Monday, 11 June 2012

[wanabidii] Kufunga mafunzo ya kikapu kwa vijana chini ya miaka 17 Arusha, 10 Juni 2012

Hotuba ya TBF kufunga mafunzo ya vijana wa chini ya miaka 17 Arusha tarehe 10, Juni 2012.

Mhe Mgeni rasmi John Mongella, Mkuu wa wilaya ya Arusha,
Greg Brittenham kocha toka Marekani,
Ndugu wanamichezo,
Wanafunzi, wazazi, walimu na Makocha,
Wadau wote wa Michezo,

Kwa niaba ya shirikisho la mpira wa kikapu Tanzania (TBF) nakushukuru sana kwa kukubali kuja kufunga mafunzo haya ya vijana wadogo chini ya miaka 17 hapa Arusha.

Awali ya yote tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kumaliza mafunzo haya salama.

Tunawashukuru wote waliotusaidia kufanikisha mafunzo haya wakiwamo watu wa Marekani, Kampuni ya Cocacola, Kocha Greg, Israel Saria wa TanzaniaSports.com na wadau wengine wengi.

Mhe. Mgeni rasmi vijana hawa wamepata bahati ya pekee katika Afrika ya kufundishwa na moja wa makocha bora kabisa duniani wa kikapu.

Kocha Greg ni kocha wa zamani msaidizi wa New York Knicks kwa miaka 20, timu inayoshiriki NBA na amendika vitabu vingi ambavyo vinatumiwa na makocha wengi kufundishia kikapu.

Baadhi ya makocha wetu wazalendo ambao nao wako hapa wakiwemo wa timu zetu za Taifa za kikapu ni dhahiri wamejifunza mengi kutoka kwa Kocha Greg.

Mhe. Mgeni rasmi michezo ni sehemu kubwa sana ya kuongeza utalii na kukuza biashara baina ya mataifa mbali mbali licha ya kusaidia kuimarisha afya na kuwaongezea wachezaji uwezekano wa kufanikiwa zaidi kama watazingatia nidhamu ya mchezo.

Mhe. Mgeni rasmi moja ya sababu ya Greg kuja Tanzania ni hamasa aliyoipata mwaka 1968 wakati wa michezo ya Olympic wakati huo Greg alikuwa mwanafunzi wa shule aliona ujasiri wa Mtanzania John Steven Akhwari jinsi alivyonuia kumaliza mbio za marathoni licha ya kuwa alikuwa ameumia vibaya lakini alijitahidi na kumaliza, John alitangaza jina la Tanzania na leo hii tumepata matunda na kuanzisha uhusiano mkubwa utakawasaidia vijana wetu kupitia michezo.

Kocha Greg alienda Mbulu kumtembelea Mbulu kumtembelea shujaa huyo wa kitanzania ambae vijana wengi hawamfahamu John Steve Akhwari, pia Kocha Greg ametembelea vivutio vyetu vya utalii ikiwemo kupanda na kufika kileleni kwa mlima Kilimanjaro.

Greg ametoa zawadi ya vifaa vya michezo kwa vijana wote hawa 100 na kila mmoja leo amependeza sana na pia ametoa Official Jersey ya New York Knicks yenye jina la Mhe. Rais Kikwete na ameomba tumfikishie Rais nasi tutafanya hivyo mara tutakaporejea Dar Es Salaam.

Mhe. Mgeni rasmi moja ya mambo ambayo tumekubaliana ni kufanya mafunzo haya yawe endeleevu na kuyafikisha sehemu kubwa ya Tanzania.

Kama mipango ikienda vizuri basi baadhi vijana toka Tanzania nao watapata fursa ya kwenda kufanya ziara za mafunzo ya kikapu huko Marekani siku za baadae.

Mhe. Mgeni rasmi tunaomba ukiwa kama mpenda michezo na kijana kusaidia manispaa ya Arusha iweze kuwa na viwanja vingi vya wazo vya mchezo wa kikapu na michezo mingine.

Pia tunaomba usisitize suala la mashule kuwapatia wanafunzi wao haki ya kucheza michezo kwa kuhakiksha shule zinakuwa na viwanja na pia vifaa vya michezo na kipindi cha michezo kinatumiwa ipasavyo mashuleni.

Kwa vijana wote mliokuja kwenye mafunzo haya tunaomba mkawe mabalozi wazuri mkirudi mashuleni kwenu na muonyeshe nidhamu nzuri katika vijwanja, nje ya viwanja , mashuleni na katika jamii zenu pia.
Ili ufanikiwe kupitia kikapu basi ni lazima pia uwe unafanya vizuri darasani, na kuyamudu yote haya ya kucheza na kusoma inabidi muwe na nidhamu nzuri na kufuata maelekezo ya viongozi, walezi, wazazi na walimu wenu.

Sisi kama shirikisho la mpira wa kikapu Tanzania tutaendelea kuwatengenezea program mbalimbali na kuunga mkono clinic nyingi kama hizi ili tuwe na vijana wengi walifundishwa vizuri ili tuzalishe na kuibua vipaji lakini pia baadae tuwe na timu bora za ngazi ya Taifa na vilabu pia.

Mhe. Mgeni rasni tunaomba utumie nafasi yako kusaidia kutatua changamoto zilizoainishwa na nyingine ambazo hatujazitaja ili kwa pamoja tuweze kuwaendeleza vijana wetu kupitia mchezo wa kikapu.

Nawashukuru wote kwa ushirikiano wenu na nawatakia kila heri.

Phares Magesa
Makamu wa Rais-TBF.
Arusha, 10 Juni, 2012.
-------------------------------------

Katika nasaha zake za kufunga Clinic hii Mhe Mkuu wa wilaya ya Arusha John Mongela aliwashukuru wote waliofanikisha ikiwemo watu wa Marekani, Cocacola , Kocha Greg na wengine wote.

Mhe. Mkuu wa wilaya alisema aliposikia Kocha Greg amekuja hakuamini kwa sababu sio kitu rahisi na ni bahati ya pekee kwa vijana wa kitanzania kupata kufundishwa na kocha aliyefundisha NBA.

Mhe. Mongella aliwaambia vijana hawa kuwa yeye pia ni mpezni wa kikapu na aliwahi kuishi New York siku za nyuma, hivyo anajua umuhimu wa kocha huyu

Hivyo aliwaomba vijana hawa wazingatie mafunzo waliyoyapata na aksema hii ni historia katika maisha yao, kwani wako vijana wengine wako Marekani lakini hawapati bahati kama waliyopata hawa vijana wa Arusha.

Mkuu wa Wilaya alikiri tatizo kubwa la viwanja na kuahidi kulifanyia kazi, pia alisema atajaribu kushirikiana na wadau wote walioko Arusha ili wasaidie kuinua mchezo wa kikapu.

Mkuu wa wilaya aliahidi kusaidia timu zote za Arusha pale zitakapokuwa zinatakiwa kushirikia mashindano ya Kitaifa.

Mhe. Mkuu wa wilaya alihimiza michezo mashuleni na kuomba walimu wawape nafasi vijana ili waonyeshe vipaji vyao mashuleni ikiwa ni pamoja na kuhimiza kila shule iwe na viwanja na walimu wa michezo.

Pia mkuu wa wilaya aliwaasa vijana wazingatie masomo darasani, michezo viwanjani na kudumisha nidhamu muda wote.

Mhe. Mongella alimuomba Kocha Greg aje tena Arusha na akaitangaze vyema Tanzania ili tuweze kuvutia watalii wengi zaidi.

Na mwisho alitamka kuafunga rasmi mafunzo haya.
------------------------------------------------
Mwisho.
-------------------------------------------------
Attached are some event photos.

Sent from my BlackBerry® smartphone provided by Airtel Tanzania.

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment