Saturday, 23 June 2012

[wanabidii] TAMKO LA TAASISI ZA KIISLAMU ZANZIBAR KUHUSU KUVUNJWA KWA MUHADHARA DONGE

Ndugu Wana bidii
Hivi hawa watu wanatuita sisi Tanzania Bara "WAKOLONI" jamani,

Hebu nipeni Faida Tano tu za kiuchumi ambazo Tanganyika inapata kwa kuwa na huu muungano

Minafikiri kama hakuna ajenda iliyojificha ya watu flani, basi waachiwe nchi yao. TUWAONE



From: Yona F Maro <oldmoshi@gmail.com>
To: Wanabidii <wanabidii@googlegroups.com>
Sent: Saturday, June 23, 2012 6:16 AM
Subject: [wanabidii] TAMKO LA TAASISI ZA KIISLAMU ZANZIBAR KUHUSU KUVUNJWA KWA MUHADHARA DONGE

BISMILLAH RAHMANI RAHIM

TAMKO LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU ZANZIBAR

Kila sifa njema anastahiki ALLAH (S.W.T), Rehma na Amani zimuendee
Mtume Muhammad (S.A.W), watu wake, Maswahaba zake na walio wema katika
Uislamu.

Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar baada ya kufuatilia kwa hatua
za awali na kufanya tathmini ya hali ya mambo namna ilivyotokea tarehe
17 juni, 2012 inatoa tamko RASMI kama ifuatavyo:

Siku ya tarehe 17 juni, 2012 majira ya saa nane na nusu za mchana
waislam waliondoka viwanja vya malindi eneo la mjini magharibi na
msafara wa gari, vespa na Pikipiki ukielekea kwenye muhadhara
Kaskazini Unguja eneo la Donge sambamba na wenzao wengine waliotoka
mashamba yote ya Unguja kuelekea hukohuko Donge katika Msikiti uliopo
eneo  linalojulikana kwa jina la Donge pwani, tulipofika Mahonda
msikiti wa Ijumaa ambao upo karibu na kituo cha polisi cha mahonda,
majira ya saa tisa na dakika kumi jeshi la polisi lililovalia sare za
askari wa FFU liliwazuia wananchi hao kuendelea na safari yao ya Donge
nakusababisha mkusanyiko usio wa lazima.

Watu waliokuwa katika msafara huo walilazimika waingie msikitini huku
wakisubiri viongozi wao wa jumuiya na taasisi za kiisilamu wawaongoze,
wakati viongozi wa jumuiya na taasisi za kiisilamu walipofika eneo
hilo walitoka kwenye gari ili kwenda kufanya mazungumzo na askari,
ndipo FFU walipoaza kurusha mabomu ya machozi ovyo na kuwatawanya
waumini hao, huu ni uvunjaji wa katiba zote mbili na ukiukwaji wa haki
ya raia na uhuru wake wa kuabudu kama inavyoelezwa na katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 19 (2) ambayo inasema "Kazi ya
kutangaza dini, kufanya ibada, kueneza dini itakua huru na jambo la
hiari ya mtu binafsi na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini
zitakua nje ya shuguli za mamlaka ya nchi…" rejea pia katiba ya
Jamhuri ibara. 19 (1), (2), (3).

Pia kufanya hivyo ni kwenda kinyume na katiba ya Zanzibar ibara ya 16
(1) kwa kuwazuwia watu kwenda watakapo ndani ya Zanzibar…, sheria kama
hii pia inaelezwa ndani ya katiba ya Jamhuri…

Ibara ya 17(1) inatamka wazi kwamba "…Kila raia wa Jamhuri ya Muungano
anayo haki ya kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano…". Pia kifungu
kidogo cha (2) (b)(i),(ii),(iii) vimetoa maelezo zaidi.

Jeshi la Polisi limekwenda kinyume na kifungu cha  18 (1) cha sheria
ya Zanzibar kwa kuzuwia uhuru wa maoni Sambamba na Kwenda kinyume na
Sheria ya mwaka 1977 ya Jamhuri ya Tanzania ibara ya 18 (1) "…kila mtu
yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta,
kupokea na kutoa habari…"

Isitoshe, juu ya ukiukwaji wote huo askari hao wamefanya unyama na
uhalifu wahali ya juu kwa kuunajisi Msikiti wa Ijumaa wa Mahonda kwa
kuwahujumu Raia wasio na silaha ndani ya Msikiti kwa kuwarushia mabomu
ya machozi yasiojulikana idadi yake ambapo hadi hii leo msikiti huo
hausaliki ndani kutokana na harufu kali ya mabomu. Pia askari hao
walipiga risasi pamoja na kuingia ndani ya Msikiti na viatu na kuvunja
kwa makusudi vyombo (Vespa, Pikipiki, Baskeli n.k) vilivyoegeshwa eneo
la msikiti huo wa Ijumaa.

Sambamba na hilo, polisi wamevunja taa ya mbele na nyuma ya vespa ya
mwandishi wa  habari wa jumuiya pamoja na taa za gari inayobeba vifaa
vya mihadhara kichuki baada ya kuikamata mapema tu na kuifikisha
polisi, hali hii ilitokea wakati gari ikiwa kituoni chini ya kizuizi
cha polisi baada ya kuikamata tokea saa saba nanusu za mchana kabla ya
kufika kwa misafara inayokwenda kwenye mihadhara hadi leo hii gari
hiyo inashikiliwa na polisi kituoni mahonda.

Pia katika jumla ya matukio ni kuandamwa na kufukuzwa kwa gari ya
kiongozi wa Jumuiya ya Maimamu Sh. Farid Hadi Ahmed yenye Namba ya
usajili Z 628 DJ aina ya NISAN X-TRAIL iliyofukuzwa kwa pikipiki
inasadikiwa na watu ambao walitumwa na jeshi la polisi kwa lengo la
uhalifu dhidi ya Amir Farid kitendo ambacho kilisababisha  ajali ya
kupinduka  kwa gari hiyo na kusababisha kujigonga na mti huko Dole
tukio ambalo liliripotiwa kituo cha polisi cha Muembe Mchomeke. Haya
yote yaliyofanywa na Jeshi la Polisi kuwajeruhi watu wasiokua na hatia
pamoja na kuharibu mali  yanakwenda kinyume na katiba na sheria za
nchi.

Jambo la kushtusha zaidi ni kitendo cha kuwadhililisha wanawake na
kufikia hadi kuwakashifu kwa kuwachania nguo zao na kuwavua mashungi
yao pia hata watoto wadogo mitaani wako walopata kipigo, kitendo cha
kuwatimba wanawake kwa viatu bila ya huruma na kuwapiga marungu na
kuwajeruhi vibaya sehemu za usoni na mwilini kwa ujumla, huo wote ni
unyama na ukiukwaji wa haki za binaadamu.

Ilipofikia wakati wa laasiri jeshi la polisi walianza pia kupiga
mabomu ndani ya msikiti wa donge pwani pamoja na kuuhujumu msikiti na
waumini wakiwa wanaswali katika msikiti wa Donge skuli na kuvunja vioo
vya msikiti huo, huu wote ni udhalilishaji wa dini ya Kiislamu pamoja
na waumini katika eneo hilo.

Vile vile, askari wa jeshi la polisi walikata kwa visu mipira ya
vyombo vya wananchi kama vile vespa na baskeli zilizokua zimeegeshwa
msikitini hapo na askari hao walivunja heshma ya msikiti kwa kuingia
na viatu ndani ya misikiti hiyo.

Sambamba na hilo,  walimkamata mzee Kassim Shekha mwenye Umri wa miaka
50 aliekua akiswali swala ya laasir walimjeruhi vibaya miguuni kwa
mlipuko wa bomu la machozi akiwa ndani ya swala, pia kijana Othman Ali
(22) aliamriwa aingie Msikitini na hatimae kujikuta akipigwa kwa
mateke, vibao na kuchaniwa nguo huku akiamriwa lazima atembee kwa
magoti pamoja na wenziwe hadi kituoni Mahonda.

Kwa taarifa tulizozipata kutoka kwa kamishna wa jeshi la polisi
Zanzibar kupitia vyombo mbali mbali vya habari ikiwemo gazeti la
serikali la Zanzibar leo toleo nambari 3789 la tarehe 18 Juni, 2012
lilisema likimnukuu Kamishna huyo ndugu Mussa Ali Mussa eti hakuna
alie jeruhiwa wakati taarifa za kuaminika zimeripoti watu thalathini
na nne ambapo wanaume ni 27 na wanawake 9. Upotoshaji huo wa jeshi la
polisi ni kuonesha namnagani jeshi la Polisi lisivyo wajali wananchi,
roho na mali zao na jinsi linavyopotosha ukweli wa mambo. Pia
kutokujali hata kwenda kinyume na viapo vyao vya uaminifu wanapoingia
kwenye ajira, Kwa kiongozi wa Jeshi la Polisi kwa nafasi kama hiyo ya
kamishna alipaswa awe mfano mzuri kwa walio chini yake.

Matukiyo yote hayo ya kunajisi Misikiti na kudhalilisha waumini wakiwa
ndani ya nyumba za ibada yanazidi kujenga imani kua ni kweli yale
yanaosemwa kua jeshi la Polisi linahusika kwa njia moja au nyengine
katika suala zima la unajisi na uchomwaji wa Makanisa kiushiriki na
ufichaji wa wahalifu kisha kutoa taarifa za uongo na  kuwafanya
Waislamu ndio chaka lao.

Baada ya hayo machache yaliyotangulia hapo juu pamoja na kukutana na
waathirika na wananchi wa Donge, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
inatamka kwamba:

    Jumuiya inasikitishwa sana na taarifa za uongo zisizo kuwa na
ukweli na inalitaka jeshi la polisi na Vyombo vyote vya Dola wafanye
kazi zao kwa ukweli na uaminifu kama wanavyotakiwa kwa mujibu wa
muongozo wa haki za binadamu wakitambuwa umuhimu wa jukumu lao la
kutunza amani na utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu. Kila
mtu anayo haki ya kuwekewa mazingira muafaka ya kitaifa na kimataifa
yatakayomuwezesha kupata haki zake za binadamu. Kwa maana hiyo
tunalitaka jeshi la polisi litueleze kwa katiba gani na sheria ipi
iliyotumika kuzuia uhuru wa kuabudu na kutoa mihadhara na kukusanyika
waumini wa kiisilamu misikitini?
Tunavyofahamu sisi jumuiya, ni kuwa jeshi la polisi na vyombo vingine
vya dola wana jukumu la kuheshimu, kulinda na kutetea haki za binadamu
kwa watu wote bila ya ubaguzi.

    Wananchi wa Donge wanasema wamechoshwa na ubaguzi na udikteta wa
Shamhuna na wanaitaka serikali ya umoja wa kitaifa kupitia baraza la
wawakilishi itoe ufafanuzi wa wazi kabisa, ni kwa sheria gani wananchi
wa Donge wananyimwa fursa ya kufaidi uhuru wa kuabudu na uhuru wa
maoni pamoja na uhuru wa kuchanganyika na ndugu zao wazanzibari? vile
vile haki ya kutumia TV na DVD zao mitaani uhuru ambao unaingiliwa na
masheha kwa kuwazuia watu kutizama watakacho na kufikia hadi kuwatisha
kuwapeleka Polisi na hata kuwanyang'anya mali hizo jambo ambalo
linaweza kusababisha uvunjifu wa amani wakati inafahamika kuwa haki
zote hizo zinalindwa na katiba ya Zanizbar kwenye ibara zifuatazo 17,
18, 19 na 20.

    Wananchi wa Donge pia wanomba ufafanuzi kutoka baraza la
wawakilishi kwani kwa miaka yote wanajiona kuwa wanabaguliwa wakati
wananchi wenzao wa mashamba yote mengine  katika wilaya tofauti
wakipata haki kikamilifu, jee wao si wazanzibari? Ni dhambi gani
waliyotenda hata wakabaguliwa kiasi hicho? Au Donge ni nchi yenye
mfalme kama wafalme wa ki-Misri wakijulikana kwa jina la FIRAUNI?

    Wananchi wa Donge wanaliomba baraza la wawakilishi tukufu ndani ya
siku kumi na nne (14) litoe ufafanuzi wa haki juu ya masuala yao yote,
ikishindakana hivyo wasije wakalaumika kwa maamuzi watakayochukua. Pia
wanaviomba vyama vyote vya siasa viwe makini sana kuwatetea haki zao.

    Jumuiya na taasisi za kiislamu zinawaahidi wananchi wa Donge kuwa
ziko tayari kuwaunga mkono kwa maamuzi yoyote watakayo yachukuwa na
kuwataka waislamu wote wawe tayari kwa hilo.

    Jumuiya za kiisilamu zinawapa pole waathirika wote na kuwapa
hongera wazanzibari wote kwa uimara na kutotetereka katika kudai haki
zao pamoja na kutoa wito wa kudumisha amani na utulivu, pamoja na kuwa
na subra na kutolipiza kisasi.

Mwisho, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu zinapenda ifahamike kwamba,
inatoa na kupaza sauti ya ukombozi wa Zanzibar kwa  njia za amani bila
ya kutumia nguvu za silaha bali  kwa kutumia nguvu za hoja na
inaendesha harakati zake  hizo za ukombozi juu ya misingi ya sheria za
nchi na katiba.

Hivyo basi, wananchi wa Zanzibar kudai uhuru wa kujiamulia mambo yetu
ni haki yetu ya msingi, na kwa hilo HATUNA MJADALA (MPAKA
TUTAKAPOIPATA NCHI YETU INSHA-ALLAH), tutaendelea kudai haki zetu kwa
kila hali bila ya kuvunja sheria za nchi.

Tunasisitiza kuendelea na kuidai Zanzibar yetu huru ingawa tunaelewa
gharama ya kufanya hivyo ni kubwa ikiwemo kupoteza roho zetu na mali
zetu. Na tunatamka wazi yakwamba tumechoka na ukoloni wa watanganyika
wachache wasioitakia mema Tanganyika na Zanzibar.

Tutaidai nchi yetu kwa gharama yoyote  mpaka kuipata Zanzibar yetu
huru.

"…FREE ZANZIBAR…"

"TUACHIWE TUPUMUE"

WABILLLAH TAWFIQ

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com  Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.




0 comments:

Post a Comment