HOTUBA YA JAJI WA MAHKAMA KUU ZANZIBAR MHESHIMIWA ABRAHAM MWAMPASHI
KATIKA UZINDUZI WA RIPOTI YA HAKI ZA BINADAMU YA MWAKA 2011
ITAKAYOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA BWAWANI RESTAURANT MJINI ZANZIBAR
TAREHE 14-06-2012.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar
Profesa Chris Maina Peter na watendaji wako mliohudhuria,
Waheshimiwa wawakilishi wa Taasisi mbali mbali za kiraia na Serikali
mliohudhuria,
Waheshimiwa waalikwa katika shughuli hii,
Mabibi na Mabwana
Asalamu Aleykum
Ndugu Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba kuchukua nafasi hii kutoa
shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa Kituo cha Huduma za Sheria
Zanzibar (ZLSC) kwa kunialika mimi kuwa mgeni rasmi katika sherehe za
uzinduzi wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2011.
Hii ni mara ya pili kupata nafasi ya kuwa mgeni rasmi katika shughuli
za Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar.
Shughuli ya kwanza niliyopata bahati kuwa mgeni rasmi katika kazi za
Kituo ni ile siku tuliokusanyika katika Ukumbi wa Grand Palace pale
Malindi kujadili haki za watoto na nafasi ya sheria.
Nilipewa heshima ya kufunga semina ile ya siku mbili iliyowajumuisha
Majaji wa Mahkama Kuu Zanzibar, Mahakimu wa Mahkama za Mikoa na Wilaya
kutoka Unguja na Pemba na Makadhi kutoka Unguja na Pemba.
Ndugu Mwenyekiti, huu ni uthibitisho kwamba Kituo kinathamini mchango
na nafasi ya Mahkama katika jamii na kipo tayari kufanya kazi na
Mahkama ikiwa ni miongoni mwa wadau wakuu katika sekta ya Sheria.
Aidha, ninafarijika sana kupokea kila mwaka nakala za Ripoti ya
Tanzania ya Haki za Binadamu zinazotolewa kila mwaka na Kituo cha
Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu (LHRC) kilichopo jijini Dar es Salaam.
Vile vile, ninafarijika kupokea nakala za Jarida la Sheria na Haki
linalochapishwa na Kituo na kutolewa kila baada ya miezi mitatu.
Ndugu Mwenyekiti, suala la haki za binadamu linaendelea kuchukua
nafasi muhimu katika ngazi za vijiji, vitongoji, mijini, taifa na
dunia nzima.
Taarifa zinazotolewa na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi
zinaelezea umuhimu wa kuheshimiwa haki za binadamu au namna haki hizo
zinavyokiukwa kwa namna moja au nyingine.
Ndugu Mwenyekiti, uchambuzi wa taarifa au ripoti za kitaalamu
zinazohusiana na haki za binadamu ni uthibitisho kwamba haki hizi
zinakiukwa na watu wenyewe, taasisi au hali ya vita vinavyozuka na
kuendelea katika pembe tofauti za dunia.
Naamini ukiukwaji huo unafanywa kwa makusudi ili kufikia malengo
maalum hususan malengo ya kisiasa na kupata madaraka yanayowezesha
udhibiti wa rasilimali za taifa.
Jambo linalouma na kusikitisha zaidi ni kwamba wakiukaji wa haki za
binadamu wanaachiwa kutamba mitaani bila ya kufikishwa katika vyombo
vya sheria (impunity).
Kitendo cha wakiukaji wa haki za binadamu kutochukuliwa hatua za
kisheria ni matokeo ya udhaifu wa sheria za nchi husika, kulindana au
kuogopana.
Ndugu Mwenyekiti, asasi za kiraia zina jukumu kubwa kufanya ushawishi
wa kuheshimiwa haki za binadamu na kuchukuliwa hatua dhidi ya wote
wanaokiuka haki za binadamu.
Njia za kufanya ushawishi wa kuheshimiwa haki za binadamu au
kuchukuliwa hatua wale wanaozivunja zipo nyingi.
Kwa mfano, kazi hii inayofanywa na asasi hizi mbili (ZLSC na LHRC) ya
kufanya utafiti, kufanya tathmini, kuchapisha ripoti na hatimaye
kuzisambaza ni jambo zuri.
Ndugu Mwenyekiti, ripoti hizi mnazozitoa zitawafichua, zitawaumbua,
zitawaamsha wanajamii na zitakuwa kumbukumbu kwa vizazi vijavyo ili
kuepuka kasoro zinazofanywa sasa.
Ninaamini taasisi makini ambazo zimeguswa katika ripoti hii kwa njia
ya moja kwa moja au njia ya kuzunguka zitashtuka na kujirekebisha.
Aidha, wale ambao wanahisi haki zao zimevunjwa watapata changamoto ya
kuzidai kisheria.
Ndugu Mwenyekiti, ninafahamu kwamba ripoti hii imegawika sehemu mbili
kuu. Sehemu ya kwanza ya ripoti imejikita zaidi kwa upande wa Tanzania
Bara. Na sehemu ya pili ya ripoti inahusu upande wa Zanzibar.
Ninafahamu kupitia vyombo vya habari kwamba Uzinduzi wa Ripoti hii kwa
upande wa Tanzania Bara ulifanyika mwishoni mwa mwezi uliopita jijini
Dar es Salaam. Sasa ni fursa yetu Zanzibar kuizindua Ripoti hii ya
Haki za Binadamu ya mwaka 2011.
Ndugu Mwenyekiti, naomba uniruhusu nichukue muda mdogo nizungumze
machache kuhusu haki za binadamu kwa upande wa Zanzibar kabla ya
kuizindua Ripoti yenu.
Pamoja na ukweli kwamba haki za binadamu zinaanza pale binadamu
anapozaliwa. Haki hizi ni za urithi wala hazitolewi na Katiba au
Sheria yeyote. Kazi kubwa ya Sheria ni kuzitambua, kuzilinda na
kuzitekeleza tu.
Lakini inaonekana kuwepo pengo kubwa la ufahamu wa haki za binadamu
hususan kwa mwananchi wa kawaida. Kwa msingi huu, ningeliishauri
taasisi yako na taasisi nyingine zinazosimamia haki za binadamu
kusimama kidete kutoa elimu zaidi ya haki za binadamu kwa nguvu zaidi
hapa Zanzibar.
Ndugu Mwenyekiti, matendo mengi yanayosababisha makosa ya ukiukwaji wa
haki za binadamu yanaweza kuepukwa ikiwa wananchi watakuwa na elimu ya
kutosha ya kuheshimu haki za binadamu.
Nitafurahi sana nitaposoma Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2012
ambayo itatolewa mwakani nikiona hatua zaidi zlizochukuliwa za utowaji
elimu ya haki za binadamu zimeelezwa na matokeo (outcome) ya ufanisi
katika jamii.
Haitoshi kuona idadi kubwa ya semina za utoaji wa elimu ya haki za
binadamu lakini tungelipenda kuona matunda au matokeo ya semina hizo
katika jamii. Swali kuu likiwa – Je! jamii yetu inabadilika au
tunaendelea na ule mtindo wa "mambo ni kama kawaida" – business as
usual.
Kwa mfano: Wazazi waliotalikiana wanaendelea kutoa malezi bora kwa
watoto wao, kuwatunza vizuri na kuwapatia huduma zote muhimu ikiwemo
elimu afya na upendo? Na wazee wasiojiweza wanahudumiwa? Uhuru wa
kutoa maoni na kuabudu unaheshimiwa?
Vile vile, sheria zilizomo katika vitabu vyetu vya sheria ambazo
zinaathiri haki za binadamu zingelianishwa na kupigiwa debe (advocacy)
kurekebishwa kwa faida ya jamii.
Ndugu Mwenyekiti, baadhi ya sheria hizo zinazoathiri haki za binadamu
ni Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Act No 6 ya 2004), Sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Criminal Procedure Act No 7 ya 2004),
Sheria ya Ushahidi (Evidence Decree, Cap 5) na Sheria ya Walemavu.
Sheria zote hizi zinahitaji kuangaliwa vizuri na kurekebishwa.
Jambo la mwisho ningelipenda kulisema hapa ni wananchi kushawishiwa
kutumia Mahkama katika kudai haki zao badala ya kulalamika mitaani;
kujichukulia sheria mikononi; au kutumia njia zilizo kinyume na
sheria.
Ninashawishika kusema kwamba muamko wa watu kutumia Mahkama kudai haki
zao hapa Zanzibar bado upo chini.
Ndugu Mwenyekiti, mwisho ninaomba kuchukua nafasi hii kwa mara
nyingine tena kuipongeza ZLSC na LHRC kwa juhudi zao nzuri za pamoja
za kutayarisha Ripoti ya Tanzania ya Haki za Binadamu ya kila mwaka
kuanzia mwaka 2006 bila kukosa na bila kutoa visingizio. Kila mwaka
tunasoma Ripoti ya Haki za Binadamu kuhusu Tanzania Bara na Tanzania
Zanzibar.
Ndugu Mwenyekiti, sasa napenda kutamka rasmi kwamba RIPOTI YA HAKI ZA
BINADAMU YA MWAKA 2011 IMEZINDULIWA HAPA ZANZIBAR.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
0 comments:
Post a Comment