Wednesday, 4 July 2012

[wanabidii] HOTUBA YA KAMBI YA UPINZANI WIZARA YA MALIASILI UTALII NA MAZINGIRA 2012/2013

*HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI WIZARA YA MALIASILI
UTALII NA
MAZINGIRA MHESHIMIWA MCH. PETER MSIGWA KUHUSU MPANGO WA OFISI YA
MAKAMU WA
RAIS MAZINGIRA WA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013* *1:
UTANGULIZI* *

Mheshimiwa Spika,* kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani,nakushukuru
kwa
kunipa nafasi hii ya kuwasilisha Maoni na Mapendekezo ya Kambi yetu
kuhusu
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa
mwaka
wa fedha 2011/2012, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(3) na
(7)
toleo la 2007.
*
Mheshimiwa Spika,* nachukua fursa hii kumsifu, kumtukuza na kumshukuru
Mwenyezi Mungu, mwenye nguvu na hekima tele kwa kunipa afya njema na
kuendelea kunipigania siku kwa siku. Nichukue nafasi hii pia
kuwashukuru
watumishi wa Mungu popote pale walipo ndani na nje ya nchi, kwa maombi
yenu
yanayonifanya niendelee kuchapa kazi ya kulijenga taifa, naomba
msichoke
kuniombea mtumishi mwenzenu na Taifa letu kwa ujumla.
*
Mheshimiwa Spika, *kwa nafasi ya kipekee kabisa napenda kuishukuru
familia
yangu, na hasa mke wangu mpenzi Victoria, kwa upendo na sala zao
kwangu. Na
huko waliko naomba niwakumbushe tena kuwa, *thamani ya utu wetu hapa
duniani haitatokana na kile tunachokichuma katika jamii, bali
itatokana na
kile tunachokitoa kwa jamii.* Naisihi familia yangu iendelee kuniunga
mkono
wakati wote ninapokuwa mbali, nikishughulikia kero na matatizo ya
wananchi
wa Iringa Mjini na taifa kwa ujumla.

*Mheshimiwa Spika*, kwa moyo wa dhati na kwa unyenyekevu mkubwa,
nawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Iringa Mjini kwa kunielewa,
kushirikiana nami na kuendelea kuniamini na hatimaye kuendelea
kulijenga
jimbo letu na taifa kwa ujumla. Niwashukuru sana kwa kunitia moyo,na
hasa
ninapokuwa nafanya ziara hapo jimboni. Niwaombe Wana Iringa kamwe
tusiruhusu akili ndogo kutawala akili kubwa katika jimbo letu. Mungu
awabariki, sita wangusha.
*
Mheshimiwa Spika, *shukrani na pongezi zangu za dhati pia nazielekeza
kwa
viongozi wakuu wa CHADEMA, kwa kukiongoza vema chama chetu na kuwa
tumaini
pekee na la uhakika la Watanzania wengi.
*
Mheshimiwa Spika*, kabla ya kuanza kueleza yale yote ambayo Kambi ya
Upinzani inaona ni muhimu kuyatoa, nitoe dira ya Taifa ya sekta nzima
ya
mazingira inayosema kuwa *"Tanzania yenye mazingira salama, yenye afya
na
endelevu"**. *Jambo muhimu la kujiuliza ni; je, Serikali inaendana
kivitendo na dira hii ya Taifa?
*
2.0. Mabadiliko ya Tabia Nchi*
*
Mheshimiwa Spika, *uharibifu na uchafuzi wa mazingira umesababisha
mabadiliko ya tabia nchi ambayo kwa jumla huathiri mfumo mzima wa hali
ya
hewa. Matokeo ya kuathirika kwa mfumo wa hali ya hewa ni kuongezeka
kwa
joto duniani, viwango vya mvua kutokuwa na mpangilio jambo ambalo
husababisha ukame na mafuriko na hivyo kuathiri maisha ya wananchi.
*
Mheshimiwa Spika*, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu duniani na
kwa
maana hiyo kuongezeka kwa shughuli za binadamu na hivyo kusababisha
uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa. Mabadiliko ya tabia nchi
duniani,
ambayo kwa ujumla yamesababisha ongezeko la joto, kupungua kwa viwango
vya
mvua, yameathiri sana ubora wa ardhi , upatikanaji wa maji safi na
salama,
upatikanaji wa chakula kwa wanyama na binadamu na hivyo kusababisha
vifo
kwa viumbe hai ulimwenguni.
*
Mhwashimiwa Spika,* mabadiliko hayo ya tabianchi yamesababisha kina
cha
bahari kupanda kwa sentimeta 17 juu ya usawa wa bahari kwa kipindi cha
miaka 100 iliyopita, joto la dunia kuongezeka kwa nyuzi joto 0.74
centigrade kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita ,pia gesi ya joto aina
ya
karbon dioxide limeongezeka sana .
*
Mheshimiwa Spika, *mwaka 2011 katika kukabiliana na tabianchi Serikali
iliandaa mkakati wa taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na
miradi miwili iliyotekelezwa ni mradi wa kuhimili mabadiliko ya
tabianchi
katika sekta za kilimo, maji, afya, wanyamapori, misitu, mifugo ,
ardhi na
mpango wa kupunguza uzalishaji wa ukaa itokanayo na ukataji wa miti na
uharibifu wa misitu.
*
Mheshimiwa Spika*, Kambi ya Upinzani tunataka kupata taarifa za kina
kuhusiana na utekelezaji wa miradi hii na hatua ambazo zimeweza
kufikiwa
mpaka sasa katika kukabiliana na hali hii nchini mwetu.
*
Mheshimiwa Spika*, ni dhahiri kwamba bila mazingira rafiki, maisha ya
binadamu hayana nafasi hapa duniani. Mazingira ndio msingi wa shughuli
zote
anazofanya binadamu katika kutegemeza maisha yake. Hali kadhalika,
mazingira ni nyenzo ya msingi kabisa katika kujenga uchumi wa taifa.
Hivyo,
ili binadamu aweze kuishi duniani na kujishughulisha na kazi
mbalimbali za
kutegemeza maisha yake na kujenga uchumi wa Taifa lake, ni lazima
mazingira
yalindwe ili yaweze kukidhi mahitaji ya binadamu.
*
2.1 Mkutano wa RIO +20 .*
*
Mheshimiwa Spika, *ni hivi majuzi tu ulimwengu mzima ulikuwa kwenye
mkutano
ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa uliokuwa ukijadili masuala mbalimbali
kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi ambao ulifanyika nchini Brazili
na
kupewa jina la RIO +20. Mkutano huu ulikuwa na maazimio mbalimbali juu
ya
mbinu na mkikakati ya kukabiliana na hali hii na serikali yetu iliweza
kuwakilishwa na Mheshimiwa Makamu wa rais , Mawaziri wa Mazingira
Muungano
na kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar .
*
Mheshimiwa Spika,* Mkutano wa mwaka huu ulijadili kuhusu maazimio ya
mwaka
1992 na namna yalivyotekelezwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa
wapatao 182. Sambamba na hilo mkutano huu ulipitisha maamuzi mapya
kuhusu
kuiweka dunia na mazingira yake katika hali ya usalama ili yaweze
kusaidia
vizazi vya sasa bila kuathiri haki ya vizazi vijavyo.
*
Mheshimiwa Spika*, lengo la mkutano huu lilikuwa ni pamoja na ufanisi
wa
nishati na mchango maradufu wa nishati mbadala kwa wote – ifikapo
mwaka
2030. Zaidi ya mashirika 50 ya serikali kutoka Afrika, Asia, Amerika
Kusini
na mataifa ya visiwa vidogo yalikubaliana kutilia mkazo jambo hilo.
*
Mheshimiwa Spika*, moja ya azimio kuu la mkutano huo lilikuwa ni
kuanzishwa
kwa mfuko utakaowezesha kuharakisha upatikanaji wa nishati, usalama wa
chakula, maji na usafiri endelevu kwa nchi mbalimbali hususan zile
maskini.
Na katika mkutano huo zilitolewa taarifa kuwa kiasi cha Dola bilioni 5
na
ahadi ya dola zaidi ya 700 bilioni zilitolewa kwa ajili ya kuufadhili
mfuko
huu.
*
Kambi ya upinzani,* inataka kupata majibu kuhusiana na mambo yafuatayo
ili
kuondokana na tabia ya nchi yetu ya muda mrefu ya kuhudhuria mikutano
na
makongamano mbalimbali lakini hakuna utekelezaji wa maazimio husika ;

i. Je, tumejiandaa vipi kama taifa ili kuweza kunufaika na fedha za
mfuko
huu? Tumeweka mpangomkakati gani?

ii. Je, tunajiandaa vipi kuweza kulitekeleza kwa vitendo azimio la
kupata
na kutumia nishati mbadala, upatikanaji na usalama wa chakula, maji na
usafiri endelevu nchini mwetu?

iii. Je, bajeti yetu ya mwaka huu wa 2012/2013 imezingatia azimio
hilo?
*
3.0 UHARIBIFU NA UCHAFUZI WA MAZINGIRA NCHINI*
*
Mheshimiwa Spika*, kwa kuwa mabadiliko haya ya tabia nchi
yanasababishwa na
uchafuzi mkubwa wa mazingira unaosababishwa na uzalishaji mkubwa wa
gesi
ukaa kutoka katika viwanda vikubwa katika nchi zilizoendelea
kiviwanda, na
uharibifu na uchafuzi mkubwa wa mazingira unaofanywa katika nchi
zinazoendelea kwa kukata miti hovyo, uchimbaji wa madini usiojali
mazingira, utupaji wa taka hovyo hasa katika miji nk. na kwa kuwa
athari za
uharibifu na uchafuzi huu wa mazingira unaifanya dunia isewe mahali
pazuri
pa kuishi, ni dhahiri kwamba kunahitajika jitihada za kitaifa na
kimataifa
kukabiliana na tatizo hili.
*
Mheshimiwa Spika*, Pamoja na nchi yetu kutambua umuhimu wa Mazingira
na
hivyo kuunda Wizara mahsusi ya mazingira chini ya ofisi ya Rais, na
kutunga
Sera ya Mazingira ya Mwaka 1998 na kuridhia mikataba mbalimbali ya
kimataifa kuhusu utunzanji wa Mazingira mfano Agenda 21, bado nchi
yetu ina
tatizo kubwa la uchafuzi wa mazingira.
*
Mheshimiwa Spika*, nchi yetu inaelekea kuwa jangwa kutokana na ukataji
miti
hovyo bila kupanda mingine, miji yetu imezidi kuwa michafu jambo
ambalo ni
hatarishi kwa afya za wananchi wetu. Kambi ya Upinzani inaitaka
Serikali
ieleze ni kwa nini tuipatie fedha Wizara hii ya Mazingira wakati
mazingira
yanaendelea kuharibiwa na kuchafuliwa kila kukicha?
*
3.1 Kuteketea kwa misitu na miti Nchini*
*
Mheshimiwa Spika*, ukataji miti na uchomaji wa misitu Tanzania
umeendelea
kwa kiwango kikubwa sana. Maeneo yaliyoathirika kwa kiwango kikubwa ni
yaliyoko katika Mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga, Pwani, Mwanza,
Mara na
Tabora. Sababu kubwa za uchomaji huu wa misitu ni kwa ajili ya
shughuli za
kilimo, kutafuta nishati hasa mkaa na kuni kwa matumizi ya kupikia na
upasuaji wa mbao.

*3.2 Usimamizi wa Misitu Nchini*

Mheshimiwa Spika, taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali
kuhusu ukaguzi uliofanyika kuhusiana na utendaji wa kifedha na
matumizi ya
fedha za Usimamizi wa Misitu (PFM) kwa mwaka wa fedha wa 2010/2011
umebaini
kuwa kulikuwa na fedha za mradi kiasi cha Sh. 178,826,876 katika
Halmashauri kumi na moja (11) ambazo hazikutumika hadi mwisho wa mwaka
ulioishia tarehe 30Juni, 2011. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali
kueleza
kama fedha za usimamizi hazikutumika, ni kwa vipi wilaya tajwa
zilifanya
kazi ya usimamizi wa misitu wakati fedha hazikutumika?

*Mheshimiwa Spika*, kukosekana au kutokutolewa kwa fedha za usimamizi
ndio
sababu kubwa ya kuongezeka kwa ukataji wa misitu na uchomaji mkaa.
Aidha,
umekuwa ni muda mrefu sana kwa uharibifu wa mazingira katika msitu wa
Shengena uliopo Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro ambapo yupo
mwekezaji
ambaye ameingia kwenye makubaliano na Halmashauri ya Kijiji cha
Marieni,
Kata ya Chome kuhusu uchimbaji wa udongo wa *Bauxite *ambao umekuwa
ukisafirishwa kwenda nchi ya jirani ya Kenya. Suala hili bado lipo na
linaendelea na limesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na
kusababisha
ukame katika vijiji vya jirani vya Bwambo, Tae, Malindi, Gonjanza na
Kata
ya Chome kwa ujumla.
*
Mheshimiwa Spika,* kuna dalili zote za nchi hii kugeuka kuwa jangwa
hasa
baada ya Serikali hii ya CCM kupandisha ushuru wa mafuta ya taa ili
kukabiliana na tatizo la uchakachuaji wa mafuta ya dizeli. Hii ina
maana ya
kwamba wananchi watashindwa kumudu bei ya mafuta ya taa kama nishati
mbadala na hivyo watageukia miti na misitu kujipatia nishati hiyo. Hii
ina
maana Serikali ya CCM inavyoendelea kutatawala ndio jinsi ambavyo nchi
yetu
inaendelea kuwa jangwa. Kambi ya upinzani inapinga utawala wa namna
hii na
tunatoa wito kwa wananchi pia kukataa kuongozwa na Serikali
inayowaelekeza
jangwani.

*3.3 Uchimbaji wa Madini na Hatima ya Mazingira Tanzania.*
*
**Mheshimiwa Spika,* ni ukweli uliowazi kuwa kutokana na shughuli za
utafutaji na uchimbaji wa madini ya aina mbalimbali hapa nchini mwetu
zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kuharibu mazingira yetu ,na hili
linathibitishwa na ripoti mbalimbali za kiutafiti zilizotolewa
kuhusiana na
mahusiano yaliyopo baina ya uchimbaji wa madini na uharibifu wa
mazingira.
*
Mheshimiwa Spika,* kwa kiasi kikubwa sana madhara makubwa zaidi
husababishwa na shughuli za uchimbaji unaofanywa na makampuni makubwa
na
yenye zana za kisasa, ikilinganishwa na kiwango kinachofanywa na
wachimbaji
wadogo wadogo.

*Mheshimiwa Spika,* ripoti mbalimbali zimeonyesha kuwa wananchi pamoja
na
viumbe mbalimbali waishio karibu na migodi mikubwa ya uchimbaji wa
madini
nchini mwetu zimeonyesha kuwa wananchi na viumbe wamekuwa wakiathirika
sana
, mathalani mgodi wa Barrick North Mara,Geita Gold Mine na migodi
mingine
mikubwa nchini mwetu.
*
Mheshimiwa Spika*, tathmini ya athari ya mazingira katika migodi
mikubwa
imekuwa ikifanywa baada ya miradi kuidhinishwa badala ya miradi
kufanywa
kabla. Hivyo thamini hizi hazisaidii kudhibiti athari za mazingira kwa
kuwa
tathmini haziathiri usanifu miradi. Miradi kama Geita Mine na North
Mara
imegeuka kuwa majanga ya kimazingira kwa sababu hii.

*Mheshimiwa Spika, **Kambi ya Upinzani inasikitishwa na uchafuzi
mkubwa wa
mazingira uliofanyika katika Migodi ya Dhahabu ya Geita na North-Mara
ambao
umeleta athari kubwa sana za kiafya kwa wananchi wa maeneo hayo.*
*
Mheshimiwa Spika**, kwa mujibu wa utafiti wa Manfred Felician Bitala
(2008)
na tafiti zilizofanywa chini ya ufadhili wa Norwegian University of
Life
Scieces na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(2009) na Utafiti uliofanywa na
Idara ya Biolojia, Chuo Kikuu cha Oslo(2011) kuhusu Uchafuzi wa
Mazingira
Geita na North-Mara ni kwamba kuna kiasi kikubwa sana cha kemikali-
sumu
(kwa mfano "cyanide") madini ya zebaki (Mercury) na madini chuma yenye
sumu
(heavy metals) katika maji na udongo katika maeneo ya makazi ya
wananchi wa
maeneo yaliyozungukwa na migodi hiyo.*
*Mheshimiwa Spika,** kwa mujibu wa matokeo ya tafiti hizi ni kwamba
wananchi wa maeneo hayo wameathirika vibaya na kemikali hizi zenye
sumu kwa
viwango vya juu sana kuliko athari za wastani za waathirika katika
nchi
nyingine zenye tatizo kama hilo. Aidha hata mifugo ya wananchi hawa
imeathirika kwa kiasi kikubwa sana.*
*
**Mheshimiwa Spika,** Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iingilie
kati na
kunusuru maisha ya wananchi wa maeneo hayo ya migodi. Aidha Kambi ya
Upinzani inataka kujua kama Serikali ina taarifa ya tafiti hizi na
imechukua hatua gani hadi sasa kudhibiti uchimbaji wa madini ambao si
rafiki kwa mazingira. Kadhalika, Kambi ya Upinzani inataka kuelewa
fidia
kwa watu wote walioathirika na uchafuzi huo wa vyanzo vya maji
wanayotumia
utafanyika lini?*
*
Mheshimiwa Spika,* ni kutokana na hali hii ndio maana tunakubaliana na
tamko la kamati ya viongozi wa dini na asasi za kiraia lijulikanalo
kama
tamko la Ngurdoto la tarehe 20 Octoba 2011 na tunaitaka serikali kuwa
tayari kufanya haya yafuatayo;

i. Ni muhimu utafiti na taarifa za madhara kwa mazingira na jamii
kutokana
na shughuli za uchimbaji wa madini ziwe zinaandaliwa na taasisi au
wataalamu wanaoaminika na kuheshimika ambao wako huru kufanya kazi zao
bila
kuingiliwa na serikali na wawekezaji binafsi. Utafiti huo ufanywe mara
kwa
mara wakati shughuli za uchimbaji zinaendelea na baada ya shughuli
hizo
kusitishwa.

ii. Ni dhahiri kuwa uharibifu wa mazingira kutokana na uchimbaji wa
madini
utaathiri pia vizazi vijavyo, na unaweza kuzisababishia jamii hizo
kuishi
maisha ya dhiki na mashaka. Kutokana na hilo, ni lazima kufanya
utafiti
kuhusu madhara yote ambayo yanaweza kutokea siku zijazo kutokana na
shughuli za uchimbaji wa madini na kuhakikisha kunakuwa na njia za
kuwafidia ipasavyo watu wote watakaoathirika;

iii. Jamii zinazoishi karibu na migodi ya madini, pamoja na wale ambao
wameondolewa kwenye maeneo yao ya asili kupisha uchimbaji madini, mara
nyingi wamekuwa wakisahaulika na kuna haja ya kuhakikisha kuwa nao
wanafaidika na shughuli hizi kwa kuwezeshwa katika kujenga maisha yao
na
haswa kutokana na uharibifu wa mazingira uliofanywa.

iv. Uharibifu wa mazingira kutokana na shughuli za uchimbaji madini
unaathiri sana jamii katika maeneo ya uchimbaji na nchi nzima kwa
jumla,
lakini jukumu la kurekebisha mazingira haya linaachwa kwa serikali na
si
kwa wachimbaji. Kampuni za uchimbaji madini zinapaswa kuwa na jukumu
la
kurekebisha na kutengeneza mazingira bora baada ya kukamilika kwa
shughuli
zao.

v. Serikali itoe ufafanuzi wa kina na wa kueleweka katika suala la
fidia,
kwa kuainisha kiwango mahsusi cha fidia kwa watu na jamii ambazo
zimeathirika na sumu zinazotokana na shughuli za uchimbaji wa madini
na
uharibifu wa mazingira yao;

vi. Serikali ihakikishe kuwa ni lazima jamii zinapewa taarifa muhimu
na
kuwezeshwa kushiriki kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na kuwa
suala
hilo liwekwe kwenye sheria na si hiari kutokana na matakwa ya
makampuni au
serikali.

*3.4 Madini ya Urani (uranium).*

*Mheshimiwa Spika,* taarifa za kugunduliwa kwa madini ya *urani
*katika
nchi yetu ni habari njema kwa kuwa madini haya yatakuwa na mchango
mkubwa
katika uchumi wetu. Kwa kuwa madini haya yanahitaji uangalifu mkubwa,
kwa
sababu ya kuwa na asili ya sumu, Serikali imejiandaa vipi kisera,
kisheria
na kiutaratibu kuhakikisha kuwa uchimbaji wa madini hayo hauathiri
mazingira na afya za wananchi na wanyama katika maeneo hayo?
*
Kambi ya Upinzani* inaitaka Serikali kujiandaa vema katika suala hili
la
madini ya urani na gesi mapema kabla ya kuingia mikataba na wachimbaji
ili
kuepuka migogoro isiyo ya lazima hasa pale wananchi na mazingira kwa
ujumla
watakapoathirika na uchimbaji huo. *

4.0 UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO NA MAZINGIRA*

*Mheshimiwa Spika*, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, pamoja na
mikakati
mingine, una mkakati mahsusi wa *kuboresha muindombinu ya usafi katika
maeneo ya mijini na vijijini.* Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo mwaka
huu
wa fedha zilipaswa kutengwa kiasi cha shilingi billioni *7.620* kwa
ajili
ya kampeni ya Taifa ya Mazingira safi na kusafisha shule. La
kushangaza ni
kuwa ukisoma taarifa ya waziri kuhusiana na idara ya mazingira malengo
ya
mwaka 2012/13 (uk.41) hakuna kipengele hata kimoja ambacho kimelenga
kutekeleza malengo haya ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano kwa
kuwa
hakuna fedha iliyoombwa kutekeleza Mpango wa Maendeleo.

*Mheshimiwa Spika*, huu ni ushahidi wa wazi kuwa Serikali haina nia ya
dhati ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo. Kama Serikali inajiwekea
Mpango
wake wa Maendeleo, halafu Serikali hiyohiyo inashindwa kutekeleza
Mpango
wake yenyewe, Kambi ya Upinzani na wananchi wenye kupenda maendeleo
tunapata wasiwasi na uwezo wa Serikali hii ya CCM kuendelea kuongoza
nchi
yetu kwani hata mipango inayojiwekea yenyewe inashindikana
kutekelezeka.

*Mheshimiwa Spika*, fedha kwa ajili ya matumizi ya maendeleo
zilizotengwa
kwa mwaka huu wa fedha ni shilingi bilioni 7.07 na kati ya hizo fedha
za
ndani ni kiasi cha shilingi bilioni 1.3 tu (randama uk .46) na
nyingine
tunategemea kuzipata kutoka nje, na miradi ambayo inaenda kutekelezwa
ni
miradi namba 5306, 6569, 6571, 5301, 5302, 5305 na 6504. Kati ya
miradi
yote hii hakuna hata mmoja unaohusiana na kuboresha miundombinu ya
usafi
mijini na vijijini.
*
Mheshimiwa Spika, *Kambi ya Upinzani inaiasa Serikali kutofanya mzaha
na
Mpango wa Maendeleo ambao una maslahi kwa wananchi. Kitendo cha
kutotenga
fedha kuboresha miundombinu ya usafi mijini na vijijini kama Mpango
ulivyoelekeza na kutozingatia vipaumbele vya Mpango wa Taifa wa
Maendeleo
ni dharau na dhihaka kwa wananchi. Kwani suala la mazingira ni suala
la
afya. Mtu anayekaa katika mazingira machafu anawezaje kuwa na afya
bora na
kufanya kazi ili alipe kodi kwa Serikali? Serikali sasa iwekeze katika
usafi wa Mazingira ili ikusanye kodi katika mazingira safi vilevile.
Serikali isilenge tu kukusanya isiko wekeza.

*5.0 UTEKELEZAJI WA MAAGIZO YA BUNGE*
*Mheshimiwa Spika,* katika bunge la bajeti lililopita kamati ya bunge
ya
maliasili na mazingira ilitoa maagizo mbalimbali na kati ya maagizo
hayo
yapo ambayo hayajatekelezwa na serikali mpaka wakati huu. Mojawapo ya
maagizo hayo ni *Agizo namba 4 – ambalo linasema "serikali itenge
fedha za
kutosha ofisi ya makamu wa rais mazingira katika bajeti ya 2012/13 ili
kuwezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na utunzaji wa
mazingira*".
Ila uhalisia ni kuwa fedha zilizotengwa ni kidogo sana na hii
inaonyesha
kuwa pamoja na serikali kutokuthamini mazingira pia haitekelezi
maagizo na
maazimio mbalimbali ya bunge. (Randama ya Ofisi ya Makamu wa Rais uk.
26)
*
Mheshimiwa Spika*, agizo lingine ni Agizo namba 5ambalo lilisema*
"serikali
ihakikishe kwamba fidia zote stahiki kwa wananchi wanaozunguka mgodi
wa
dhahabu wa North Mara zinalipwa na ahadi zilizotolewa na mwekezaji wa
mgodi
kwa jamii ya eneo husika zinatekelezwa".* Taarifa ya serikali ya
Januari -
Mei 2012 inasema kuwa jumla ya wananchi 474 wamelipwa jumla ya
shilingi *
22,387,234,156/=* ikiwa ni fidia zao kwa maeneo yaliyopo ndani ya mita
200
kutoka kwenye mgodi. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya serikali kuhusu
utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 (Randama uk 26).
*
Mheshimiwa Spika,* taarifa hizi za serikali sio sahihi kwani kwa
wastani ni
kuwa kila mwananchi amelipwa kiasi cha shilingi *47,230,451.* Kambi ya
Upinzani inaitaka serikali kueleza kwa kina ni lini fedha hizi
zililipwa na
zililipwa kwa kutumia utaratibu gani? Ni vigezo gani vilitumika katika
kuwateua wananchi waliopaswa kulipwa fidia hii ?
*
Mheshimiwa Spika,* katika bunge la mwezi februari 2012 siku ya tarehe
03/02/2012 wakati Naibu waziri wa Nishati na madini Adam Malima
akijibu
swali namba 48 la Mheshimiwa Ester Matiko kuhusiana na fidia kwa
wananchi
hawa alisema, naomba kunukuu hansard *"**Mheshimiwa Naibu Spika,…...
Pamoja
na kufanyika tathmini kwa kaya zinazozunguka mgodi, kumejitokeza
matatizo
mbalimbali; mfano, kaya tano hazijaridhia kufanyika kwa tathmini hiyo
ya
fidia. Majadiliano yanaendelea kwa kushirikisha Kijiji cha Nyangoto.
Familia 40 ziliamua kurudi katika maeneo waliyokwishalipwa na kwa sasa
wanadai fidia upya.

……..Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi la kulipa fidia kwa Wananchi
wanaotakiwa
kupisha shughuli za Mgodi wa North Mara linasimamiwa na Serikali
katika
ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime". *
*
Kambi ya Upinzani,* tunataka maelezo ya kina juu ya taarifa hizi, na
kukinzana kwa taarifa za Serikali na zile za wananchi kuhusiana na
ulipaji
wa fidia kwa wananchi. Tuchukue jibu lipi ? Lililopo kwenye hansard,
la
wananchi au la waziri mwenye dhamana ya mazingira?

Fidia hizi zililipwa kwa ajili ya fidia ya uchafuzi wa mazingira
uliofanywa
na mgodi wa North Mara kwa wananchi hawa au ni fidia ya aina gani hii?
*
Mheshimiwa Spika,* taarifa hiyohiyo ya serikali inasema kuwa visima
vya
maji 16 vimechimbwa katika vijiji vya Kewanja, Nyamwaga, Nyakunguru,
Genkuru, Kerende, Matongo na Nyangoto na kuwa kati ya visima hivyo ni
visima 14 ndio vinatoa maji.
*
Mheshimiwa Spika*, taarifa ni kuwa mwekezaji kwenye mgodi wa North
Mara
ameweka utaratibu wa kusambaza maji kwa wananchi kwa kutumia magari.
Kambi
ya Upinzani inajiuliza kama visima vimechimbwa na kuwa vinatoa maji ni
kwa
nini magari yatumike kusambaza maji tena kwa ratiba maalum?
*
5.1 Mbinu za kuhifadhi mazingira yetu.*

*Mheshimiwa Spika*, kuhusu kutunza na kulinda mazingira yetu, Kambi ya
Upinzani inaona kuwa Serikali haijaweka suala la kutunza na kulinda
mazingira katika vipaumbele vyake, jambo ambalo ni hatari kwa mifumo
ya
ikologia na maisha ya binadamu na viumbe hai vingine kwa ujumla. Hili
ni
janga kubwa na Serikali inapaswa kuzinduka sasa na kuchukua hatua za
kukabiliana na janga hili. Kama kawaida Kambi ya Upinzani tunawapa
Serikali
bila choyo mbinu za kufanya kukabiliana na tatizo kama ifuatavyo:

i. Serikali ihimize na ijenge mazingira wezeshi ya kutumia nishati
mbadala
na hasa kwa kutumia vyanzo vya upepo, jua na umeme vijijini na hii
itasaidia kuokoa miti mingi ambayo hutumika kwa ajili ya nishati na
Serikali igharimie uwepo na upatikanaji wa nishati hizo. Hii inatokana
na
ukweli kuwa ni asilimia 14 tu ya Watanzania ndio wameunganishwa kwenye
umeme wa gridi ya Taifa;

ii. Gharama za vifaa vya ujenzi ipunguzwe, na hii ni kwa vifaa kama
sementi ili wananchi waweze kujenga nyumba kwa kutumia tofali badala
ya
kutumia miti na hii itaokoa asilimia kubwa ya miti ambayo hutumika kwa
ajili ya ujenzi;

iii. Itolewe elimu ya kina katika kupanda miti na kutunza miti pamoja
na
misitu iliyopo kwani hali hii isipochukuliwa hatua madhubuti sehemu
kubwa
ya taifa itageuka jangwa. Ukame uliokithiri maeneo mbalimbali ya nchi
ni
kiashiria cha unyemelezi wa jangwa.

iv. Mitaala ya Shule za Msingi na Sekondari ibadilishwe na iweke
msisitizo
katika umuhimu wa kupanda miti na kutunza miti. Hili litasaidia katika
kizazi kinachokuja kujua umuhimu huu wa miti katika maisha yao na
maisha ya
vizazi vijavyo;

v. Watendaji wa Vijiji, Mitaa na Kata kote nchini, moja ya majukumu
yao
liwe ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapanda miti na hiki kiwe ni
kipimo kimojawapo katika kupima utendaji kazi wa viongozi hawa; na

vi. KilaHalmashauri nchini itenge fedha kwa ajili ya kununua miche ya
miti
na kuigawa bure kwa wananchi kila kipindi cha masika kwenye maeneo
husika
na Watendaji wa Vijiji, Mitaa na Kata wagawe miche hiyo kwa kila kaya
na
kila mwananchi apande miche hiyo.

vii. Usafi mijini uwe ndio kipimo cha utendaji wa Mameya wa miji na
majiji.
*
Mheshimiwa Spika,* mwisho kabisa na kwa umuhimu napenda kuchukua
nafasi hii
kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Mhe.
James
Lembeli (Mb) pamoja na wajumbe wa kamati hii kwa ushirikiano katika
kutetea
maslahi ya taifa.
*
Mheshimiwa Spika*, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi ya
Upinzani,
nawashukuru waheshimiwa wote kwa kunisikiliza,
*
Mheshimiwa Spika*, naomba kuwasilisha.

*……………………………………*
*Mch. Peter Msigwa (Mb)*
*Msemaji Mkuu Kambi ya Upinzani- Wizara ya Maliasili, Utalii na
Mazingira*
*04.07.2012*

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment