Tuesday, 19 June 2012

[wanabidii] Wazanzibari wataka uwiano katika Muungano

WAJUMBE wa baraza la wawakilishi wametaka uwiano sawa katika nafasi za
juu za Muungano izingatiwe uteuzi wa wazanzibari ili kutoa haki sawa
kwa pande zote mbili. Baadhi ya wajumbe wa baraza la wawakilishi
wametoa kauli hiyo katika kipindi cha masuali na majibu ambapo
walihoji kwa nini nafasi za majeshi na polisi zinashikiliwa na watu
kutoka upande mmoja wa muungano peke yake.

Mwakilishi wa Jimbo la Wawi (CUF) Salim Nassor Juma alisema kutokuwepo
na uwiano katiak kushika nafasi za uongozi na nafasi nyeti katika
utumishi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania ni kero na inahitaji
kushughulikiwa.

Aidha Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub na
Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe (CUF) Salim Abdallah Hamad walitaka
nafasi ya mkuu wa jeshi la polisi na nafasi ya mkuu wa majeshi ya
ul;inzi na usalama ishikwe na wazanzibari.

Akijibu hoja hizo za wajumbe Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa pili wa
rais, Mohammed Aboud Mohammed alisema kwa mujibu wa katiba rais wa
jamhuri ya muungano wa Tanzania ndio mwenye mamlaka ya uteuzi huo na
halazimiki kufuata ushauri wa mtu yeyote.

"Hata hivyo marekabisho ya sasa ya katiba ambayo yataanza hivi
karibuni ni pahala pazuri pa kuwasilisha malalamiko na kutoa
mapendekezo juu ya mamlaka ya rais, toweni malalamiko yenu kwa tume na
ninakunasihini mfanye hivyo" alisema Aboud.

Aboud alisema katika uteuzi wa nafasi zote za juu katiba haikuweka
vigezo, uwiano wala fomula maalumu katika uteuzi na ni mamlaka
aliyonayo mheshimiwa rais ambaye ni pia jemedari mkuu wa majeshi ya
ulinzi na usalama.

Kutokana na kuwepo na hali hiyo Aboud alisema ni wakati mwafaka kwa
wananchi pamoja na wajumbe wa baraza la wawakilishi kutoa maoni yao
kwa tume ya kuratibu maoni ya katiba mpya inayoanza kazi yake hivi
karibuni.

Viongozi wagoma kuhama nyumba za serikali

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema inakabiliwa na upungufu wa
nyumba za kuishi viongozi wa kitaifa kutokana na tabia ya baadhi ya
viongozi hao kutotaka kuhama wanapomaliza muda wao wa uongozi.

Naibu Waziri wa wizara ya maji Ardhi, Makaazi na Nishati, Muhidin
Makame alisema kuwa kwa miaka mingi serikali ilikuwa na nyumba zake za
kuishi kiwemo viongozi wa kitaifa lakini matatizo yaliojitokeza ni
baadhi ya viongozi hao kuwa na tabia ya kutohama katika nyumba za
serikali baada ya muda wao wa uongozi kumalizika.

Hayo ameyaeleza Naibu waziri huyo wakati akijibu suali la msingi la
Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua
mipango ya serikali katika kuwapatia viongozi nyumba za kuishi na
kuepuka gharama za kukodi.

Alisema jambo jengine ambalo limesababisha serikali kuwa na nyumba
pungufu ni uchakavu wa nyumba hizo kutokana na kutokuzifanyia
matengenezo kwa muda mrefu.
"Hivi sasa serikali inaandaa mpango maalumu wa kuzifanyia matengenezo
nyumba zote za viongozi ambazo zipo katika hali nzuri na pia kuzivunja
kwa zile amabzo zipo katika hali mbaya ili kutoa nafasi kwa ujenzi wa
nyumba mpya" aliahidi naibu huyo.

Aidha naibu waziri huyo aliwataka viongozi wanaomaliza muda wao
kuzihama nyumba za serikali ili kuwapisha wengine ili kuondokana na
upungufu wa nyumba na kutoa nafasi kwa viongozi wengine wanaoteuliwa
nafasi hizo.

Baadhi ya nyumba za serikali ambazo zinakabiliwa na uchakavu mkubwa ni
nyengine kuwa katika hatari ya kuanguka zipo katika maeneo ya
mazizini, migombani na chakechake kisiwani Pemba.

Zanzibar kutengeneza bendera nyingi zaidi

WAZIRI wa Katiba na Sheria Zanzibar, Abubakar Khamis Bakari amesema
jana kuwa serikali inakusudia kutengeneza bendera za kutosha za
Zanzibar ili kuondoa upungufu na kuwawezesha wananchi kuzitumia.

Akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae (CCM) Mohammed Said
Mohammed ambaye alitaka kujua kama matumizi ya bendera ni kosa
kisheria.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu
alihoji upungufu wa bendera za Zanzibar katika visiwa vya Unguja na
Pemba ikilinganisha na bendera za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akijibu masuali hayo Bakari alisema sio kosa kisheria kwa wananchi
kutumia bendera ya nchi yao katika shughuli mbali mbali ikiwemo
kupachika katika baiskeli au gari au kutumia kwa matumizi ya sheria za
nchi na sherehe nyenginezo.

"Serikali haimzuwiii mwananchi kutembea na bendera ndogo ya Tanzania
wala ya Zanzibar kama ataiweka ndani ya gari yake au vyombo vya
maringi mawili, hii ni fakhari kuona wananchi wanaipenda nchi yao"
alisema Waziri huyo.

Waziri Bakari alisema matumizi ya bendera yanafanana katika mahala
mingi duniani hasa pale ambapo wananchi wanasherehekea kitu Fulani
kama vile mpira, siku ya kitaifa na kadhalika kwa sababu hakuna tatizo
lolote la kisheria.

"Kama kuna upungufu wa bendera nitashirikiana na taasisi inayohusika
tuweze kutengeneza bendera za kutosha ili wananchi waweze kuzipata na
kuzitumia" alisema.

Hata hivyo katika majibu ya ziada Naibu Waziri wa Mawasiliano na
Miundombinu Issa Haji Gavu alisema kwa hivi sasa zipo bendera za
kutosha na kuwataka wananchi wende wakazinunue ambapo bendera moja
inauzwa kwa bei ya shilingi 40,000.

Zanzibar ilipitisha sheria ya kuwa na bendera yake mwaka 2005 ikiwa
sehemu ya kielelezo cha utaifa baada ya bendera hiyo kutokuwepo
kufuatia Zanzibar kujiunga na Tanganyika mwaka 1964.

Chalezo kipya kujengwa Zanzibar

ZANZIBAR inakusudia kujenga chelezo ambapo meli na boti za kijeshi
zitatengenezwa ili kuondoa mchanganyiko wa vifaa vya kijeshi na sehemu
za raia.

Hayo yameelezwa katika kikao cha baraza la wawkailishi kianchoendelea
na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini wakati
akijibu suali la msingi la Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani (CCM) Ali
Salum Haji aliyetaka kujua kwa nini kikosi cha KMKM kimeshindwa
kufufua chelezo chake hapa Zanzibar.

Waziri alisema hivi sasa serikali imo katika mipango ya kuangalia
gharama za kufufua chelezo cha KMKM ambacho ni kikosi maalumu cha maji
ya Zanzibar.

"Chelezo cha KMKM kilichindwa kufanya kazi tangu miaka ya 1970 lakini
hivi sasa kwa msaada wa jamhuri ya kidemokrasia ya ujerumani tuna
mpango wa kufufua chekelezo hicho" alisema waziri Makame.

Alisema kampuni ya Damen Shipyard kutoka Uholanzi imo katika kufanya
upembuzi yakinifu na kuangalia gharama halisi ili kazi iweze kufanyika
na kwamba jeshi kuwa na chelezo chake ni muhimu.

Waziri huyo aliwaambia wajumbe wa baraza hilo kwamba kikosi cha KMKM
kutumia chelezo chake kwa ajili ya matengenezo ya boti zake na hasa
ikizingatia kanuni za kiusalama.

Kikosi cha kuzuwia magendo (KMKM) ni miongoni mwa vikosi vitano vya
serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ambavyo vina majukumu mbali mbali
ikiwemo ulinzi na usalama nchini.

Vikosi vyengine ni Valantia, Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Magereza,
Kokosi cha Uokozi na Zima moto (KUZ) ambavyo voye vinatambulika
kisheria.

Utafiti wa madini joto ni muhimu

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema itaendelea kusimamia na kufanya
uchunguzi wa viwango vya madili joto katika chumvi inayozalishwa na
kutumika zanzibar ili kuepuka madhara ya kukosekana kwa madini hayo
mwilini.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri hiyo, Dk Sira Ubwa Mamboya wakati
akijibu suali la msingi lililoulizwa na Mwakilishi wa Wawi (CUF) Saleh
Nassor Juma aliyetaka kujua nafasi ya wataalamu wa afya katika
kushauri matumizi ya madini joto katika chumvi hasa kwa uzalishaji
unaoendelea kisiwani Pemba.

Waziri alisema wataalamu wa wizara yake kitengo cha lishe kwa
kushirikiana na shirika la kimataifa la Unicef wametoa mafunzo kwa
vikundi vya uzalishaji chumvi ili kuzingatia uchanganyaji wa chumvi na
madini joto.

Alisema wizara yake imetoa mafunzo kwa maafisa wa afya kusimamia
viwango vya madini katika chumvi inayouzwa kwa ajili ya matumizi ya
wananchi.

"wizara ya afya kupitia bodi ya chakula, dawa na vipodozi itaendelea
kusimamia na kufanya uchunguzi wa viwango vya chumvi ili wananchi
watumie chumvi inayotakiwa" alisema Dk Sira.

Aidha Naibu waziri huyo amesema wameshirikiana na jumuiya ya
wazalishaji chumvi kisiwani Pemba (Association of Zanzibar Salt
Prcessing Organisation – AZASPO) ili kuwanunulia madini joto na
kuwakabidhi wao kama ni wadhamini na wasimamizi wa vikundi vyote vya
uzalishaji chumvi.

"Lengo la kufanya hivyo wao AZASPO walitakiwa wawauzie wazalishaji na
pesa wanazokusanya waziendeleze kwa kununulia madini joto ikiwa ni
fedha za kimzunguko (revolving fund)" alisema naibu huyo.

Kwa mujibu wa wizara ya afya, ukosefu wa madini joto unasababisha
matatizo mbali mbali ya kiafya ikiwemo kutoimarika kwa mifupa mwilini
na maradhi ya uvimbe shingoni (goiter).

Zaidi ya bilioni 1.5 zatolewa kwa vikundi

ZAIDI ya shilingi bilioni 1.5 zimetolewa kwa vikundi vya ujasiriamali
Zanzibar hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu kupitia mfuko wa rais
Kikwete na Rais Karume.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Kiuchumi na Ushirika,
Haroun Ali Suleiman wakati akijibu suali la msingi la Mwakilishi wa
nafasi za wanawake, Mwanaidi Kassim Mussa ambaye alitaka kujua ni
wananchi wangapi walinufaika na mfuko huo kwa upande wa Zanzibar.

Waziri alisema jumla ya mikopo 750 ilitolewa ikiwemo watu binafsi,
vikundi vya wajasiriamali, saccos na vikundi vya kiuchumi ambapo
sehemu ya fedha hizo tayari zimesharejeshwa.

"Fedha zilizorejeshwa ni zaidi ya milioni 765,000 hadi kufikia Aprili
mwaka huu ambapo ni sawa na asilimia 50. Jumla ya wanawake 170 katika
mkoa wa mjini magharibi wamepata mkopo huo kati ya wanawake 276
waliopewa mkopo kwa Zanzibar nzima" alisema waziri huyo.

Waziri Suleiman aliwaeleza wajumbe wa baraza hilo kwamba waazilishi wa
mfuko huo ambao ni marais wa Tanzania na Zanzibar, maarufu mfuko wa JK
na AK wanadhamira ya kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuwaendeleza
wananchi wenye kipato cha chini ili kupunguza umasikini nchini.

Mfuko wa JK na AK ambao umeanzishwa mwaka 2005 kwa lengo la kupunguza
umasikini na ukosefu wa ajira nchini unaowanufaisha zaidi ni makundi
ya akina mama kupitia miradi yao mbali mbali.

http://zanzibaryetu.wordpress.com/2012/06/18/wawakilishi-wataka-uwiano-katika-muungano/#more-10376

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment