisha muswada husika kuwa sheria.  Na baada ya Katibu wa Bunge (Clerk of the National Assembly) kuusaini inabaki kazi ya Raisi kuusaini (assent) ili sheria ianze kutumika.

Kwa hiyo Zanzibar waliridhia na kuthibitisha Mkataba wa Muungano isipokuwa  kulikuwa na matatizo katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kutoa Tangazo katika Gazeti la Serikali baada ya Baraza la Mapinduzi kupitisha Mkataba wa Muungano kuwa sehemu ya sheria za Zanzibar.

Tarehe 27 April, 1964 majira ya saa kumi na moja jioni kulifanyika sherehe kubadilishana nyaraka za Muungano. Muda huo Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume walibadilishana Nyaraka za Muungano mbele ya Bunge la Tanganyika. Na vile vile siku hiyo wajumbe saba wa Baraza la Mapinduzi kutoka Zanzibar waliapishwa kuwa wabunge wa Bunge la Muungano. Wajumbe hao wa Zanzibar ni Abeid Karume, Kassim Abdallah Hanga, Abdulrahman Babu, Hassan Nassor Moyo , Aboud Jumbe Mwinyi, Hasnu Makame  na Idris Abdul Wakil.

Kwa upande wa Zanzibar, Baraza la Mapinduzi pia lilipitisha na kuikubali sheria ya Muungano (Sheria ya Muungano wa Zanzibar na Tanganyika)) kulingana na taratibu za Zanzibar za wakati huo.

Kifungu cha 4 cha Sheria ya Muungano kinasomeka hivi:-

Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar katika siku ya Muungano (Union day); zitaungana kuwa dola moja na Jamhuri moja na kuitwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwa hiyo, siku ambayo Mwl. Nyerere alichanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar ndiyo ilikuwa siku ya Muungano. Siku hiyo waliobeba vibuyu na vyungu ni Mama Sifaeli Shuma ambaye alibeba kibuyu kilichokuwa na udongo wa Tanganyika, Khadija Rajabu Abbas alibeba chungu chenye udongo wa Zanzibar, Omari Hassan Mzee alibeba chungu kilichokuwa na udongo wa Tanganyika na Zanzibar baada ya kuchanganywa.
Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar liliendelea kutumika kwa muda mfupi kwani wengi waliliona kuwa ni refu. Mwezi Desemba 1964; Bunge la Muungano lilitunga Sheria ya kutumia jina Tanzania. Sheria hiyo iliitwa Sheria ya Jamhuri ya Muungano (kutangazwa kwa Jina la Nchi), Namba 61 ya mwaka 1964. Kuanzia Desemba 1964, jina TAN (TANganyika) & ZA (ZAnzibar) NIA (ya kuungana) lilianza kutumika.

Nyaraka za Serikali ya Muungano kabla ya Decemba 1964 zilionyesha jina la nchi kama Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Miradi ambayo Mwalimu Nyerere aliizindua mfano jiwe la Msingi la Jengo la Ushirika lililopo Mtaa wa Lumumba, Ilala, Dar es Salaam linasomeka hivi hadi leo:-

"Jiwe la Msingi limewekwa na Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mwl. J.K. Nyerere leo tarehe ………….. 1964.


JE, MUUNGANO WA ZANZIBAR NA TANGANYIKA NI WA KIPEKEE HAPA DUNIANI?

Kuna wanasiasa na wasomi wamekuwa wakieleza maneno kuwa dunia hii hakuna Muungano kama huu wa Tanzania yaani  Muungano na serikali mbili; kwamba kuna Muungano wa kubaki na serikali moja au tatu! Jambo hili si la kweli. Wanasiasa na wasomi wanaosema hivyo ni watu wanaohubiri siasa rahisi (cheap politics) na kufundisha wanafunzi wetu taaluma ya kichochezi kabisa.

Ukweli ni kuwa Muungano wa Zanzibar na Tanganyika unafanana kwa kila hali na Muungano wa Uingereza (England) na Scotland. Muungano wa England na Scotland ulizaa United Kingdom of Great Britain siku ya Mei Mosi 1707 baada ya nchi hizo kusaini Mkataba wa Muungano. (Treaty of the Union between Kingdoms of Scotland and Britain). Mkataba huu unafanana (pari material) na Mkataba wa Muungano (Articles of the Union wa Zanzibar na Tanganyika.

Mambo yanayofanana katika mikataba hiyo miwili ni kuwepo kwa Serikali ya Muungano ambayo pia inashughulikia masuala ya upande mmoja wa Muungano (Tanganyika/Uingereza). Pili nchi ndogo (Zanzibar/Scotland) kuruhusiwa kuwa na serikali yao kwa masuala yasiyokuwa ya Muungano.

Mkataba wa Muungano wa Scotland na England ulithibitishwa na mabunge yote yaani la Scotland na la England. Mpaka leo hii, huu Muungano upo licha ya kuwepo kwa changamoto nyingi zinazoukabili.

Changamoto zinazoukabili Muungano wa Scotland na England zinafanana na changamoto za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Ni rai yangu kuwa wasomi na wanasiasa wa Tanzania wanapaswa wajifunze na wafanye utafiti makini kuhusu faida za Muungano kabla hata ya kutoa maoni kuhusu kulazimisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uvunjwe.

Muungano wa Uingereza haukuishia kuunganisha Scotland pekee ila baadae waliungana na Ireland ya Kaskazini (Northern Ireland), na Wales pia. Kwa hiyo hivi leo Uingereza tunayoijua ni Muungano wanchi ambazo ni England, Northern Ireland, Scotland na Wales.

Zile nchi ndogondogo yaani Scotland, Northern Ireland na Wales zina serikali zao hadi leo kwa ajili ya Masuala yasiyokuwa ya Muungano (non- union matters) kama ilivyo kwa Zanzibar. Isipokuwa England yenyewe kama ilivyo Tanzania Bara haina serikali kwa masuala yake yasiyokuwa ya Muungano (non – union matters). Mambo yasiyokuwa ya Muungano ya England yanashughulikiwa na serikali ya Muungano yaani Government of United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland. Pia ikumbukwe kuwa nchi ya Ireland ambayo iko jirani na Uingereza ni tofauti na Northern Ireland.

Northern Ireland mji mkuu wake ni Belfast, Scotland ni Edinburg, Wales mji mkuu wake ni Cardifff. Wakati London ni mji mkuu wa Muungano wa Uingereza yote.

Uingereza ndio taifa la kwanza duniani kuwa na viwanda vikubwa. Pia ni taifa kubwa lenye nguvu za kiuchumi, kijeshi, kisayansi, kiutamaduni na ushawishi wa kisiasa. Sasa jiulize kwa nini lilihitaji Muungano – tunaona maskini hatutaki Muungano – tunaona hauna maana. Tumepoa, tumepotoka!.

Licha ya Muungano huo; Uingereza ni Mwanachama wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya Madola, Halmashauri ya Ulaya (Council of Europe), G7, G8, G20, NATO, OECD, World Trade Organization na Mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC).

Kwa hiyo Scotland, Wales na Northern Ireland hazina dola ingawa ni nchi. Nchi yenye dola ni ule Muungano wao yaani United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland. Wasomi wengine huita nchi hii 'nchi nne ndani ya nchi moja' yaani four countries within a country.

Mara nyingi watu wanaifahamu nchi hii kwa jina moja tu United Kingdom (UK) au Britain au England lakini hawajui kama nchi hii imeundwa na nchi zilizoungana kama ilivyo Tanzania Bara na Zanzibar. Raia wa Uingereza huwa wengine wanajitambulisha kama Wabritish, Wainglish, Wascottish, Wawelsh au Wanorthern Irish. Kama ilivyo kwa raia wa Tanzania; wengine hujiita Wazanzibar, wapo wanaojiita Watanganyika kama Mch. Christopher Mtikila. Lakini jambo la msingi ni kuwa Pasi yake ya kusafiria inasema Mch. Mtikila ni raia wa Tanzania na siyo raia wa Tanganyika.

Vile vile licha ya Uingereza kuwa ni Muungano wa nchi nne zilizokuwa na dola bali pia Uingereza ni nchi yenye utawala wa kifalme. Uingereza si Jamhuri (Republic) bali ya kifalme (Monarchy).

Ufalme (Monarchy) wa  Uingereza una haki ya kuombwa ushauri na serikali, hali ya kushawishi serikali na wananchi. Pia ufalme una haki ya kuionya serikali/wananchi. Mfalme au Malkia ni Mkuu wa Nchi pia na ndiye anaye (assent) saini sheria ikiishapitishwa na Bunge ili ianze kutumika. Waziri Mkuu wa Uingereza ni mkuu wa serikali. Waziri Mkuu wa Uingereza hapigiwi kura na nchi nzima isipokuwa hutoka kwenye chama chenye wabunge wengi katika Bunge la Makabwela (House of Commons). Uingereza kila kiongozi wa juu wa chama cha siasa huwa anagombea Ubunge na ikatokea chama chake kinapata viti vingi katika Bunge, Kiongozi huyo wa chama chenye wabunge wengi huwa Waziri Mkuu. Waziri Mkuu wa Uingereza na Baraza lote la Mawaziri huteuliwa kiutawala na Ufalme (Monarchy) kuunda serikali ingawaje kiuhalisia ni Waziri Mkuu ndiye anayewachagua mawaziri. Kwa taratibu za Uingereza, ufalme huheshimu wote ambao huteuliwa na Waziri Mkuu.

Mawaziri wote wa Uingereza kutoka katika Bunge la Makabwela ambalo lina wabunge 650 kutoka katika majimbo 650. Uingereza pia ina vyama vikubwa vya siasa vitatu yaani Conservative Party (Chama rafiki na CHADEMA), Labour Party (Chama rafiki na CCM) na Liberal Democrats. Vyama vingine ni vidogo na huwa havishindi viti vya ubunge au wakati mwingine hupata kiti kimoja hivi au viwili kwa bahati. Hata Tanzania vyama vya Siasa vikubwa ni vitatu kwa sasa na vingine huwa wasindikizaji.  Uingereza hakuna viti maalum. Kila anayetaka Ubunge huwa anaenda jimboni kugombea ubunge.

Wales, Northern Ireland na Scotland huwa zina serikali na mabunge yao. Waziri Mkuu wa hizi nchi (Wales, Northern Ireland na Scotland) huitwa First Minister kama ilivyo kwa Zanzibar, Chief Minister na sasa Makamu wa Pili wa Raisi.

Jambo lingine la kuvutia kwa Uingereza ni kuwa, nchi hii ina katiba ambayo haijaandikwa (uncodified constitution) tofauti na Tanzania. Katiba ya Uingereza ambayo haijaandikwa huwa inarekebishwa na Bunge la Uingereza kwa kipengele/taswira ya Katiba ambayo haijaandikwa au imeandikwa.

MUUNGANO WA UINGEREZA UNAVYOFANANA NA MUUNGANO WA TANZANIA

Wales, Northern Ireland na Scotland huwa zina Serikali na mabunge yao. Waziri Mkuu wa hizi nchi (Wales, Northern Ireland na Scotland) huitwa first Minister kama ilivyo kwa Zanzibar Chief Minister na sasa Makamu wa Pili wa Raisi wa Zanzibar.

Ile nchi kubwa ya Uingereza (largest country of United Kingdom) haina serikali yake kama nilivyokwisha fafanua awali bali hutegemea serikali ya Muungano kwa masuala yote ya ndani ya Uingereza kwenyewe.

Pia Bunge la Uingereza lina Baraza la juu zaidi ambalo huitwa Baraza la Mabwanyenye (House of Lords) wajumbe wa Baraza hili huteuliwa kutoka katika viongozi wa dini wa kanisa la Uingereza na wengine huteuliwa na Ufalme kutoka miongoni mwa Waingereza wenye sifa na heshima kwa taifa ambao si wabunge wa Bunge la Makabwela. House of Lords ni wataalamu wa maarifa mbalimbali ambao huchambua sheria zilizopitishwa na House of Commons. Wabunge wa House of Lords hawachaguliwi kwa kupigiwa kura na wananchi lakini hulinda maadili ya Taifa pia na walinzi wa katiba kwani wana uwezo au nguvu (Parliamentary Soreignity) ya kufuta maamuzi ya mahakama na hata masuala ya katiba. Mawaziri wachache sana huteuliwa kutoka katika House of Lords. Kwa sasa House of Lords ina wajumbe 189.

Kuna haja ya Katiba mpya ya Tanzania kuwa na Bunge la Ushauri (Senate) vilevile likiwa na wajumbe ambao ni watu mashuhuri au viongozi wastaafu.

JE, ZANZIBAR ILIBURUZWA KATIKA MUUNGANO?

Si sahihi kabisa kusema katika Muungano Zanzibar iliburuzwa. Viongozi wa Zanzibar, Sheikh Abeid Karume, Mzee Thabit Kombo, Hassan Nassor Moyo, Idris Abdul Wakili, Abdul Jumbe na wengineo hawakuwa viongozi wa kuburuzwa hata kidogo.

Hata uamuzi wa nani awe Raisi wa Muungano ni uamuzi wa Sheikh Karume kwani ndiye aliyemwambia Mwl. Nyerere awe Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ukisikiliza hotuba za Sheikh Karume za kati mwaka 1964 na 1969 amerudia sana haya maneno. Naomba ninukuu kama ifuatavyo:-

"Nimemwambia Mwalimu tuungane yeye awe Raisi na Mimi niwe Makamu wake"

Hakuna jambo hata moja ambalo Tanganyika iliiburuza Zanzibar. Kila jambo la Muungano liliamuriwa kwa muafaka wa pande zote mbili. Utaratibu huu unaendelea hadi leo hii. Licha ya elimu ya darasani ndogo aliyokuwa nayo Sheikh Karume lakini alikuwa na busara na mapenzi kwa watu wake kuliko hata wasomi wa leo hii ambao hawana mapenzi kwa taifa lao.

Mfano, Sheikh Karume aliweza kujenga nyumba za makazi kwa wazanzibar ambazo zimetoa malazi kwa zaidi ya familia mia tisa. Nyumba hizi zinatumika mpaka leo.

KWA NINI RAISI WA ZANZIBAR SIYO MAKAMU WA RAISI WA TANZANIA TENA!

Baada ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa ilionekana hakuna haja ya Raisi wa Zanzibar kuwa Makamu wa Raisi wa Muungano. Kwani iwapo Raisi wa Zanzibar akitoka chama tofauti na Raisi wa Muungano: ingekuwa ngumu kuongoza nchi na hata vikao vya Baraza la Mawaziri. Kwani huyo Makamu wa Raisi (Raisi wa Zanzibar) angeweza kuwa na msimamo tofauti na Raisi wa Tanzania kuhusiana na ilani ya uchaguzi, sera na mtazamo wa kisiasa.

Sababu nyingine ambayo ilipelekea Raisi wa Zanzibar kuondolewa kuwa Makamu wa Raisi wa Muungano ni kuzuia madaraka makuu ya nchi (Raisi wa Muungano na Makamu wa Raisi wa Muungano) kwenda kwa upande mmoja wa Muungano iwapo Raisi wa Muungano atakuwa Mzanzibar. Raisi wa Tanzania akiwa Mzanzibar na ikumbukwe kuwa Raisi wa Zanzibar kwa nafasi yake alikuwa anakuwa ni Makamu wa Raisi wa Muungano; basi nafasi za juu za uongozi zingekuwa chini ya upande mmoja wa Muungano.

Ili kuleta usawa katika kugawana madaraka makuu ya nchi katiba ya Muungano ilirekebishwa na Makamu wa Raisi ni mgombea mwenza wa Raisi wa Tanzania na wanatokana na Chama alichotoka mgombea wa uraisi. Iwapo mgombea wa uraisi atatoka upande wa kwanza wa Muungano basi mgombea wa Makamu wa Raisi wa Muungano anapaswa atoke upande wa Pili wa Muungano!

Ikumbukwe pia Raisi wa Muungano (kama anatoka Bara) anapotaka ushauri kuhusu masuala ya Zanzibar; ushauri huu anaupata kwa Raisi wa Zanzibar na siyo kwa Makamu wa Raisi (hata kama makamu wa Raisi anatoka Zanzibar).

KATIBA YA ZANZIBAR.

Tangu mwaka 1963; Zanzibar iliongozwa kwa amri ya Raisi (Presidential Decrees) na Baraza la Mapinduzi. Baraza la Mapinduzi lilikuwa ni Serikali na Bunge kwa wakati huo huo.

Ni mpaka mwaka 1984 ndio Zanzibar ilipata katiba iliyoandikwa katika nyaraka moja na Baraza la Wawakilishi liliundwa na wajumbe wa Baraza la Mapinduzi/Mawaziri walianza kuteuliwa na Raisi kutoka miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

MABADILIKO YA KATIBA YA ZANZIBAR MWAKA 2010 YA KUWEKA NAFASI YA MAKAMU WA PILI WA KWANZA WA RAISI WA ZANZIBAR KUNATAMBULIWA NA KATIBA YA MUUNGANO?

Ibara ya 102 hadi ya 107 (Sura ya Nne) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatambua uwepo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Katiba ya Zanzibar. Hivyo kisheria inamaanisha kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatambua Katiba ya Zanzibar na marekebisho yeyote yale yatakayofanyika Katiba ya Zanzibar.



KWANINI HAIRUHUSIWI KUTOA MAONI KATIKA TUME YA KUREJEA KATIBA YA MUUNGANO KWA MASUALA YA MIPAKA YA MUUNGANO?

Ni sahihi kabisa kwa wananchi wa pande zote za Muungano kuzuiwa kujadili mipaka ya kijiografia ya Muungano na kujadili au kupiga kura ya maoni kama Muungano uwepo au usiwepo!

Ni viongozi wendawazimu tu ndio wanaoweza kuwauliza watanzania kama wanataka, Muungano au hawataki! Kiongozi mbaguzi ndiye anayeweza kuhoji mipaka ya kijiografia ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Ni sababu nzuri kuzuia watanzania wasijadili mipaka ya Tanzania bali Muungano uboreshwe.

Ukiruhusu watanzania wajadili na hata kupiga kura ya kuukataa Muungano kwa kisingizio kuwa hawakuulizwa kabla ya kujiunga na Muungano ni uendawazimu na ufinyu wa fikra. Kwani kila mkataba wa kimataifa ambao Tanzania iliusaini/inaousaini ni mwananchi yupi aliulizwa? Mikataba ya kimataifa husainiwa na Raisi wa nchi kwa niaba ya wananchi na nchi bila kupata ruhusa ya moja kwa moja ya wananchi. Hakuna mwananchi ambaye amewahi kupiga kura ya maoni ili kutoa ruhusa kwa serikali kusaini mkataba wa kimataifa. Isipokuwa mikataba hiyo baada ya kusainiwa na Raisi, hujadiliwa na kuridhiwa na Bunge kabla ya kuanza kutumika Tanzania.

Si haki ya Mzanzibar wala ya Mtanzania Bara kuwa alipaswa aulizwe kabla ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume kusaini mkabata wa Muungano ambao ni mkataba wa kimataifa. Hakuna haja ya kuwauliza watanzania kama wanapenda Muungano au la! Iwapo watanzania wataukataa Muungano; kwangu huo utakuwa ni uwazimu. Kwani hata Zanzibar nje ya Muungano; wapemba au waunguja watasema hawakuulizwa kabla ya Pemba na Unguja kuwa Taifa la Wazanzibar.

Hivyo nje ya Muungano; Pemba na Unguja pia lazima zitajitenga: kama Pemba itapiga kura isiwe sehemu ya Zanzibar na Unguja nayo ipige kura ya maoni isiwe sehemu ya Zanzibar; je kutakuwa na hiyo Zanzibar ambayo Uamsho wanaidai!

