Watawala wanapojivunia kula pweza gizani!
Na Mashaka Mgeta
SIKU moja nikiwa kisiwani Unguja, niliwahi kutembelea Mjini Magharibi, nikapita karibu na ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), tawi la Mtoni.
Ni jengo kubwa, lenye ukumbi mkubwa na ofisi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiofisi. Linakifaa chama hicho kilicho miongoni mwa vyama tawala duniani.
Katika udadisi wangu, mmoja wa wenyeji niliokuwa nao akanisimulia hekaya tofauti zinazozungumzwa kuhusu osifi hiyo, lakini zote zikionyesha ukosefu wa umakini kwa viongozi wa chama hicho.
Sitaki kuzitaja hekaya hizo kwa maana ni fedheha kubwa kwa watawala, na kwa vile sikuwahi kuwahoji ili wanieleze uhalisia wake, ninaawachia CCM na jingo lao katika tawi la Mtoni huko Zanzibar.
Hata hivyo, mtoa taarifa wangu akiwa katika kuelezea masikito yake jinsi udhaifu kadhaa uliopo katika hekaya ya jengo, alisema "tatizo la chama chetu (CCM), watu wanafanya mambo yao bila hofu, utadhani wanakula pweza gizani." Pweza ni aina ya viumbe wanaopatikana baharini, akiwa na umbile lenye miguu mingi, lakini zaidi analiwa na wakazi wa pwani ya bahari, kwa nyama na supu yake. Ni mtamu sana.
Nikashawishika kuhoji, ina maana gani kusema "CCM wanafanya mambo bila hofu utadhani wanakula pweza gizani?" Mtoa taarifa wangu akasema, pweza ni aina ya samaki asiyekuwa na mifupa kama walivyo wengine.
Hivyo ulaji wake hausababishi hofu kwa mlaji hata akiwa anamtumia kwenye eneo lililo na giza totoro, ataendelea kula kwa 'raha zake, kwa maana hana hofu ya kukutana na mwiba unaoweza kuwa kikwazo kwake. Kwa mfano huo, mtoa taarifa anasema mambo yanayofanywa na CCM ni kama mlaji pweza gizani! Hana hofu, hana wasiwasi, anajiamini. Hivi karibuni, umma umeshuhudia mjadala mkubwa bungeni kuhusu bajeti ya mwaka 2012/2013, ikiwasilishwa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa.
Wapo wabunge walioisifia, ingalikuwa heri wakapata nafasi pana, basi wangeinyanyua juu, wakazunguka nayo kwenye ukumbi wa Bunge huku wakiimba nyimbo za masifu na mapambio ya kila aina. Wakisema ni bajeti safi, tena safi sana.
Wapo walioikosoa, wakibainisha maeneo mengi yenye kasoro na kama ingewastahili kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, wangeweza kuidurufu, waisambaze ndani na nje ya ukumbu wa Bunge ili kila anayefika kwenye eneo hilo, aisigine.
Yote mawili hayakuwezekana, kwa maana ni kinyume cha Kanuni za Bunge. Hivyo njia pekee ilikuwa ni kujenga hoja.
Ukiondoa maneno yanayochapishwa kwenye karatasi yakiwa ni majina ya vyama vya siasa walivyopitia wabunge kupata wadhifa huo, wote ni wawakilishi wa wananchi. Wananchi walio wanachama na wasiokuwa wanachama wa vyama vya siasa. Katika hali ya kustaajabisha, wapo wabunge wamekaririwa na vyombo vya habari, ndani na nje ya Bunge, wakijiweka kando kabisa na maslahi ya umma. Wanawakejeli wenye kuikosoa bajeti hiyo.
Kwa kufanya hivyo, wabunge wanaowakejeli, wengi wao wakiwa kupitia chama tawala, wakafanya hivyo huku wakitambua kwamba wabunge wakosoaji si raia wa Rwanda, Uganda, Tunisia, Misri, Afghanstan, Marekani ama kwingineko duniani. Ni raia halali wa Tanzania.
Hivyo ukosoaji wao hauwezi kutafsiriwa kwa namna yoyote kama usiokuwa na nia njema kwa nchi na watu wake. Wanafanya hivyo ili kuchagiza kasi ya uboreshaji wa huduma za jamii kupitia bajeti 'iliyotulia'
Kufanya hivyo kunaonekana kuwa dhambi mbele ya watawala. Wanawakejeli wabunge wenye nia na mapenzi mema. Wengine wameripotiwa kufikia hatua ya kupendekeza kufukuzwa uanachama kwa wabunge wa CCM walioipinga bajeti.
Kuna neno moja Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipenda kulitumia akimaanisha viongozi wa umma wanaofanya mambo ya hovyo. Akawaita wendawazimu. Ninashindwa kuamini kwamba watawala wakiwemo wabunge kupitia CCM, wanapata wapi ujasiri wa kujiweka mbali na umma, huku wakijigamba kuwa na uhakika wa kuliongoza taifa hili?
Watawala kupitia CCM wanashindwa vipi kutambua kwamba ubovu wa huduma za jamii kama miundombinu, afya, elimu, maji haviwaathiri watu kwa misingi ya itikadi, bali kwa ujumla wao wote?
Kwamba kama ni barabara mbovu, walio wa CCM na wasiokuwa katika chama hicho wanaguswa. Kama ni maji machafu yanawaathiri wote, kwa maana maeneo ya jiografia hayawatengi CCM na raia wa kawaida.
Kama ukosefu wa dawa ama tiba ya aina yoyote, kama ni tatizo la wajawazito kujifungulia majumbani kutokana na kutokuwepo zahanati, vituo vya afya ama hospitali, vinawapata wote pasipo kujaliwenye kuendeleza salaam za CCM hoyeeeeee, Peoples' power ama nyingineyo ndani ya vyama vya siasa.
Watawala wanapaswa kutambua kwamba jamii imechoka. Sehemu kubwa ya raia wa taifa hilo wamepigika. Wamesubiri tumaini la kuwa na maisha bora kwa kila Mtanzania, hawalioni. Hawausikii hata upepo wenye sauti za wimbo uliosheheni beti za ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya. Raia wamekuwa wapo kama hawapo. Walio wengi, kila leo inakuwa heri ya jana. Wamekata tama.
Katikati ya hali hiyo, watawala wanatenda pasipo hofu, hawauogopi umma, hawauheshimu umma. Wanakiogopa chama ambacho ni maneno juu ya karatasi, wanakiheshimu chama kuliko watu. Watawala hawapaswi kufikia hatua hiyo. Na kama wapo hapo pasipo kujali ni kwa muda gani, wastuke, waamke waondoke. Wanawaweza kujiamini mithili ya mtu anayekula pweza gizani, lakini asipokuwa makini kujiandaliwa mazingira ya kumiliki chombo kinachotoa nishati ya mwanga, ipo siku pweza hatapatikana.
Kwa mazoea ya kula pweza gizani, anaweza kumpata samaki mwingine kama ningu anayepatikana ziwa Viktoria akiwa na miba mingi. Itamchoma, itamkwama kooni, ikamuathiri ikibidi kumuua.
Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kwenye simu namba +255 754n 691540, 0716635612 ama barua pepe: mgeta2000@yahoo.com. Source: NIPASHE Jumapil June 24, 2012 |
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com Kujiondoa Tuma Email kwenda wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma Disclaimer: Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
0 comments:
Post a Comment