Habari za kazi?
Nina maswali ambayo yananitatiza kidogo. Hivyo si vibaya nikashare na wengine na kama ni wasiwasi wangu tu basi nifahamu hivyo. Najiuliza maswali kadhaa kuhusu mchakato mzima wa kuandika katiba mpya.
Swali la kwanza: Je kwa mwendo huu tutaweza kuwa na katiba mpya ifikapo 2015, kabla ya uchaguzi?
Hali inavyokwenda sasa inanipa tabu kuamini kuwa katiba mpya itakuwa imepatikana by 2015. Kwa nini nina wasiwasi? Mpaka hivi sasa Tume haijaanza kazi! Ni lazima tukumbuke ukubwa wa nchi yetu na mambo mengine makubwa yanayoendelea kama vile sensa n.k. Aidha kuna mvutano wa kisheria juu ya Tume ya Katiba kuweza kufanya kazi Zanzibar kabla ya kuidhinishwa na Baraza la Wawakilishi. Pili baadhi ya Wazanzibari tayari wanaona tuwe na process tofauti, yaani kwanza tuwe na kura ya maoni kuwauliza wananchi iwapo wanautaka muungano ama hawautaki. Hii nayo ni changamoto nyingine itakayoleta mjadala mrefu.
- Bado haujapatikana muafaka wa namna Bunge maalum la kutunga katiba litakavyoundwa. Suala hili linaweza kuleta malumbano ya muda mrefu. Na kwa uzoefu wetu serikali yetu hukubali kupokea maoni pale inapokuwa imeshinikizwa kila kona na kila upande. Mashinikizo haya yatachelewesha process.
- Bado haujapatikana muafaka juu ya namna ya kuendesha zoezi la kura ya maoni. Aidha hakuna muafaka juu ya nani atasimamia zoezi hili la kura ya maoni.
- Pia zipo tofauti nyingine ambazo bado hazijapatiwa muafaka kama vile iwapo watanzania wengi wataikataa katiba mpya katika kura ya maoni, basi katiba ya zamani itaendelea kutumika. Hili bado nalo lina utata na linahitaji majadiliano ambayo yatachukua muda na kulifanya zaoei la katiba mpya kuweza kuchelewa sana.
- Hata suala la ni asilimia ngapi itakuwa considered kuwa imeshinda ni utata mtupu. Wapo wanaona kuwa asilimia iliyowekwa ni ndogo sana. Hivyo katiba inaweza kupita wakati imekatiliwa na nusu ya Watanzania. Iwapo hili litatokea huwezi kuita hiyo ni katiba Watanzania. Hili nalo lina utata na linaweza kuleta mjadala mrefu, kubadilisha sheria n.k. Natoa sababu hizi kuonyesha ni namna gani tunaweza tukafika 2015 hatuna katiba mpya kama ambavyo tunatarajia. Na iwapo itakuwa hivyo, maana yake nini? Hili linanipeleka katika swali langu la pili.
Je tupo tayari kuingia katika uchaguzi wa 2015 na katiba hii iliyopo?
Nina hakika Chama tawala kitafurahi kweli na kinaweza kudelay process ili tusipate katiba mpya by 2015 na tuingie katika uchaguzi tukiwa na katiba hii ya kisultani na watakwepa kuwajibika kwa hilo kwa kutoa visingizio mbalimbali. Je tupo iwapo itakuwa hivyo, tutakuwa na uchaguzi huru na wa haki? na jee haliwezi kutupeleka katika machafuko? Je tupo tayari kuingia katika uchaguzi na Tume hii ya uchaguzi?
Katika siku za mwanzoni, wapo waliopendekeza kuwa ni vyema mchakato wa kuandika katiba usiharakishwe, badala yake upewe muda wa kutosha, isiwe lengo 2015 tuwe na katiba mpya. Ili tuwe na uchaguzi huru na na wa haki 2015, Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ipeleke mswada wa kuunda Tume huru ya Uchaguzi, Ofisi huru ya msajili wa vyama vya siasa na ifanye marekebisho yote ya kisheria ili tuwe na uwanja sawa wa ushindani 2015, huku tukijipa muda wa kutosha kuandika katiba mpya. Watu kama kina Jenerali Uimwengu ndio walikuwa na mawazo haya. Nadhani kwa hali inavyokwenda mawazo yao tunaweza sasa kuanza kuwaelewa kwa nini walifikiria hivyo.
Swali langu la mwisho: iwapo 2015 hatuna katiba mpya ni nani atawajibika kwa hilo? Serikali? wanasiasa wote kwa ujumla? au nani? Tukumbuke kuwa tumeingia katika mchakato wa kuandika katiba mpya huku tukikabiliwa na mambo yafuatayo: ombwe la uongozi, hatuna uongozi ambao unaaminika una ushawishi na unakubalika; tuna tofautiana katika mambo mengi sana ambayo tulitakiwa tuwe na muafaka wa kitaifa juu ya mambo hayo miaka mingi iliyopita, lakini tulifanya ajizi na sasa mambo hayo yamekuwa ni magumu zaidi, yaani ni kama kidonda ndugu. Mambo haya yanaleta changamoto nyingi sana katika mchakato wa kuandika katiba. Hii imetokana na tabia ya serikali kutokushughulikia masuala kwa wakati na kuyaacha yakiota mizizi huku wakifikiria kuwa yatajitatue yenyewe. Akili ya mbuni kuficha kichwa chake katika mchanga pindi anapomuona adui. Mathalani chukua suala la muungano na suala la kadhi, haya tu yanaweza kutupa changamoto kubwa sana katika zoezi hili. Na kwa maoni yangu tulitakiwa tuwe na muafaka wa kitaifa zamani sana juu masuala kama haya na mengine.
Jamani nafikiria tu kwa sauti. Yawezekana huo ni wasiwasi wangu tu. Naomba kusikia kutoka kwenu.
Selemani Rehani
0 comments:
Post a Comment