Kwa Tanzania Bara, vilevile iwapo raia wa Tanzania Bara watapiga kura ya Maoni kujitoa katika Muungano basi tujue madhara na hasara yatakayo patikana baada ya kurudi kwa taifa la Tanganyika ni makubwa kuliko hata changamoto za Muungano. Nje ya Muungano; wasukuma, wagogo, au wanyakyusa watahoji kuwa hawakuulizwa ili wakubali wawe sehemu ya Tanganyika. Na makabila mengine pia yatasema hivyo hivyo na hata watanganyika katika mikoa au kanda watasema wapige kura kwani mkumbuke watanganyika hawajawahi kupiga kura ya maoni kukubali kuwa watanganyika.

Mfano wasukuma au watu wa kanda ya ziwa au hata kabila dogo kama wakerewe wapige kura ya maoni kujitoa katika Tanganyika; Je, kutakuwa na Tanganyika hapo?

VYOMBO VYA HABARI VINAVYOHARIBU MUUNGANO

Televisheni ya Taifa (TBC) inayoendeshwa kwa kodi za Watanzania mwezi Aprili ilirusha kipindi cha This Week Perspective. Mmoja wa wageni waliyoalikwa ni wakili maarufu Harold Sungusia yeye hujitambulisha kama mwanaharakati wa haki za binadamu ila mimi huwa namuona ni shabiki wa Chadema na si mtetezi wa haki za binadamu. Ndg. Sungusia huwa hasifiii mazuri ya CCM, yeye husema mabaya ya CCM tu na mabaya ya Chadema huwa hayasemi kabisa hata kwa bahati mbaya. Ndiyo maana mimi humwona yeye kama shabiki wa Chadema na si mwanaharakati wa haki za binadamu. Mgeni mwingine katika kipindi hicho alikuwa ni Ndg. Hans Kitine. Huyu amewahi kuwa Waziri, Mbunge na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa. Baada ya kushindwa ubunge, Ndg. Kitine amekuwa na mawazo hasi kabisa juu ya CCM na serikali yake. Mwendesha kipindi hicho ni mwandishi mkongwe Adam Simbeye. Kipindi cha siku hiyo kilikuwa kinajadili kuhusu miaka 48 ya Muungano wa Tanzania.
Kwanza nilimshangaa Mzee Kitine anayesema Muungano ni mzuri ila wananchi hawakuulizwa kama wanataka Muungano. Alipokuwa serikali mbona hakuuliza hivyo? Yeye kama Mbunge na Waziri alifanya lipi jema kwa Muungano? Baada ya kushindwa ubunge amekuwa akiulaumu CCM na kusema itakufa! Mimi naamini hata yeye Kitine amechangia matatizo ya CCM. Ndg. Kitine amesahau alivyofuja hela za umma kwa matibabu hewa ya mkewe huko Kanada. Kama aliweza kuwa Mkurugenzi wa Idara nyeti kama Usalama wa Taifa na bado hana uwezo hata wa kiintelejensia wa kujua kuwa Zanzibar ikiwa nje ya Muungano itagawanyika katika Upemba na Uunguja! Na Tanganyika ikiwa nje ya Muungano itakawanyika vilevile katika makabila au ukanda!

Hivi Mzee Kitine, Usalama wa Taifa aliongozaje kama hajui kuwa nje ya Muungano; Tanzania Bara nayo itataka ipige kura ya maoni ili Watanganyika wakubali kuwa sehemu ya Tanganyika.

Wewe mzee Kitine unasema Watanganyika hawakuulizwa kuwa watanzania! Je, ni lini basi Wazanzibar waliulizwa kwa kura ya maoni ili wawe wazanzibar? Na ni lini Watanganyika waliulizwa kwa kura ya maoni ili wawe watanganyika?

Mwaka 1964, Mzee Kitine ulikuwepo na upo hadi leo! Mbona hukuomba kura ya maoni? Mawazo ya Mzee Kitine yaliungwa mkono na wageni wengine akiwepo na Ndg. Harold Sungusia na mwendeshaji wa kipindi Ndg. Adam Simbeye.

Namshangaa Harold Sungusia ambaye ni mwanasheria na ninaamini anajua Sheria ya kuondoa utawala wa Machifu, namba 53 ya 1963 (Chiefs Abolition of Office: Consequent) Act. Sheria hii iliondoa utawala wa machifu na kulipa fidia kwa machifu. Na baada ya hapo machifu walitumiwa katika nafasi mbalimbali za uongozi wa nchi kama Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, mabalozi na watumishi katika serikali ya Tanganyika. Je, Sungusia unataka kila kabila la Tanganyika hivi leo tupige kura ya maoni ya kukubali, au kukataa uchifu kwani hakuna kabila lililoulizwa kabla ya machifu kuondolewa!

Mimi napendekeza TBC itafakari sana uwezo wa Simbeye katika kuongoza kipindi hicho. Kama tunataka kulinda maadili ya Taifa basi TBC mjue ni nani anayepaswa aalikwe katika vipindi vyenu ili kuepuka upotoshaji kwa umma.
Hivi Sungusia hujui kuwa mikataba yote ya kimataifa kama ilivyokuwa kwa mkataba wa Muungano baina ya Zanzibar na Tanganyika wananchi huwa hawaulizwi. Isipokuwa Bunge tu kwa mujibu wa Ibara ya 63 ya Katiba ya Tanzania ndiyo lenye mamlaka ya kuudhibitisha mkataba wa kimataifa ili uanze kutumika katika nchi kama sehemu ya sheria za Tanzania.

Ni lini wewe Sungusia, Simbeye na Kitine mlipiga kura ya maoni kukubali Tanzania ijiunge na Umoja wa Mataifa, SADC, EAC, Comesa, South Commission, AU, WTO, World Bank, IFM, Nchi zisofungamana na upande wowote (Non-Alignment Movement), Jumuiya ya Madola, na nyinginezo?

Hebu acheni ubaguzi. Ukiona mtu anataka watanzania wapige kura ya maoni kuukubali au kuupinga Muungano wetu ujue kuwa huyo mtu ni mbaguzi mkubwa. Tafadhali usimjali na usimsikilize kabisa, mtu huyo ni wa kuogopwa sana.

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, tarehe 13 Machi 1995 alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika hoteli ya Kilimanjaro alitoa moja kati ya hotuba zake kali alizozitoa mwishoni kabisa ya maisha yake na mimi huichukulia hotuba hii kama wosia. Mwalimu alisema hivi na hapa namnukuu:-

"Kwangu Muungano (Tanzania) ni muhimu kuliko jambo lolote….. nje ya Muungano wazanzibar mtajikuta kuna wazanzibar na wazanzibara … nje ya Muungano wa Tanganyika mtaongelea ukabila….Hamwezi mkakaa salama baada ya kutenda dhambi ya kuwabagua watu wa nchi yenu ile ile moja mkawaita wale 'wao' na hao 'sisi'. Dhambi ile ya ubaguzi haiishii hapo. …….Huwezi kufanya ubaguzi wa namna hiyo halafu dhambi ile ikuache hapo hapo…….hiyo dhambi itakuandama tu…..Mkipate Boris Yelstin wenu hapa atawetenganisha."

Licha ya hotuba hii nzuri ya Mwalimu bado wazee wangu Simbeye na Kitine, hawaelewi Muungano. Nguli Sungusia naye vilevile. Nawashangaa watu hawa wanakuwa na mawazo kama ya kikundi cha kibaguzi cha Uamsho.

Hata gazeti la Mwananchi limekuwa likichochea Muungano uvunjwe. Gazeti hili linamilikiwa na wanahisa kutoka nchi jirani ya Kenya. Hivi nyinyi watu wa Mwananchi mbona hamjaenda Kenya kusema kilomita 25–50/maili 16–31 ya pwani ya Kenya (Mombasa na Lamu) zijitenge na Kenya na ziwe sehemu ya Zanzibar. Kwani wakati wa utawala wa Sultani wa Zanzibar zilikuwa sehemu ya Zanzibar.

Nawaonya wanaharakati na waandishi wa Tanzania. Jiangalieni yasije yakawapata kama yaliyompata Arap Sang. Arap Sang alishangaa sana jina lake lilipotajwa kuwa mmoja wa watuhumiwa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Wakati mwandishi wa habari anavunja sheria anaweza asijue kama anavunja sheria lakini kutokujua sheria si utetezi.

Ni lazima watanzania tujifunze kuheshimu mipaka iliyowekwa na wakoloni na mipaka iliyowekwa na Muungano. Historia lazima isonge mbele, tupende tusipende. Haya ndio mabadiliko ambayo watanzania tunapaswa tuyafuate. Asiyekubali mabadiliko haya, mabadiliko yatambadili mpaka atakapokubali kubadilika.

WANASHERIA WAACHE KUCHOCHEA KUUA MUUNGANO.

Wanasheria wenzangu tusiwadanganye watu kwa kutaka umaarufu. Si kweli kuwa kila jambo muhimu la nchi lazima kura ya maoni ipigwe ili kuamua nini kifanyike. Ikiwa kura ya maoni ni yakupigwa kila mara, basi kila mwezi na kila wiki tunaweza tukawa na kura ya maoni kwa vile yako mambo mengi ya nchi yakuyapigia kura.

Siyo kila jambo ni lazima kwa watanzania au wananchi watoe maoni yao. Yako masuala hayaitaji maoni ya wananchi labda tu kama maoni hayo ni ya kuyaboresha.

WANAHARAKATI WA KUDAI UZANZIBAR.

Ninyi mnaojiita wanaharakati wa kudai Uzanzibar nje ya Muungano na utanganyika nje ya Muungano. Mbona hamuwaulizi wazazi wenu kwanini hawakuwauliza KAMA MNATAKA kuzaliwa kabla ya kuwaleta duniani?

Ni kwa nini hamjahoji kwanini umezaliwa mzanzibar, mchaga au mrangi? Muungano ndio asili yetu anayeukashifu sidhani kama akili zake ziko sawa. Msomi Harold Sungusia anasema …… 'miaka 48 ya Muungano haina kitu'. Na kuongeza kuwa …. 'Muungano ni kama binadamu mwenye magonjwa mengi'. Sungusia alikejeli pia na kusema Muungano ni kama mwanamke aliyejichubua na dawa haramu za kutoa weusi katika ngozi (mkorogo). Sikubaliani na mifano mfu anayoitumia "mwanaharakati" huyu.

Mimi hupenda kuufananisha Muungano na ndoa. Ingawaji wanasiasa wengi hawapendi mfano huu ila mimi lazima niutumie ili masikio yenu yasikie na akili zenu zielewe maana ya Muungano.

Ndoa ni Muungano wa hiari wa mwanamke na mwanaume ambao wanategemea kuishi kwa maisha yao yote kwa mujibu wa Kifungu cha 9 Cha Sheria ya Ndoa ya Tanzania, Namba 5 ya 1971.

Kwa hiyo Muungano lazima uwe wa maisha yote; ikitokea unafunga ndoa ni lazima iwe kwa maisha yote. Talaka ni bahati mbaya katika ndoa kwani saa ya kuungana hakuna anayepaswa kuwaza talaka. Muungano pia ni hiari – hiari ya nchi na si hiari ya wananchi. Maslahi ya kila mwananchi ni tofauti na maslahi ya nchi. Nchi kwanza mwananchi baadaye. Hata ndoa ni Muungano wa hiari-hiari ya mwanamke na mwanaume, siyo hiari ya wazazi, ndugu, marafiki, majirani, miiko, mila au hata dini.

Muungano kama ilivyo ndoa, hakuna ndoa hata moja isiyokuwa na matatizo au changamoto. Jambo la msingi katika ndoa ni kukabiliana na changamoto za ndoa bila kuumiza upande wowote ule.

Tusidanganyike Watanzania kuwa upo Muungano duniani ambao hauna matatizo. Na hata nje Muungano, matatizo ya Zanzibar au Tanganiyika yatakuwa mengi kuliko hata kero za Muungano. Kero za Muungano zinaweza kutatuliwa hata kero hizo zikiisha nyingine mpya zitafuata.

KWANINI UPANDE FULANI WA MUUNGANO UNANUFAIKA NA MWINGINE HAUNUFAIKI?

Ukiwauliza baadhi ya Wazanzibar watakuambia Zanzibar inanyonywa na Tanzania Bara. Watasema Zanzibar ilipoteza kiti chake UNO! Zanzibar haina ubalozi nje ya nchi! Zanzibar haina dola, Zanzibar inapewa mapato kidogo ya Muungano, Zanzibar haipewi nafasi za kutosha katika serikali ya Muungano, Wazanzibar wananyanyaswa, wazanzibar hawakushirikishwa katika kujiunga na Afrika Mashariki, Zanzibar imezuiwa kujiunga na OIC. Vilevile wazanzibar hao husema Zanzibar inazuiwa isiwe na wimbo wake wa Taifa na mengine mengi ni madai ya kibaguzi ya kudai Zanzibar ijitoe katika Muungano.
Kama nilivyoeleza katika ndoa. Si kila mwanandoa atanufaika kwa kiwango sawa sawa na mwenzie. Hebu firikiria ndoa ambayo mwenzi mmoja anatoka katika familia tajiri na mwenzi mwingine anatoka katika familia fukara. Ni dhahiri mwenzi anayetoka katika familia fukara atafaidi zaidi kiuchumi kwa kuwa na mwenzi anayetoka katika familia tajiri. Na mwenzi anayetoka katika familia tajiri hawezi kunufaika kiuchumi kutoka kwa mwenzi wake anayetoka katika familia duni. Hata mwenzi mwenye kipato kidogo atafaidi zaidi iwapo mwenzi wake atakuwa na kipato kikubwa.

Kwenye ndoa kuna mwingine lazima abebe mimba na mwingine habebi mimba. Kuna anayenyonyesha na mwingine hanyonyeshi. Sasa katika Muungano au ndoa kila upande ukitaka uwe sawasawa kimajukumu na kimaslahi itawezekana kweli; haiwezekani kabisa.
IDADI YA MAJIMBO YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR

Hadi leo hii, Wazanzibar wapo Milioni Moja (1,000,000) lakini wana majimbo hamsini ya ubunge wa Muungano wakati wilaya ya Kinondoni ina wakazi Milioni Moja na Laki Tisa (1,900,000) lakini ina majimbo matatu ya uchaguzi! Je ni nani anayefaidi kutokana na Muungano hapa!? Nashangaa wazanzibar kusema wananyonywa na Muungano.

MGAWANYO WA MAPATO YA MUUNGANO KWA IDADI YA WATU

Tunaweza kuchukua uwiano wa idadi ya watu katika kugawana mapato ya Muungano. Katika mapato ya Muungano, Zanzibar inapewa 4% ya mapato ya Muungano na Tanzania Bara inachukua 96% ila ikumbukwe kuwa Wazinzibar ni asilimia 2.5% ya Watanzania. Lakini bado Zanzinar inasema kuwa 4% ya mapato ya Muungano haiwatoshi!

MAMBO AMBAYO ZANZIBAR IMENUFAIKA NAYO KATIKA MUUNGANO

Ulinzi na amani umeimarika Zanzibar kwani baada ya mapinduzi ya Zanzibar, wengi waliamini Zanzibar ingepinduliwa kama nchi nyingi za Afrika ambazo zilikuwa na Mapinduzi kwa wakati huo.

Zanzibar inashiriki vizuri katika masuala ya Muungano. Zanzibar ina wabunge hamsini wa majimbo katika Bunge la Muungano licha ya Zanzibar kuwa na wananchi karibu 1,000,000. Wilaya ya Kinondoni ina wakazi 1,900,000 lakini ina wabunge watatu katika Bunge la Muungano.

Wafanyabiashara wengi wa Zanzibar wamejenga nyumba za makazi, nyumba za biashara na kuwekeza biashara zao katika ardhi ya Tanzania. Fursa hii wasingeipata kwa Zanzibar kwani Zanzibar ina soko dogo yaani watu milioni moja tu!

Zaidi ya Wazanzibar laki tatu huishi na kufanyakazi katika ardhi ya Tanzania Bara. Biashara nyingi na kubwa za Zanzibar zimewekezwa Tanzania bara na faida ya biashara hizo hurejeshwa nyumbani Zanzibar.

Ikumbukwe kuwa Mzanzibar anaruhusiwa kumiliki ardhi bara, kugombea ubunge/udiwani wa jimbo la Tanzania Bara. Lakini Mtanzania wa Tanzania Bara haruhusiwi kumiliki ardhi Zanzibar na haruhusiwi kugombea ubunge/ udiwani huko Zanzibar. Hii ni faida ya aina yake ambayo Zanzibar inaipata katika Muungano.

Zanzibar imeweza kupata mapato kutokana na mapato ya Muungano ambayo husaidia kuendesha serikali na kuleta maendeleo ya Zanzibar.

Zanzibar pia imekuwa inachangia pato la Muungano mfano makusanyo ya kodi kwa mwaka 2009/10 Zanzibar ilikusanya kodi ya mapato Shilingi Bilioni 1 na Tanzania Bara kwa kipindi hicho ilikusanya Shilingi Bilioni 1,498 sawa na asilimia 99.93% ya makusanyo yote ya kodi za Muungano. Lakini katika kugawana, licha ya Zanzibar kukusanya chini ya 1% ila hupewa 4%.

Yapo maendeleo mengi ya kiuchumi kisiasa na kiutamaduni ambayo Zanzibar inanufaika na Muungano.

KWA NINI TANGANYIKA NA ZANZIBAR ZILICHUKUA MFUMO WA SERIKALI MBILI BAADA YA MFUMO WA SERIKALI TATU AU MOJA?

Ili kulinda utamaduni na mapokeo ya Zanzibar ilionekana ni busara sana kwa serikali ya Zanzibar ibaki ikiwa na nguvu ya kuendesha mambo machache kwa ajili ya Wazanzibar.

Hivyo basi busara ilionesha serikali ya Tanganyika iondoke na Tanganyika na Tanzania zitatumia serikali ya Muungano kwa masuala yote.

Hakuna shaka kuwa hata mifano ya Uingereza ilizingatiwa katika Muungano huu wa Tanzania.

Mfumo wa serikali tatu ulionekana utaleta gharama kubwa katika uendeshaji. Mfano serikali tatu zingeleta mabunge matatu, serikali tatu na Taasisi tatu hata kwa masuala machache tu. Muungano wa serikali tatu pia si Muungano moja kwa moja.

Kwa kawaida sheria zote za Tanzania hutungwa si tu kwa kuzingatia katiba ya nchi bali hata kwa kuzingatia mila, desturi na maadili ya Tanzania. Inajulikana kuwa Zanzibar ni nchi tangu Sultan wa Omani alipoingia Zanzibar mwaka 1698 hivyo isingekuwa busara serikali ya Zanzibar kuondoka kama ya Tanganyika.
Utaifa wa Zanzibar tayari ulikuwa umeenea na kukuza biashara na watu wengi wa nje. Kwa sababu za kuvutia utalii ilikuwa bora kwa serikali hiyo kubaki.

Kihistoria ilionekana ni vema serikali ya Zanzibar ibaki ili kuweka sawa historia kwa kuihifadhi na kuifundisha kwa vizazi hadi vizazi na kuwafundisha wageni na watalii pia.

Ilionekana ni vema kwa Zanzibar iwe na serikali yake kwa ajili ya masuala machache yasiyokuwa ya Muungano hadi leo hii Zanzibar ni nchi isiyokuwa na dola na isiyokuwa na mamlaka kamili. Zanzibar ina mamlaka yote isipokuwa masuala 22 ambayo yametajwa katika jedwali la kwanza la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

KWA NINI ZANZIBAR NA TANGANYIKA ZILIUNGANA?

Zanzibar na Tanganyika ziliungana na kuwa dola moja na Taifa moja. Historia ya mataifa haya zinafanana. Karibu 40% ya Wazanzibar asili yao ni Tanganyika. Watanganyika walioenda kuuzwa katika soko la watumwa pale Zanzibar na kwa bahati hawakununuliwa kutokana na kutokuwa na nguvu au kwa sababu yeyote ile walibaki Zanzibar na hawakurudishwa Tanzania Bara. Watumwa walipotoka Bara na kufikishiwa soko la watumwa Zanzibar walionunuliwa ni wale wenye nguvu na afya na ambao hawakununuliwa walibaki Zanzibar kama watu huru na hawakurudishwa makwao huko Bara. Historia ndio ambayo hufanya watu kuwatania Wazanzibar kuwa ni wavivu! Ndio maana kazi au mzigo ukiwa mzito; wazanzibar husema mzigo mzito mbebeshe mnyamwezi (kwa Kiswahili cha Zanzibar: mnyamwezi ni jina linalotumika kumaanisha mtu wa kutoka Bara). Hata hivyo mimi siamini kuwa wazanzibar ni wavivu. Kila kabila lina watu wavivu. Pia naona biashara za Wazanzibar hata zilizoko hapa Bara zimeendelea kukua siku hadi siku. Sasa kama ni wavivu wangeendelezaje biashara zao kwa kasi kubwa namna hii!

Jamii ya watu weusi karibu wote wa Zanzibar walitoka Tanzania Bara. Ndio maana ya kuwa na Wazanzibar wenye majina ya Kisukuma, Kinyamwezi, Kinyakyusa na majina ya makabila mengine ya Bara. Mfano ni Marehemu Adam Mwakanjuki, Jaji Othman Makungu, majina kama Bundala, Shija na mengineyo.

Ilionekana ili kuweza kulinda mipaka ya baharini ya Zanzibar na Tanganyika ni vema kwa nchi nizi kuungana na kuwa na jeshi imara la umoja la kulinda mipaka ya nchi hizi. Kutokana na machafuko yaliyofanywa na USA katika kisiwa cha Cuba kati ya mwaka 1955 hadi 1958 baada ya Fidel Castrol kuipindua Cuba. Zanzibar ilionekana ni kisiwa ambacho kingeweza wavamiwa na mabeberu wa magharibi na kwa namna yeyote ile wangeathiri uhuru si tu wa Zanzibar bali hata Tanganyika na Afrika yote. Hata watu wa magharibi walidhani Zanzibar itakuwa kama Cuba hivyo nao walitaka kuiangalia na kuidhibiti.

Mawazo ya kizalendo ya kiafrika yaliwasukuma waasisi wa Muungano na kuona ni vizuri kuunganisha Zanzibar na Tanganyika. Busara hiyo ilitegemea kuwa nchi nyingine za Afrika nazo sitaungana kikanda (regional cooperation) na baadaye kuwa na taifa moja la Afrika. Zanzibar na Tanganyika ndio zitakuwa mfano wa kuigwa. Na kwa kweli mpaka leo hii Muungano huu ni wa mfano kwa bara zima la Afrika.

MGAWANYO WA MADARAKA NA NAFASI KATIKA MUUNGANO

Baada ya Muungano nafasi zote za Muungano ziligawanywa kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Sheria ya Muungano ilimfanya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Kwanza wa Raisi wa Muungano na Raisi wa Zanzibar alikuwa anakuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri wa Muungano.

Bunge la Muungano lilipokea wabunge kutoka Zanzibar na nafasi zote za Muungano ziligawanywa kwa usawa kutoka pande zote za Muungano.

KIKUNDI CHA UAMSHO NA KUPINGA MUUNGANO

Matukio ya mwishoni mwa Mei 2012 Jijini Zanzibar, mkoani Mjini Magharibi, Unguja.  Kama tujuavyo sote kulitokea ghasia zilizochochewa na viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu maarufu kwa jina la Uamsho.  Taasisi hii imeanzishwa kwa madhumuni ya kidini, lakini hivi sasa viongozi wake wameamua kuyaacha madhumuni hayo na kubeba ajenda za siasa. Matukio haya pia hayajaanza mwaka huu, yapo muda mrefu ila chini chini na yanaendeshwa na watu pia wanafundishwa jinsi ya kupigana na vyombo vya dola na wale wote wenye mapenzi mema na Tanzania.

Siku za nyuma, hawa viongozi wa kundi hili, wakitumia muda mwingi kuilaumu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa lawama hizo sasa hazisikiki.  Lakini, mara tulipoanzisha mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mihadhara yao imeelekezwa kupinga Muungano na kuwakashifu viongozi waasisi wa Muungano na hata waliopo sasa.  Isitoshe wamekuwa wakipandikiza chuki dhidi ya ndugu zao wa kutoka Tanzania Bara na wale wafuasi wa dini ya Kikristo.

Baya zaidi, katika uchochezi huo majengo na mali za Makanisa mawili  zilichomwa moto, maduka ya watu kuvunjwa na mali zao kuibiwa.  Kwa kweli vitendo hivi ni uhalifu ambao haukubaliki na wala hauvumiliki.  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kauli yake alisema katika mkutano wake na waandishi wa habari ya kukemea vikali na kulaani uhalifu huo. 


Ni jambo la kusikitisha na kushangaza kwamba, wenzetu hawa wamefanya uhalifu huo kwa hoja ya kupinga Muungano.  Haiwezekani mtu anayepinga Muungano, akaitetea hoja yake kwa kuchoma moto makanisa au kuvunja maduka ya watu na kupora mali zao.   Ukristo haukuingizwa Zanzibar na Muungano, bali ulikuwepo karne kadhaa kabla ya Muungano na wala haukutokea Tanzania Bara. Na kama alivyoeleza Mheshimiwa Rais Ali Mohamed Shein jana, ukweli ni kwamba, dini ya Kikristo kama ilivyo ya Kiislamu imeenezwa Bara kutokea Zanzibar.  Kanisa kuu la Anglikan Zanzibar lilijengwa kuanzia mwaka 1873 na lile la Katoliki kuanzia 1893 ni miongoni mwa Makanisa makongwe kuliko mengi kama siyo yote kwa upande wa Afrika Mashariki si Zanzibar na Tanzania Bara tu. 

Katika hotuba yake ya kuwalaumu, Mheshimiwa Rais, Dkt. Ali Mohamed Shein, pamoja na kueleza kwa ufasaha ukweli huu, pia alisisitiza suala la haki na uhuru wa Kikatiba wa mtu kuchagua au kubadilisha dini au imani yake (Ibara ya 19 ya Katiba ya Zanzibar na Ibara ya 19 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano). Katika kutumia uhuru huo, mtu hastahili kuingiliwa au kulazimishwa na mtu yo yote. Hayo pia ndiyo matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Kwa kweli yanayofanywa na ndugu zetu wa Uamsho ya kuchoma moto makanisa siyo sawa hata kidogo.  Na, wanapoyafanya kwa kisingizio cha Muungano ni jambo lisiloeleweka kabisa na wala halina mantiki.  Labda wenzetu wana lao jambo ambalo ni kuleta chuki za kidini. Wapo baadhi ya viongozi wa kundi hilo wamekuwa wakisafiri nchi nzima, bara na visiwani kuhamasisha waumini wa uislamu kudai taifa hili liwe la kiislamu. Katika mafundisho yao ambayo nimepata kuiona nakala ya mafundisho yao katika CD; Mkufunzi huyo amesema kuwa wako tayari kufa au kuuwa ili mradi tu nchi hii iwe ya kiislamu. Mkufunzi huyo amesema kuwa; kufa kutawapeleka mbinguni na kuuwa kutawapeleka mbinguni. 

Jambo lingine la kushangaza zaidi ni kule kutokea vurugu na ghasia hizi dhidi ya Muungano wakati ambapo Serikali imetoa fursa sasa kwa watu kutoa maoni yao kwenye mjadala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.  Kama tujuavyo sote, Tume ya Katiba imekwishaundwa na inajiandaa kupita kote nchini kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba mpya waitakayo.  Kama mtu ana maoni yake kuhusu Muungano, hiyo si ndiyo fursa ya kufanya hivyo.  Utaratibu mzuri umewekwa kwa ajili yetu sote, vurugu za nini? Ubaguzi wa kidini wa nini?

Mimi sioni sababu ya msingi ya kusababisha kuvurugika kwa  amani kwa jambo ambalo limewekewa utaratibu muafaka wa kulishughulikia. Nawaomba tutumie utaratibu mzuri uliowekwa badala ya kufanya mambo yanayoleta mifarakano katika jamii na yanayosababisha uvunjifu wa amani na kuharibu sifa na sura ya Wazanzibari na Watanzania.   

Serikali lazima ifanye na isisite kuchukua hatua kali dhidi ya watu hawa wahuni wa uamsho.  Watanzania wajiepushe na ajenda za kisiasa na kupandikiza chuki zitakazosababisha mifarakano baina ya wananchi wa pande zetu mbili za Muungano na baina ya Wakristo na Waislamu.

Uamsho wamesema Zanzibar inanyonywa katika Muungano. Labda niulize!? Zanzibar ina wananchi Milioni Moja tu lakini ina majimbo 50 katika Bunge la Muungano wakati wilaya yangu ya kinondoni ina wakazi Milioni Moja na laki tisa ila ina majimbo matatu tu katika bunge la Muungano. Je ni nani anaemnyonya mwenzie?

Nauliza tena, Wazanzibar wanaruhusiwa kugombea ubunge jimbo lolote Tanzania Bara na pia wanaruhusiwa kumiliki ardhi Tanzania Bara lakini mtanzania bara haruhusiwi kugombea ubunge wala kumiliki ardhi Zanzibar. Je ni nani anaemnyonya mwenzie?

Ikumbukwe kuwa watanzania ni ndugu na wamekuwa wakiishi pamoja kwa upendo na furaha licha ya tofauti zao za rangi, makabila, dini na maeneo watokako. Kimeharibika kipi hata leo yatokee haya? Naamini kuwa wapo baadhi ya viongozi wetu wa kisiasa ambao wamechochea harakati za Uamsho. Uamsho kama yalivyo makundi haramu kote duniani yana mkono wa wanasiasa. Siwezi amini tofauti na hivyo. Kama kundi haramu la Mungiki pale Kenya na Uamsho ni hivyo hivyo.

Wenye maoni kuhusu Muungano wetu, muundo wake na uendeshaji wake watumie fursa ya mjadala wa Katiba kutoa maoni yao.  Hatuhitaji kufanya ghasia kutoa maoni kuhusu Katiba.


Hali kadhaliak nawapongeza vijana wetu wa Jeshi la Polisi kwa juhudi kubwa waliyoifanya ya kudhibiti hali ambayo mwelekeo wake haukuwa mwema.  Nawaomba waendelee kuwa macho ili watu wasioitakia mema nchi yetu na watu wake wasipate nafasi ya kutuvurugia amani na utulivu wetu.  Naamini tukidumisha utamaduni wetu wa kuheshimiana, kuvumiliana, kuzungumza pale tunapotofautiana na hata kukubali kutokukubaliana hakuna litakaloharibika. Haya shime tufanye hayo.

MAPENDEKEZO YANGU KUHUSU UAMSHO

Ninapendekeza kuwa Kikundi hiki cha Uamsho kifutiwe usajili na kifungwe, kwani kama walisajiliwa kufanya shughuli za kidini, imekuaje wakaanza kufanya mihadhara ya masuala ya siasa?

Kundi lolote lile au mtu yeyote yule anaye kashfu viongozi waasisi wa taifa letu na viongozi waliopo madarakani washtakiwe mara moja.

Wananchi waelimishwe kuhusu faida za Muungano na vikundi vinavyochochea udini vifungwe na Serikali.

Uamsho wametoa CD zenye matusi ya kukashifu wakristu, Serikali iwashitaki kwa kosa la kuingilia uhuru wa dini nyingine.

Serikali ihakikishe usalama wa mali na maisha ya wananchi. Waandishi wa habari waache kuandika habari za Uamsho. Viongozi wa Uamsho wakiitisha mikutano na waandishi wa habari, ndugu wana habari msiende. Tafadhari sana. Nyinyi waandishi wa habari mnapoenda kuwasikiliza wale wendawazimu na wabaguzi wakubwa mnakuwa mnawapa nguvu ya kuendelea kubagua na kuleta fujo. Ndugu wanahabari, jiangalieni msije mkawa kama Arap Sang wa Kenya. Arap Sang alikuwa akitangaza tu habari za kibaguzi kama alivyozipokea kutoka kwa wabaguzi na wafanya fujo. Kitendo hicho kimempeleka the Hague.

Nanyi wanahabari wa Tanzania hakika nawaambieni, ipo siku mtapelekwa the Hague wakati Uamsho watakapopelekwa pia. Mtabaki mnazubaa kama Arap Sang mkiulizana. Mbona mimi ni mwanahabari na sikushika silaha kuuwa? Bali niliandika yaliyokuwa yakitokea tu?

Katika kuandika habari, mwana habari hauruhusiwi kuandika habari za uchochezi au za kibaguzi. Hotuba zote za Uamsho ni za kibaguzi. Inakuwaje sasa wanahabari mnaziandika. Mimi naomba niwalaumu na nyinyi pia kwa kutumia muda mrefu kuwahoji viongozi wa Uamsho na wafuasi wake bila kupata hata dakika moja tu ya kutuhoji sisi waumini wa Muungano au kuhoji watu wenye dhamana ya kuulinda Muungano.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ubariki Muungano.

Imeandikwa na Ndugu Emmanuel Makene, wakili wa kujitegemea na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Kinondoni.

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment