HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR MHE. MAALIM SEIF SHARIF
HAMAD KATIKA UZINDUZI WA KONGAMANO LA MUUNGANO NA MCHAKATO WA
MABADILIKO YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA MWAKA 1977
KATIKA UKUMBI WA EACROTANAL, TAREHE 13 JUNI, 201
Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Kituo cha Huduma za
Sheria Zanzibar na watendaji mliohudhuria
Mheshimiwa Mwakilishi wa Ford Foundation Ofisi ya Afrika Mashariki
Waheshimiwa Viongozi wa Taasisi mbali mbali za Serikali na za Kiraia
Waheshimiwa Wageni wote waalikwa nyote Mabibi na Mabwana
ASSALAM ALEYKUM.
Awali ya yote hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenye
wingi wa rehma kwa kutujaalia afya njema na kutukutanisha hapa, kwa
ajili ya kujadiliana masuala muhimu ya Muungano wa Tanzania na
Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
Mwaka 1977.
Aidha, natoa shukurani zangu za dhati kwa Asasi mbili za Kiraia yaani
Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar na Ford Foundation Ofisi ya
Mashariki mwa Afrika yenye Afisi zake mjini Nairobi, Kenya.
Nakupongezeni kwa mashirikiano yenu na ubunifu wenu wa kutayarisha
mkusanyiko huu ambao umekuja katika wakati muafaka.
Vile vile sina budi kutoa shukurani zangu nyingi kwenu waandalizi wa
Kongamano hili, kwa uamuzi wenu wa kunialika mimi kuja kujumuika
nanyi. Kwangu mimi binafsi hii naona ni heshima kubwa mliyonipa na
ninaithamini sana, nasema Ahsanteni.
Niruhusuni nichukua nafasi hii kuipongeza Afisi ya Ford Foundation
katika Afrika Mashariki kutimiza miaka 50 tokea ilipoanza shughuli
zake katika Afrika Mashariki mwaka 1962. Aidha, naiomba Ford
Foundation yenye Makao Makuu yake huku New York iendelee kushirikiana
na Asasi za kiraia hapa Zanzibar katika sekta mbali mbali.
Tunaishukuru pia Ford Foundation kwa kuisaidia Zanzibar katika maeneo
tofauti kwa mfano Tamasha la Filamu; Idara ya Nyaraka, Makumbusho na
Mambo ya Kale; Tamasha la Nchi za Jahazi; Chama cha Waandishi wa
Habari Zanzibar; na Jumuiya ya Asasi Zisizo za Kiserikali Zanzibar.
Huu ni msaada mzito na wenye maana kubwa kwa nchi yetu. Sisi katika
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunatambua na kuthamini mchango huu
mkubwa kwa nchi yetu.
Kinachodhihirika wazi hapa ni kwamba, malengo ya Asasi mbili hizi
yanafanana au tuseme yanashabihiana, na ndio sababu mukaweza
kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kafanikisha maandalizi ya
Kongamano hili ambalo tunategemea litakuwan na faida na maslahi kwa
nchi yetu na wananchi wake. Nashawishika kusema hayo kwa kuzingatia
ule msemo wa Waingereza usemao "Ndege wa aina moja huruka pamoja"
yaani "Birds of the same feather fly together".Kwa kifupi Madhumuni ya
Asasi hizi ni kusaidia wanyonge, ili nao wapate haki na kudumisha
heshima ya binadamu na Utawala wa Sheria.
Waheshimiwa Waalikwa wa Kongamano
Mada ya Kongamano hili yaani Muungano na Mchakato wa Katiba ya Jamhuri
ya Muungano, ni mada nyeti ambayo inamgusa kila Mtanzania. Kutokana na
ukweli huo, ni matarajio yangu wajumbe wa Kongamano mtatumia ujuzi,
uwezo na uzoefu wenu mkubwa kufanya mjadala ulio hai, usiokuwa na
jazba, ambao hatimaye utazaa mawazo na fikra zitakazosaidia kupata
Katiba iliyo nzuri inayojali maslahi ya Watanzania wote, iwe wa
Tanzania Bara au wa Zanzibar.
Mjadala juu ya Muungano wa Tanzania ni mada kongwe, ambayo wasomi,
wanasiasa, wananchi mbali mbali na hata wageni wamekuwa wakiijadili
mara kwa mara kwa mapana, na kwa mitazamo tafauti tokea Muungano huo
ulipoasisiwa mwaka 1964. Wapo miongoni mwao wanao usifu Muungano wetu
kuwa ni Muungano mzuri na wa mfano kutokana na kudumu kwake. Hao wana
sababu zao, kati ya hizo ni nchi kadhaa za Afrika zilijaribu kuungana
lakini baada ya muda mfupi, nchi hizo zilijikuta katika mizozo na
migogoro hatimaye zilitengana.
