Thursday, 5 July 2012

[wanabidii] UJUMBE WA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI KWA WATANZANIA WOTE WENYE MAPENZI MEMA

UJUMBE WA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA KWA WAAMINI WAKATOLIKI
NA WATU WOTE WENYE MAPENZI MEMA
30-06-2012

SISI Maaskofu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tumekutana
katika mkutano wetu Mkuu wa 65 wa kawaida tangu tarehe 23/06/2012 hadi
30/06/2012 Uliowajumuisha Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na wakuu wa
Idara ,Tume na Taasisi za Baraza Pamoja na Wawakilishi Walei.

Lengo la Mkutano huu likiwa kutathimini shughuli za kazi zetu za
Kichungaji na za huduma za Jamii kwa Kipindi cha miaka Mitatu
iliyopita 2009-2012 na vilevile kupanga mikakati ya kuboresha shughuli
hizo za Kichungaji na za Huduma za Jamii katika Nyanja za Afya, Elimu,
Misaada kwa wasiojiweza utetezi na ushawishi kwa kipindi cha miaka
Mitatu ijayo 2012-2015.

Pamoja na kufanya tathimini ya kina ya utendaji wa Baraza letu katika
kipindi hicho kilichopita. Na kupanga mipango kabambe kwa ajili ya
utendaji wa Baraza kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo Mkutano wetu
Mkuu umekuwa na Fursa ya kujadiliana na kushirikishana baadhi ya
matukio/mambo ambayo kwa hakika yametikisa jamii yetu ya Watanzania
na kuidhalilisha nchi mbele ya Jumuiya ya Kimataifa.

Kwa namna ya pekee kabisa tumetafakari juu ya vurugu za kidini hivi
karibuni zilizotokea Visiwa vya Zanzibar kuanzia tarehe 26-28 Mei 2012
na kupelekea kuchomwa moto kwa baadhi ya Makanisa Visiwani humo
pamoja na uharibifu wa mali na uvunjifu wa amani.

Bila kupenda kurudia matamko ya wadau mbalimbali wakiyatoa katika
nyakati tofauti kulaani bila kusita hali hiyo iliyojitokeza Visiwani
Humo ,Tunaunga mkono kwa nguvu zote kauli na jitihada za wale wote
wenye mapenzi mema walioguswa na vitendo hivyo na hivyo
kulaani.Tunatoa pole na kueleza mshikamano wetu wa kindugu kwa wale
wote walioathirika kwa namna moja au nyingine kwa vitendo hivyo vya
vurugu ambavyo vimefanya sehemu ya jamii ya wakazi wa visiwani humo
hasa Wakristo kuhishi kwa wasiwasi mkubwa kutokana na vitisho
vinavyoendelea kutolewa na baadhi ya vikundi pamoja na hali ya
kutopewa ulinzi wa kutosha na vyombo husika.Tunaendelea kuwaahidi sala
na mshikamano wetu katika kipindi hiki kigumu.

Pamoja na hayo tunapenda kuwakumbusha Watanzania wenzetu hasa wa
Mamlaka husika kutafakari na kuzingatia busara za Wahenga waliosema
kwamba mwanzo wa makubwa ni madogo na kwamba mdharau mwiba mguu huota
tende kumbukumbu zinatuambia kwamba chuki za wazi za kidini zilianza
kuinyemelea nchi tangu miaka ya 1990 pale mihadhara ya kashfa ya
kidini ilipoanza kuruhusiwa. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa
kuongozwa na busara ya kichungaji kwa nyakati tofauti liliandika barua
kuziomba na kuzihimiza Mamlaka husika kuingilia kati na kuhakikisha
kwamba mihadhara kama hiyo haipati nafasi kuendelea katika nchi yetu
kwani kamwe haiwezi kuwa na tija ispokuwa kuamsha hisia kali za
kidini, jazba na kujenga chuki miongoni mwa waamini wa dini tofauti,
kwa bahati mbaya ushauri huo wa Braza la Maaskofu ulipuuzwa na
Mamlaka husika .

Hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la vyombo vya Habari ambavyo
vimeanzishwa na ambavyo badala ya kuzingia malengo mazuri ya vyombo
vya Habari kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha vimeonyesha malengo
ya wazi ya kueneza uzushi, kashfa, chuki na uchochezi. Bado kuna CD,
DVD na kanda chungu nzima zinazagaa mitaani zenye mambo kama hayo
ambapo kwa mshangao mkubwa wa raia wema licha ya wahusika kufahamika
na kuonekana waziwazi hakuna hatua za kisheria zilizochukuliwa dhidi
yao.

Tunachelea hata kudhani kwamba Mamlaka za Dola zinawakingia kifua
wadau wa harakati hizo. Mkusanyiko wa mambo yote haya ndiyo
uliotufikisha hapa tulipo. Kwa upendo tulionao kwa nchi yetu na kwa
kuzingatia historia ya mlolongo wa matukio yaliyotufikisha hapa
tulipo, tuna hofu,l akini kwa uwazi tunapenda kuwaambia mamlaka husika
watu wote wenye mapenzi mema na Watanzania wote kwa ujumla kwamba,
iwapo hatua mathubuti hazitachukuliwa mara moja ili kurekebisha hali
hii baada ya miaka michache, hakika kwamba nchi yetu inaweza kuingia
katika machafuko ya kidini.

Ili kuepuka hali hii isitokee kwa moyo wa unyenyekevu kabisa,
tunapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe: Sisi Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania tutaendelea kusali kuiombea nchi yetu Amani licha
ya Sala na maombi ya kawaida kwa ajili ya lengo hilo, Mkutano Mkuu
umeamua kwamba tutakuwa na siku moja ya kusali kitaifa ya kuomba
Amani, Tutaendelea kutumia sauti yetu ya kinabii kuonya kukemea
kukaripia vitendo vyote vile vinavyoashiria kueneza chuki miongoni mwa
watu wa dini mbalimbali kwa kutumia tume na Idara zetu.

Tutaendelea kujenga na kueneza mazungumzo na waamini wa dini
mbalimbali tukiheshimu tofauti zilizopo hii ni kwa sababu tunaaamini
kwamba suala la dini ni wito na hiari ya mtu na hakuna mtu yeyote
aliye na haki ya kumlazimisha mwingine ajiunge na dini nyingine. Kwa
upande wa wadau wengine na hasa kwa Serikali yetu pamoja na vyombo
vyake vya usalama tunapendekeza yafuatayo:

Mihadhara, Makongamano na Mikutano yenye lengo la kutoa kashfa na
kuchochea chuki miongoni mwa dini mbalimbali ipigwe marufuku, vyombo
vya habari vinavyoeneza uzushi, kashfa na uchochezi vizibitiwe kwa
kuchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungiwa, uzushi na
uongo unaoenezwa na vyombo vya habari na watu wenye lengo la
kuwachonganisha Watanzania na waamini wa dini mbalimbali utolewe
ufafanuzi mara moja na Wizara na vyombo vingine vinavyohusika, kuweko
mpango kabambe wa kutoa Elimu ya Uraia yenye kina na upana katika
nafasi zote itakayowawezesha vijana wetu kuwa wazalendo wa nchi yao na
kuepuka propaganda za kuwagawa Watanzania kwa misingi ya Dini.

Suala la ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana liangaliwe kwa
umakini kwani linaweza kuwa moja ya sababu zinazowafanya vijana wengi
kujiingiza katika vikundi vya kidini vinavyojenga chuki na kutoa
matumaini ya uongo lakini zaidi ya yote iwapo Serikali yetu na
Mamllaka husika inataka kuwa na imani mbele ya jamii kwamba ina nia
thabiti ya kuhakikisha kwamba vurugu za kidini hazipati nafasi katika
nchi yetu wale wote waliohusika na vurugu hizo wachukuliwe hatua za
kisheria mara moja! Ni vigumu kuamini kwamba katika kipindi cha kuanzi
mwaka 2001 mpaka sasa Makanisa Ishirini na Tano yamekwisha kuchomwa
moto kisiwani Zanzibar lakini hakuna aliyekamtwa na kuchukuliwa hatua
za kisheria!

Tumefanya mkutano wetu katika mazingira ya kuwepo mvutano kati ya
Madakitari na Serikali na kwa bahati mbaya sana, kama tulivyokwisha
kutamka huko nyuma mvutano huo utaleta athari kubwa kwa Raia wasio na
hatia, athari ambazo haziwezi kurudishwa. Uhai wa raia wa Tanzania
unaaangamia kwa kukosa ulinzi wa tiba katika hali hii tunapenda
kukumbusha kuwa kila mmoja ni mdau. Hakuna hata mmoja anayeweza
kulikwepa hili tunapenda kurudia himizo letu la awali kwamba ipatikane
njia nyingine iliyomwafaka zaidi ya kudai haki na mazingira yanayofaa
ya kazi bila ya kuleta madhara ya kupoteza uhai ambayo ni haki ya
msingi ya kila mwanadamu.

Tunaisii Serikali yetu ikae tena na Madaktari na kuchambua hoja
zitakazowekwa mbele yao. Uwazi na ukweli vikitawala hakuna pande
itakayokataa kuridhia eti kwa sababu ya kukataa tu bila hoja. Taifa
letu limejipatia aibu mbele ya macho ya Ulimwengu ya jinsi
tunavyoshindwa kuhishi kile tunachosema katika majukwaa.

Mwisho tunaendelea kuwaalika Watanzania wenzetu hasa viongozi wa Dini
mbalimbali kuwahamasisha waamini wawe raia wema wa nchi hii kwa
kuungana pamoja kuhamasisha upendo, haki, amani na maridhiano miongoni
mwa Watanzania wote.

Licha ya tofauti zetu tuzingatie hasa yale yanayotuunganisha,
ubinadamu wetu na uraia wetu wa nchi yetu tukufu ya Tanzania ambamo
tutake tusitake ni lazima wote tuhishi tuepuke ushindani ambao hauna
tija isipokuwa kutupeleka katika chuki na hali ya kuzaniana vibaya
miongoni mwa waamini wetu. Iwapo kuna sababu ya kushindana, tushindane
katika mbinu za kujenga upendo na amani miongoni mwa Watanzania katika
kutafuata njia za kuwaletea maendeleo yatakayowatoa katika umaskini,
ujinga na maradhi ambavyo ni adui wetu sote. Tunaiombea nchi yetu
amani na usalama.

MWISHO

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment