HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI, MHE. RIZIKI OMAR
JUMA (MB), KUHUSU MAKADIRIO NA MATUMIZI YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS
MAMBO YA MUUNGANO KWA MWAKA WA FEDHA 2009/2010
….
Mheshimiwa Spika,
Wakati tunaheshimu sana na tunaamini njia ya mazungumzo kama suluhisho
la pekee kufikia utatuzi wa matatizo yanayolikabili taifa, hatuamini
kuwa mazungumzo kwa maana ya mazungumzo tu yanaweza kutufikisha
popote. Mazungumzo yenye uwezo huo wa kutoa suluhisho ni yale
yanayozingatia nini kinazungumzwa, nani wanazungumza, vipi na kwa nini
yanazungumzwa. Kila moja kati ya maswali haya lina maana kubwa kwa
hitimisho na suluhisho litokanalo na mazungumzo yenyewe. Tunachelea
kusema kwamba, haya yanayofanyika baina ya Ofisi za Waziri Mkuu na
Waziri Kiongozi ni mazungumzo kwa manufaa ya mazungumzo na sio
mazungumzo kwa manufaa ya suluhisho. Na kwayo, fedha za walipa kodi wa
nchi hii zinateketea lakini tatizo la Muungano halitatuliwi, zaidi ya
kulizidisha.
Mheshimiwa Spika,
Turuhusu tupige mfano mmoja wa karibuni, kati ya mingi
iliyokwishatokezea, kuthibitisha khofu yetu kwamba mazungumzo haya
hayatatui tatizo halisi la Muungano. Mfano huu unakhusu Ripoti ya
Baraza la Mapinduzi la Zanzibar ya 2003.
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 29 Mei 2003, Ikulu ya Zanzibar ilichapisha Ripoti ya Baraza la
Mapinduzi juu ya Matatizo na Kero za Muungano na Taratibu za
Kuziondoa, ambapo katika sura yake ya tatu, ripoti hiyo ilitoa orodha
ya mambo yanayopaswa kuondolewa katika Muungano. Mambo hayo ni:
Mafuta na Gesi Asilia
Elimu ya Juu
Posta
Simu (Mawasiliano)
Biashara ya Nje
Kodi ya Mapato
Ushuru wa Bidhaa
Usafiri wa Anga
Takwimu
Utafiti
Ushirikiano wa Kimataifa
Leseni za Viwanda
Polisi
Usalama
Mheshimiwa Spika,
Katika kuhakikisha kuwa haya yanatekelezeka, SMZ ilitaka kuwepo kwa
misingi mitano ya kuzingatiwa, ambayo ni:
Masuala ya Muungano yalindwe kwa misingi ya Katiba na Sheria badala ya
siasa na maelewano
Muungano uwe na maeneo machache yanayoweza kusimamiwa na kutekelezwa
kwa urahisi
Muungano uanishe washirika wake wakuu, mipaka na haki zao
Muungano utowe fursa sawa za kiuchumi kwa pande zote mbili za Muungano
Lazima pawe na Muungano unaoweza kuhimili mabadiliko ya kisiasa na
kiuchumi
Mheshimiwa Spika,
Hivi ndivyo SMZ ilivyosema tangu mwaka 2003; na kwa hakika – angalau
katika hili – serikali hii imesema vile ambavyo Wazanzibari wamekuwa
wakisema tangu siku za mwanzo za Muungano huu. Ni wazi kuwa ripoti hii
ya SMZ iko mezani kwa Ofisi zote mbili, ya Waziri Mkuu na Waziri
Kiongozi. Lakini kinachotokezea kila baada ya kikao cha watendaji
wakuu wa serikali mbili, ni taarifa ya kuhuzunisha panapohusika kile
hasa kinachohitajika kutatuliwa.
.
.
Mheshimiwa Spika,
Kambi yetu inaitupia lawama za moja kwa moja serikali ya Muungano
kwamba imejiundia siasa zake maalum kuelekea suala la Muungano huu.
Siasa hizo zinasomeka katika nukta mbili: moja ni kupuuzia maoni
yoyote yanayotolewa na watu kuhusiana na Muungano wenyewe na ya pili
ni kuudharau uhalisia wa Muungano wenyewe.
3.1 Kupuuzia Maoni Yanayohusu Muungano
Mheshimiwa Spika,
Nilitagulia kusema kwamba, panapohusika suala la Muungano, Watanzania
tuna bahati mbaya ya kuwa na serikali yenye utamaduni wa kujifungia
kwenye viambaza vyake vinne, ikajisemesha yenyewe, ikijisikiliza
yenyewe na kisha ikatoka na mwangwi wa sauti yake yenyewe kwenda
kuufanyia kazi. Bila ya shaka, haya hayakuanza leo, bali ni muakisiko
na muendelezo wa utamaduni huo mkongwe; kwamba kila kinachosemwa na
Watanzania wengine wowote ambao hawamo kwenye "Super Structure" ya
Muungano, ni kelele za mlango ambazo hazimzuii mwenye nyumba kulala.
Kitabu cha bajeti iliyopo mbele yetu sasa ni shahidi wa hayo.
…
Riziki O. Juma (Mb)
Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni (Muungano)
--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
0 comments:
Post a Comment