Baadhi ya nchi hizo ni pamoja na Ghana na Guinea zilizoungana mwaka
1958, Muungano wa Senegal na Gambia (Senegambia Confederation) wa
Mwaka 1982 hadi 1989, Muungano wa majaribio wa Libya, Tunisia,
Mauritania, Morocco na Algeria (Muungano wa Maghreb) wa mwaka 1956,
Muungano wa Misri na Syria wa Mwaka 1958 (United Arab Republic) ambao
ulivunjika baada ya miaka mitatu hapo mwaka 1961.
Aidha, watu wengi duniani wakiwemo wasomi mashuhuri, wanafalsafa,
wanasiasa waliobobea na wachambuzi wa mambo wanajiuliza kuna siri gani
hata Muungano wa Tanzania uliotokana na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na
Jamhuri ya Tanganyika umedumu kwa muda wa miaka 48 na bado unaendelea.
Maswali mengine yanayouulizwa ni pamoja na kwamba, Jee Muungano huu ni
wa watu wawili? Yaani waliouasisi Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh
Abeid Amani Karume au Muungano huu ni wa watu wote? Jee, Muungano huu
ulikusudiwa uwe wa muda, kutokana na mazingira yaliyokuwepo wakati
huo? Jee, Muungano huo unakidhi sheria za Kimataifa? Jee, Muungano huu
ni wa kisiasa? Kwanini hakuna manung'uniko mengi kuhusu Muungano huu?
Mimi binafsi naamini sina jukumu la kujibu maswali yote hayo. Bali
Watanzania wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano watapata nafasi
ya kutoa mawazo yao mbele ya Tume iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano kwa madhumuni ya kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi
kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Lakini angalau kuhusu hili swali la mwisho linalouliza kwamba kwanini
kuna manung'uniko ndani ya Muungano? Hili liko wazi. Ni kweli kuwa
kumekuwa na manung'uniko mengi na ya muda mrefu juu ya Muungano wetu.
Tume mbali mbali ziliundwa kuangalia malalamiko au kama wengine
wanavyoziita kero za Muungano, na zote zimethibitisha kuwepo kwa
manung'uniko hayo, na hata kupendekeza hatua za kuchukuliwa kutokana
na wakati husika.
Katika uhai wa Muungano huu, wengine wanasema wanabanwa, wanafinywa,
wanaumizwa, wanabebwa, wanajitutumua na wanajitanua.
Miongoni mwa Tume zilizoundwa ni pamoja na Tume ya Mheshimiwa William
Shellukindo juu ya Changamoto za Muungano, Tume ya Jaji Francis
Nyalali kuhusu mfumo wa Vyama vya siasa nchini na Kamati ya Jaji
Robert Kisanga kuhusu White Paper iliyotolewa na Serikali.
Kwa upande wa Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo iliwahi
kuunda Kamati kadhaa kushughulikia kasoro zilizopo katika Muungano.
Kwa mfano, Kamati ya Mheshimiwa Amina Salum Ali mwaka 1992, Kamati ya
Baraza la Mapinduzi kuhusu Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
ya mwaka 1990 na Kamati kuhusu Marekbisho ya Sera ya Mambo ya Nje
mwaka 1999.
Pamoja na Kamati zote hizo na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati hizo,
bado kero za Muungano hazikumalizika. Na badala yake mara nyingi
matokeo ya Tume yalikuwa chachu ya kuibua mijadala mipya juu ya kero
za Muungano.
Waheshimiwa Waalikwa wa Kongamano
Katika zama hizi tulizonazo, ambapo misingi ya demokrasia inapewa
nafasi ya kipekee, hatuna budi kuendelea kuyajadili mambo kama haya
ambayo yanagusa maisha na maslahi ya wananchi walio wengi kwa uwazi
mkubwa. Vyama vya siasa na baadhi ya jumuiya za Kiraia nchini
zimekuwa mstari wa mbele katika kujadili suala la Muungano kwa dhamira
moja tu ya kuwa na mfumo au utaratibu utakaoleta haki na kuondoa
malalamiko yaliyopo.
Wapo wanaosema dawa ya matatizo haya ya Muungano ni kuwa na serikali
moja tu, wapo wanaosema tuendelee kuwa na serikali mbili huku
tukitatua kero zinazojitokeza, wapo wanaosema tuwe na serikali tatu.
Na nyote ni mashahidi, wapo wanaokuja na mawazo na fikra kwamba
Muungano huu tuuvunje kabisa. Au kama wengine wanavyosema 'tugawane
mbao'.
Aidha, hivi sasa kumekuwa na mtazamo mpya ambao ni kufanya marekebisho
ya Muundo wa Muungano, ili kuwe na Serikali mbili ambazo ni Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar yenye uhuru na mamlaka kamili ya kujiamulia
mambo yake, na Serikali ya Tanganyika yenye uhuru na mamlaka kamili ya
kujiamulia mambo yake. Kisha Muungano utakaoanzishwa kwa njia ya
mkataba, kwa mambo ambayo nchi mbili hizi watakayo kubaliana.
Wenye mawazo ya mfumo huu wanaamini kuwa huo ndio mwarubaini wa
matatizo ya Muungano yanayodumu muda mrefu na ambayo yanaendelea
kujitokeza. Mfumo wa Muungano wa mkataba si jambo geni na umekuwa
maarufu sana hivi sasa Duniani. Hata Jumuiya ya Afrika Mashariki na
Umoja wa Ulaya (European Union) ni mfumo wa aina hii ya Muungano.
Chini ya utaratibu huu kila serikali inakuwa na mamlaka kamili, lakini
katika baadhi ya mambo wanayokubaliana yawe ya pamoja nchi husika
zinafungana mikataba ya kuyaendesha na kuyasimamia.
Naamini kwa Wazanzibari lililo muhimu zaidi ni Muungano, na si haki
kuwazuia Wazanzibari wasitoe maoni yao juu ya Muungano. Na kwa maana
hiyo kwetu lililo muhimu zaidi ni hili la Muungano.
Waheshimiwa Waalikwa wenzangu
Mimi ni mmoja miongoni mwa viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar na pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Siasa cha CUF. Lakini pia
mimi ni Mzanzibari na Mtanzania. Kwa hiyo nitakuwa na haki ya kutoa
maoni yangu wakati ukifika. Tuombe Mwenyezi Mungu atujaalie uhai.
Hata hivyo, nachukua nafasi hii kuendelea kuwahimiza na kuwashauri
Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kuzisoma Hati mbali mbali za
Muungano, Katiba za Tanganyika, Katiba za Tanzania na Katiba za
Zanzibar na maandiko mbali mbali ya wasomi katika vitabu au magazeti.
Wakati utakapofika Tume ya Katiba itakapokuja wananchi waweze
kuchangia huku wakiwa wanajua kwa undani Muungano wetu, ikiwemo faida
na kasoro zake na waseme bila ya woga wanachokitaka.
Hii ni fursa adhimu ambayo wengi wamekuwa wakiililia kwa siku nyingi
juu ya haja ya Watanzania kupata fursa ya kutoa maoni yetu, juu ya
masuala yote yanayohusiana na Muungano.
Wananchi wawe huru kutoa maoni yao kwa uwazi na pawepo na uvumilivu.
Hata kama mtu hakubaliani na maoni, hoja zinazotolewa na mwengine,
inabidi asikilize kwa uvumilivu. Naye akipata fursa aseme yake kwa
uwazi pia.
Waheshimiwa Waalikwa wenzangu
Naomba kutoka nasaha zangu kwamba katika mchakato wa kukusanya maoni
ya wananchi juu ya mabadiliko ya katiba, ni vizuri sote tukatumia
busara ya hali ya juu, hekima na uvumilivu, ili mchakato uende kwa
salama. Tukumbuke kuwa vurugu na misuguano ya aina yoyote haina faida
na isipewe nafasi katika kutoa maoni yetu kuhusu mchakato wa
mabadiliko ya katiba.
Na mwisho wa yote hayo, ni lazima tukubaliane kwamba maoni ya wengi
yaheshimiwe baada ya wale wachache kupewa haki yao ya kusikilizwa kwa
kikamilifu. Naomba kuchukua nafasi hii kuwatoa wasi wasi wananchi na
hasa Wazanzibari. Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi wametokana na
Wazanzibari wenyewe. Viongozi hao ni Wazanzibari kindaki ndaki, wenye
kujawa na kiwango kikubwa cha uzalendo. Wanaipenda Zanzibar kama
Mzanzibari mwengine yoyote yule.
Viongozi wapo kulinda maslahi ya Zanzibar na watu wake, kama vile
viongozi wa Tanganyika walipo kulinda maslahi ya wananchi wenzao wa
Tanganyika. Kwamwe viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hawata
wasaliti wananchi wa Zanzibar.
Tutaheshimu na kutetea maoni yenu wananchi kama mlivyo yatoa kwa Tume
ya Jaji Warioba. Muhimu jitokezeni kwa wingi mtoe maoni yenu. Maoni ya
wengi naamini yataheshimiwa. Naomba nitahadharishe watu wasijefanya
kosa la kuto kwenda kutoa maoni yao. Kama mtu hakwenda anaweza kuja
kujilaumu, pale ambapo maoni ambayo yeye hayaungi mkono yakaja kuwa
ndio maoni ya wengi, kwa sabababu tu yeye na wenziwe wenye maoni kama
yake hawakujitokeza kutoa maoni yao.
Baada ya kusema hayo machache nachukua nafasi hii kukushukuruni nyote
kwa kunisikiliza kwa makini na sasa natamka kwamba kongamano la
Muungano na Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba limefunguliwa rasmi.
Ahsanteni.
--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
0 comments:
Post a Comment